Kituo cha kurushia vyombo vya angani
Kituo cha kurushia vyombo vya angani (kwa Kiing. spaceport) ni mahali pa kurushia vyombo vya angani kama vile satelaiti na vipimaanga kwa kutumia roketi zinazozibeba hadi anga-nje. [1]
Kituo cha kwanza cha aina hiyo kilikuwa kituo cha Umoja wa Kisovyeti katika Kazakhstan kilichopokea baadaye jina la Baikonur. Mnamo mwezi wa Oktoba 1957 satelaiti ya kwanza Sputnik 1 ilirushwa huko.
Kituo cha Baikonur kilikuwa pia mahali pa kuanza safari ya mwanaanga Yuri Gagarin aliyekuwa binadamu wa kwanza kufika angani.
Baada ya mwisho wa Umoja wa Kisovyeti, Shirikisho la Urusi lilikodisha eneo la Baikonur kutoka Kazakhsztn na liliendelea kulitumia kwa miradi yake kwenye anga-nje.
Baada ya mafanikio ya Wasovyeti, Marekani ilijenga kituo chake huko Cape Canaveral katika jimbo la Florida. Kilifuatwa na Kituo cha Kennedy Space Center ambako wanaanga walirushwa hadi Mwezi katika chombo cha Apollo 11 mnamo Julai 1969.
Ufaransa ilifuata kwa kujenga kituo cha kurushia cha Kourou katika Guyana ya Kifaransa kwenye bara la Amerika Kusini. Korou iliendelea kuwa kituo kikuu cha kurushia cha Umoja wa Ulaya na taasisi yake ya ESA.
China inatumia kituo cha Jiuquan kilichopo katika jangwa la Gobi.
Marejeo
hariri- ↑ Roberts, Thomas G. (2019). "Spaceports of the World". Center for Strategic and International Studies. Iliwekwa mnamo 1 Julai 2020.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link)