Reale
Reale (pia: riale) ilikuwa pesa iliyotumika kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki wakati wa karne ya 19. Kwa kawaida ilimaanisha "Reale ya Shamu" jinsi Dolar ya Maria Theresa ilivyoitwa huko na jina hilo likatumiwa pia kwa sarafu nyingine za fedha.
Asili ya jina
haririReale ni jina lenye asili ya Kireno[1] kwa maana ya "kifalme" lililofika katika mazingira ya Uswahilini tangu safari ya nahodha Mreno Vasco da Gama aliyevuka Rasi ya Tumaini Jema mnamo mwaka 1498 na kufika Uhindi kupitia Mombasa. Jina liliendelea kutumiwa Uarabuni na katika Afrika ya Mashariki kwa sarafu za fedha kutoka nchi mbalimbali, hadi pesa ya leo inayoitwa "Riyal" huko Oman, Saudia na Iran.
Reale ya karne ya 19
haririMiji ya Waswahili haikutoa pesa zao za pekee bali ilitumia sarafu za nje. Hapo wafanyabiashara waliangalia thamani ya sarafu hizo Uarabuni kusini na Uhindi kwa sababu hizo zilikuwa nchi muhimu zaidi kwa biashara ya nje.
Katika karne ya 19 "reale" ilitumiwa katika Afrika ya Mashariki kwa sarafu za fedha kutoka nchi mbalimbali. Hasahasa ilimaanisha sarafu za Dolar ya Maria Theresa au Maria-Theresien-Thaler. Pesa hiyo ilitolewa nchini Austria wakati wa malkia Maria Theresa kuanzia mwaka 1741. Ilisambaa haraka katika nchi za Mediteranea na Milki ya Osmani hadi Uarabuni; ilipendwa kwa sababu asilimia ya fedha ndani yake haikupungua. Kutokana na mahitaji Austria iliendelea kutoa sarafu hiyo hata baada ya kifo cha malkia mwaka 1780. Dolar ya Maria Theresa iliendelea kuwa pesa kuu Uarabuni na Ethiopia ikawa pia pesa ya kawaida Uswahilini, ikiitwa "reale ya Shamu" na kutumiwa pamoja na rupia ya Kihindi kwa kubadilisha rupia mbili kwa reale moja.[2]
Sarafu hiyo (inayotolewa hadi leo kwa wakusanyaji wa sarafu) ina kipenyo cha milimita 39.5 na uzani wa gramu 28; kiwango cha fedha ndani yake ni 833⅓/1000, hivyo ina gramu 23.389 za fedha tupu.
Katika karne ya 19 sarafu hiyo ilitumiwa pia kama kipimo cha uzani wa wakia au aunsi moja.[3]
Jina reale kwa sarafu za Hispania na Ufaransa
haririKulikuwa pia na sarafu za Hispania na Ufaransa zilizoitwa "reale" ambazo zilifanana kwa uzani na kiasi cha fedha na reale ya Shamu.
"Reale mzinga" ilikuwa jina la "columnario" ya Kihispania, sarafu ya real nane za Hispania yenye uzani wa gramu 27[4] na jina lilitokana na nguzo mbili kwenye uso wake.
Sarafu ya franc tano za Kifaransa ilijulikana kama "Reale ya Fransa"[5] ikiwa nyepesi kidogo kuliko Reale ya Shamu na Reale mzinga kwa gramu 25 lakini kiwango cha fedha ilikuwa 9000/1000 ikiwa na kipenyo cha milimita 37.
Marejeo
hariri- ↑ "Real" ni pia neno la Kihispania, hivyo jina la pesa ya madini ya fedha katika nchi jirani mbili katika karne za kati hadi karne ya 19.
- ↑ Madan, uk 325
- ↑ Krapf 1882, uk 422: "Wakia, a weight of one dollar (small weight); ni uzito wa reali; e.g. the weight of a dollar when given for the same weight of something else; the dollar was formerly used as a weight"
- ↑ Columnario Archived 20 Machi 2018 at the Wayback Machine., tovuti iliangaliwa 24-03-2017
- ↑ Madan uk. 325