Kanuni ya Mt. Klara

Kanuni ya Mt. Klara ni kanuni ya kitawa ya kwanza kutungwa na mwanamke katika historia ya Kanisa.

Piero della Francesca, Mt. Klara.

Historia hariri

Klara wa Asizi (16 Julai 1193 - 11 Agosti 1253), bikira anayehesabika kuwa mwanzilishi mwenza wa Mabibi Fukara wa Utawa wa Ndugu Wadogo, alipenda kujiita mche mdogo wa Fransisko wa Asizi, akimfuata kiroho kwa kuishi katika mji wao toba kali iliyojaa matendo ya upendo na ibada. Akipenda kwa namna ya pekee ufukara wa hiari, hakukubali kamwe kuachanishwa nao, hata alipopatwa na hali ya kuhitaji na kuugua sana[1].

Baada ya Mtaguso IV wa Laterano (1215) kukataza kanuni mpya iliwabidi wapokee mojawapo ya zamani ili wakubaliwe na Kanisa Katoliki kama watawa. Basi wakaichagua ile ya Benedikto wa Nursia, wakiifuata katika mambo kadhaa kadiri yalivyopatana na mtindo wao mpya, bila ya nia ya kuwa Wabenedikto.

Hasa Klara hakutosheka na uhalali wa monasteri yake mbele ya Kanisa, bali kwa njia ya Fransisko aliomba akapewa na Papa Inosenti III “fadhili ya ufukara” (1216), yaani ruhusa ya kuishi bila ya mali hata kijumuia, kama jambo la msingi katika wito wake wa “kuishi kadiri ya ukamilifu wa Injili takatifu”, kwa kuungana na Yesu fukara kama bibiarusi fukara.

Kardinali Ugolino, akiona monasteri za namna hiyo zinavyoongezeka huko na huko, alizitungia katiba (1219) iliyopitishwa na Papa Honori III (1216-1227) ambayo ikawa msingi wa kanuni zote zilizoandikwa baadaye kwa Utawa II.

Lengo lake lilikuwa kukinga monasteri hizo dhidi ya upinzani na kuzipa mtindo wa kimonaki zaidi bila ya kuondoa usahili wake maalumu, ziwe muundo mpya wa aina moja chini ya Kanisa la Roma moja kwa moja.

Desturi kali alizoziagiza humo hazikumtisha Klara, ambaye alijishinda tayari na kujitesa kwa ushujaa mkubwa (katika kula, kuvaa, kulala n.k.) mpaka akakatazwa asizidishe.

Wala hakuogopa ukali wa ugo ulioagiwa na katiba hiyo, ili kutunza mazingira ya sala.

Wasiwasi wake ulihusu ufukara mkuu akiona hautajwi na katiba hiyo.

Mwanzoni Ugolino alitaka msimamo huo udumu katika monasteri kadhaa, ila alipochaguliwa kuwa Papa akaanza kuzipatia mali nyinginyingi, labda kisha kung’amua matatizo yaliyojitokeza.

Lakini Klara hakukubali kabisa akamuomba amtibitishie “fadhili ya ufukara” akakubaliwa (1228), lakini si kwa monasteri zote.

Suala lingine lililojitokeza mapema, halafu likaendelea kusababisha migogoro, ni nani awajibike kuwasaidia Waklara upande wa roho na upande wa riziki.

Fransisko alipokuwa Mashariki ya Kati, Filipo Longo aliteuliwa msimamizi wao, lakini mwanzilishi aliporudi uteuzi huo ukafutwa, masista wakasimamiwa tena na wasio Wafransisko, mpaka Ugolino, kisha kuchaguliwa awe Papa Gregori IX (1227-1241) alipowalazimisha Ndugu Wadogo kuwajibika (1221).

Klara alipoona wito wake wa Kiinjili upo hatarini upande wa sheria, kwa kuwa kanuni na katiba hazikuwa za Kifransisko, akaanza kuomba aweze kuahidi kushika kanuni ya Ndugu Wadogo badala ya ile ya Benedikto.

Mwaka 1234 akaja kumuunga mkono Anyesi wa Praha, binti mfalme ambaye alikataa kuolewa na mfalme mkuu Federiko II wa Ujerumani akaanzisha monasteri yake iliyokubaliwa “fadhili ya ufukara”.

Alitunga kanuni mpya kwa kuchanganya “mtindo wa maisha” alioandika Fransisko na katiba ya Ugolino, akamuomba Gregori IX, halafu Papa Inosenti IV (1243-1254) waithibitishe, lakini akakataliwa.

Kumbe Inosenti IV akathibitisha katiba ya Ugolino (1245) na kusisitiza ifuatwe kanuni ya Benedikto kwa sababu ina sifa nyingi.

Wakati huohuo alijaribu kusuluhisha mgogoro wa uhusiano kati ya Ndugu Wadogo na Waklara.

Klara alikuwa akiendelea kudai kwa nguvu msaada wa kiroho wa ndugu hao kulingana na ahadi ya mwanzilishi.

Kumbe Mtumishi mkuu Kreshensi wa Iesi (1244-1247) aliomba shirika liondolewe mzigo liliobebeshwa na Gregori IX, yaani himizo la kuanzisha konventi ndogo karibu na kila monasteri ya Waklara.

Basi, Inosenti IV aliamua Waklara wawe chini ya uongozi na mamlaka ya Ndugu Wadogo, akapendekeza masista waunganishwe na Utawa I.

Lakini shirika likazidi kuona litalemewa na wingi wa monasteri.

Mwaka 1247 Inosenti IV akatunga katiba mpya badala ya ile ya Ugolino iliyokwishaenea katika monasteri zote za Kifransisko, ikitumika pengine pamoja na desturi maalumu za mahali.

Katiba hiyo ilifanya kanuni ya Ndugu Wadogo kuwa msingi wa sheria za Waklara bila ya kuwadai waishike katika yote, ila katika utiifu, utovu wa mali na useja mtakatifu.

Katiba hiyo ilimuondolea Kardinali mlinzi mamlaka juu ya Waklara, ambao wakawekwa moja kwa moja chini ya viongozi wa Utawa I.

Kwa katiba hiyo Waklara wakaja kutambulikana Wafransisko kisheria, lakini ndani mlikuwa na pigo kubwa kwa Klara, yaani iliandikwa wazi kuwa monasteri zao zinaruhusiwa kuwa na mali za kujitegemea.

Ndiyo sababu monasteri chache tu zikaipokea katiba hiyo.

Vilevile Ndugu Wadogo wakazidi kulalamika hadi Kardinali mlinzi akajitwalia polepole mamlaka yao na hatimaye (1250) aliwaandikia wasithubutu kujiingiza katika uongozi wa Waklara.

Hivyo kwa muda mfupi katiba hiyo ikashindikana pande zote.

Klara, mgonjwa toka siku nyingi, alipoona kifo kinamkaribia, aliandika wasia wake ambamo alimuiga Fransisko katika kukumbusha asili ya wito wake na wa jamaa yake, na kutamka kwa msisitizo mkubwa nia imara ya kufuata ufukara mkuu “aliouahidi kwa Mungu na kwa Mt. Fransisko” pamoja na kuhimiza sana umoja wa dada zake.

Lakini pia, upande wa sheria, aliona haja ya kutunga upya “mtindo wa maisha” kwa kulinganisha kanuni ya Ndugu Wadogo na masharti ya maisha ya ndani tu.

Humo aliingiza pia maandishi mawili mafupi ya Fransisko kwao, kuhusu ufukara mkuu na kuhusu ahadi ya kwamba yeye na Ndugu Wadogo watawahudumia Waklara sawa na wenzao wa kiume.

Upande wake Klara aliahidi kuwatii waandamizi wa mwanzilishi. Kiini cha huo “mtindo wa maisha” kinasisitiza kwa nguvu nia ya kuishi bila ya mali yoyote, isipokuwa monasteri na bustani.

Jambo lingine linalokazwa ni udugu: humo neno “dada” linapatikana mara 66!

Udugu huo unatimizwa siku kwa siku chini ya “abesi na mama” kwa umoja wa mioyo pasipo ubaguzi wowote (tofauti pekee ni kati ya wanaojua na wasiojua kusoma kuhusu Sala ya Kanisa).

Hata dada “wa nje” (yaani “wanaohudumia nje ya monasteri” bila ya kubanwa na ugo) washiriki maisha ya jumuia sawa na wenzao.

Hao ni kundi maalumu la mtindo wa Kiklara, linalohitajika kadiri wenzao wanavyojifungia ndani: ni “akina Marta” kwa “akina Maria” kadiri Fransisko alivyowapangia Ndugu Wadogo wanaoishi upwekeni.

Udugu huo unajitokeza hata katika mikutano, ambayo inatakiwa kufanyika kila wiki kwa mchango wa wote, kupanga shughuli za maana na kuteua watakaoshika nyadhifa mbalimbali.

Abesi mwenyewe, ingawa anachaguliwa kwa maisha yake yote, kadiri ya mapokeo ya kimonaki, anaweza kubadilishwa na dada zake wakiona hawezi kutimiza vizuri kazi zake.

Uhusiano na Utawa I unasisitizwa tena kwa kudai msimamizi wa monasteri awe daima Ndugu Mdogo, pamoja na kuomba Utawa huo uipatie monasteri mapadri 2 na mabradha 2 kwa huduma za kiroho na za kimwili.

Huo “mtindo wa maisha” ukakubaliwa na Kardinali mlinzi (1252) halafu na Inosenti IV (1253).

Klara akapewa hati yake kitandani akaibusu; siku mbili baadaye akafa akiishika mikononi, wakihudhuria Leo, Anjelo na Yunipero, “wenzi watatu” wa Fransisko; pia inasemekana alijaliwa faraja za Bikira Maria na wanawake watakatifu kadhaa.

Tanbihi hariri

Marejeo kwa Kiswahili hariri

  Makala hii kuhusu Kanisa Katoliki bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kanuni ya Mt. Klara kama historia yake au maelezo zaidi?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.