Yakobo wa Marka (1 Septemba 1393 - 28 Novemba 1476) alikuwa Mwitalia maarufu kama mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo na padri wa Kanisa Katoliki.

Yakobo wa Marka

Alitangazwa mwenye heri na Papa Urban VIII tarehe 12 Agosti 1624 na mtakatifu na Papa Benedikto XIII tarehe 10 Desemba 1726.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kifo chake[1].

Maisha ya awali hariri

Alizaliwa Monteprandone (karibu na Ascoli Piceno, leo katika mkoa wa Marche, nchini Italia) tarehe 1 Septemba 1393. Baada ya kufanya kazi ya kuchunga mifugo, alikimbia kwa ndugu yake fulani amsaidie kusoma.

Kisha kupata elimu kubwa katika sanaa huko Ascoli Piceno alijipatia digrii ya Sheria huko Perugia kwenye mwaka 1412. Baadaye alifanya kazi kama hakimu na wakili huko Bibbiena na Firenze katika mkoa wa Toscana.

Wito na malezi hariri

Kisha kufunga urafiki na Wafransisko wa huko na kutafakari mafumbo ya ukombozi kwenye mlima La Verna, aliacha kazi na kuingia utawani mnamo Julai 1416. Huko alilelewa pamoja na Yohane wa Kapestrano na Bernardino wa Siena. Mwaka 1423 alipewa daraja takatifu ya upadri.

Utume hariri

 
Confessione, 1476

Mhubiri hodari, alitumwa na shirika lake kupinga uzushi wa Wabogomili huko Bosnia na wa Wausi huko Austria na Boemia; alianzisha konventi kadhaa katika Ulaya ya Kati, akieneza ibada kwa Jina la Yesu na kutetea vita vya msalaba dhidi ya Waturuki.

Alishiriki Mtaguso wa Firenze wenye lengo la kurudisha umoja kati ya Wakatoliki na Waorthodoksi.

Kwa juhudi zake mwaka 1446, tena mwaka 1463, alipatanisha miji ya Fermo na Ascoli Piceno iliyokuwa imeshindana muda mrefu. Pia alitunga katiba za miji 11 huku akianzisha vyama vya kitume pia.

Pamoja na kazi hizo, alitunga vitabu 18, alijenga makanisa, konventi, hospitali, maktaba, visima n.k.

Alifariki huko Napoli tarehe 28 Novemba 1476. Tarehe hiyo ndiyo sikukuu yake ya kila mwaka katika liturujia.

Tazama pia hariri

Tanbihi hariri

  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.