Mikaeli wa Cesena (jina asili la Kiitalia: Michele Fuschi[1]) (1270 hivi – 29 Novemba 1342) alikuwa padri Mfransisko, mkuu wa shirika la Ndugu Wadogo, na mwanateolojia kutoka Italia.

Mchoro wa ukutani wa Andrea di Buonaiuto huko Firenze. Mbele anaonekana Mikaeli wa Cesena akijadiliana na William wa Ockham na askofu mkuu wa Pisa Simone Saltarelli; nyuma yao papa Inosenti VI kati ya Egidio Albornoz na Karolo IV wa Luxemburg.

Maisha hariri

Mzaliwa wa Cesena, alijiunga na shirika akasoma huko Paris alipopata digrii ya teolojia.

Baadaye alifundisha huko Bologna na kuandika vitabu mbalimbali.

Jinsi alivyotetea ufukara wa Kiinjili ilimfanya ashindane na Papa Yohane XXII (1316-1334), hasa baada ya kuchaguliwa mkuu wa shirika (31 Mei 1316). Ndipo shirika lilipopitia hatari kubwa kuliko zote za historia yake.

Ni kwamba kiburi kilichowapata Ndugu Wadogo katika karne yao ya kwanza, kutokana na mafanikio yao na mashindano na Maaskofu, kikafikia upeo walipopingana na Papa pia, ambaye mamlaka yake ilikuwa imeanza kupungua.

Mara baada ya kuchaguliwa, Papa huyo, akisukumwa na [Mikaeli wa Cesena, alifululiza kutoa amri zilizolenga kukomesha ndugu “wa Kiroho”, mpaka 4 kati yao walichomwa moto sokoni. Hapo uasi wa wengi ukawa wazi usijali kutengwa na Kanisa wala kuhukumiwa adhabu ya kifo. Hasa Waklareno wakaendelea hivyo zaidi ya miaka mia mpaka Yohane wa Capestrano na Yakobo wa Marka walipowapatanisha na Kanisa (1430 hivi), hata wakarudi chini ya Mtumishi wa shirika lote (1473) wakiwa na Makamu maalumu wa kwao.

Mwaka 1323 Papa, akiendelea na vita vyake, alitoa hati ya kulaani dhana ya Ndugu Wadogo wote (iliyokubaliwa na mkutano mkuu 1322) kuwa Yesu Kristo na mitume wake hawakumiliki chochote wala binafsi wala kwa pamoja.

Badala ya kukubali tamko hilo, Mtumishi mkuu na wanashirika karibu wote walilikataa hata kumtangaza Yohane XXII kuwa mzushi. Mfalme mkuu wa Ujerumani, ili apate nguvu dhidi ya Papa, akawapokea Ndugu Wadogo chini ya ulinzi wake akafanya mmojawao atangazwe kinyume cha sheria kuwa ni Papa badala ya Yohane XXII (bado hai).

Baadaye kidogo uasi huo ukaisha, lakini matokeo ya kwazo kubwa hivi yalichangia sana kudidimia kwa shirika.

Tanbihi hariri

  1. Donovan, Stephen. "Michael of Cesena". The Catholic Encyclopedia. Iliwekwa mnamo 12 December 2011.  Check date values in: |accessdate= (help)

Viungo vya nje hariri

  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.