Hipatia wa Aleksandria

Hipatia wa Aleksandria (370 - 415) alikuwa mtaalamu wa kike wa hisabati, astronomia na falsafa nchini Misri. Alikuwa kati ya wanawake wa kwanza waliotambuliwa kuwa mtaalamu katika hisabati, falsafa, na astronomia (elimu ya anga na nyota). Alikuwa kati ya viongozi wa harakati ya Uplatoni Mpya katika falsafa iliyopanua mafundisho ya mwanafalsafa Plato wa Ugiriki ya Kale. Aliuawa na kundi la Wakristo wenye itikadi kali wakati wa vurugu ya kidini na ya kisiasa jijini Aleksandria.

Hipatia alizaliwa huko Aleksandria, wakati ule mji mkubwa wa Misri. Wakati wa Hipatia, Aleksandria ilikuwa na kimoja kati ya vyuo bora duniani pamoja na maktaba mashuhuri ya Aleksandria. Baba yake alikuwa mwanahisabati Theon anayekumbukwa kwa masahihisho ya muswada wa Euklides na maelezo juu ya Ptolemaio. Kwa kipindi fulani alikuwa pia mkuu wa chuo cha Aleksandria.

Muswada wa Euklides uliohaririwa na Theon, baba yake Hipatia.

Mwalimu wa falsafa, hisabati na astronomia Edit

Hipatia alianza kufundisha fani zake alipokuwa na umri wa miaka michache juu ya 20. Ustadi wa Hipatia ulikuwa maarufu alikuwa na wanafunzi kutoka pande mbalimbali za Dola la Roma. Alitoa mihadhara nyumbani kwake, chuoni na pia hadharani. Alifundisha juu ya astronomia, hisabati na falsafa. Aliandika vitabu kadhaa juu ya hisabati, alihariri pia muswada wa Almagesti ya Ptolemaio.[1][2] [3]

Kati ya wanafunzi wake kulikuwa na Wakristo, Wapagani na Wayahudi. Synesio aliyekuwa baadaye askofu wa Kirene alikuwa mwanafunzi wa Hipatia. Barua zake zinatupa habari muhimu zaidi juu ya maisha yake na mafundisho yake. Alimfundisha Synesio juu ya ujenzi wa astrolabi, kifaa cha kupimia mahali pa nyota angani.

Hipatia hakuwahi kuolewa kwa sababu alisema "ameolewa na ukweli". Katika chanzo kimoja kuhusu maisha yake kuna habari kuwa mwanafunzi mmoja alijaribu kuwa karibu naye na kumwoa, lakini alikataa alipoendelea kumsumbua wakati alipokuwa na hedhi yake, alimtupia mlembe usoni na kumwambia, "Ni hicho tu unachotafuta, lakini huelewi uzuri wa kweli ni nini."[4]

Katika vyanzo vya kihistoria dini yake inatajwa kuwa "Mpagani", maana yake hakuwa Mkristo. Falsafa ya Uplatoni ya wakati wake ilikuwa mafundisho ya kiroho yaliyolenga kutambua asili ya ulimwengu iliyotajwa kama "ile moja" na kuona katika hisabati lugha ya siri ya ulimwengu. Uplatoni ulifundisha pia masharti ya kuishi maisha mema ya kufuata maadili.

Hipatia na hali ya siasa ya Aleksandria Edit

Ilhali Hipatia aliheshimiwa na watu wengi katika mji ule, gavana wa Kiroma Orestes alitafuta mara kwa mara ushauri wake. Wakati ule Aleksandria ilikuwa mji Wenye mabishano kati ya makundi kati ya wakazi wake; ilIkuwa na jumuiya kubwa ya Wayahudi, idadi kubwa walikuwa Wakristo, na wengine wafuasi wa dini mbalimbali za kale. Wakristo wakati ule walikuwa na migawanyiko kati yao, na askofu Sirili wa Aleksandria aliwahi kutumia ushawishi wake kufunga makanisa yote ya madhehebu ya Wanovasyani akalenga pia kufukuza wafuasi wa Nestori. Baada ya mapigano kati ya Wayahudi na Wakristo waliongoza umati wa Wakristo dhidi ya Wayahudi. Hapo gavana Orestes aliona Sirili ameingilia madaraka ya serikali akalenga kumzuia. Mwaka 415 kundi la wamonaki na wafuasi wa Sirili lilimshambulia Orestes na kumjeruhi. Baada ya kupona Orestes alimkamata kiongozi wa wamonaki hao akamhukumu adhabu ya kifo. Sirili alijibu kwa kumtangaza mtakatifu na shahidi wa imani. Sirili alijaribu kuelewana na gavana lakini huyo alikataa alidai utii wake.

Mauaji ya Hipatia Edit

Hapa uvumi ulienezwa kati ya wafuasi wa Sirili kwamba Hipatia aliwajibika kuzuia mapatano kati ya gavana na askofu. Siku moja kundi la Wakristo wafuasi wa Sirili lilimshambulia Hipatia wakati alitembea barabarani, wakambeba hadi jengo la kanisa moja, wakavua nguo zake na kumwua. Walikatakata mwili wake vipandevipande na kuchoma mabaki ya maiti[5].

Gavana Orestes aliandika taarifa kwa kaisari huko Konstantinopoli na serikali ilifanya uchunguzi wa mauaji; nafasi ya Sirili iliangaliwa pia, ama haikuwezekana kuthibitisha alishiriki katika njama ya kumwua Hipatia, ama alihonga maafisa ili wasimshataki.

Watu wengi walishtuka walipopokea habari za mauaji hayo. Wakristo wasiomfuata Sirili waliona tendo hilo kama aibu na dhambi. Katika nyakati za kisasa waandishi mbalimbali walitunga vitabu juu yake; ziko pia filamu.

Wanaastronomia wametunza kumbukumbu yake kwa kuita asteroidi moja Hypatia baada ya ugunduzi wake mnamo mwaka 1884. Pia kasoko moja kwenye Mwezi imepokea jina lake. Mnamo mwaka 2015 Umoja wa Kimataifa wa Astronomia uliamua kuipa sayari-nje Iota Draconis b jina lake.

Chanzo cha Sokrates wa Konstantinopoli Edit

Mwandishi Mkristo Sokrates wa Konstantinopoli aliandika miaka michache baada ya matukio habari zifuatazo kuhusu Hipatia katika Historia yake ya Kanisa: (Historia ecclesiastica)

Kulikuwa na mwanamke huko Aleksandria aliyeitwa Hipatia, binti wa mwanafalsafa Theon, ambaye alipata mafanikio makubwa katika fasihi na sayansi, hadi kuzidi wanafalsafa wote wanaume wa wakati wake. Akifuata mapokeo ya ya Plato na Plotinus, alielezea kanuni za falsafa kwa wanafunzi wake, ambao wengi wao walitoka mbali kupokea mafundisho yake. Kwa sababu ya kiwango chake cha kujiamini na utulivu wake wa ndani, ambao alikuwa amepata kwa sababu ya kukuza akili yake, alifika mara kwa mara hadharani mbele ya wakubwa wa mji. Wala hakujisikia aibu kuja kwenye mkusanyiko wa wanaume. Wanaume wote walimtukuza kwa sababu ya utu wake wa ajabu na fadhila. Hata hivyo hata yeye aliathiriwa na wivu wa kisiasa ambao wakati huo ulitawala. Kwa kuwa kwa vile alikuwa na mahojiano ya mara kwa mara na Orestes, iliripotiwa kwa nguvu kati ya watu wa Kikristo, kwamba ndiye yeye aliyezuia Orestes kupatanishwa na askofu. Baadhi yao, kwa hiyo, wakiharakishwa na bidii kali na ya kupindukia, ambaye kiongozi wake mkuu alikuwa msomaji wa kanisani aliyeitwa Peter, walimshambulia akirudi nyumbani, na kumburuta kutoka kwenye gari lake, walimpeleka kwenye kanisa linaloitwa Cæsareum, ambapo walimvua nguo kabisa, na kisha wakamuua kwa vigae vikali. Baada ya kuurarua mwili wake vipande vipande, walipeleka vipande vya mwili wake mahali palipoitwa Cinron, na hapo wakaiteketeza. Jambo hili halikuleta shida ndogo, sio tu kwa Sirili, bali pia kwa kanisa lote la Aleksandria. Na hakika hakuna kitu kinachoweza kuwa mbali na roho ya Ukristo kuliko mauaji, mapigano, na shughuli za aina hiyo. Hii ilitokea mwezi wa Machi wakati wa Kwaresima, katika mwaka wa nne wa uaskofu wa Sirili, chini ya ukonsuli wa kumi wa Honorius, na wa sita wa Theodosius. [6]

Marejeo Edit

  1. M.E. Waithe, Ancient Women Philosophers: 600 B.C.-500 A. D., Springer 1987, uk. 173
  2. Hypatia Of Alexandria. Gale Student Resources. Encyclopedia of World Biography (1998). Iliwekwa mnamo March 31, 2017.
  3. Calinger (2017). Hypatia. World Book Student. Iliwekwa mnamo March 31, 2017.
  4. M.E. Waithe, Ancient Women Philosophers: 600 B.C.-500 A. D., Springer 1987, uk. 172
  5. Waithe, uk. 173
  6. Imetafsiriw kutoka Kiingereza cha “Socrates - The Murder of Hypatia (415) - original Greek Text with English translation”, Historia Ecclesiastica, 7. 15, tovuti ya earlychurchtexts.com

Viungo vya Nje Edit