Taasubi ya kiume ni mtazamo unaomnyanyua mwanamume kwa kila jambo huku ukimtweza mwanamke. Mtazamo huo unasema kwamba "mwanamume awe kiongozi katika kila jambo, huku kazi ya mwanamke ni kufuata mwelekezo wa mwanamume na kufanya kazi ndogondogo za nyumbani, kama vile kupika, kufua na kupiga deki pamoja na kuzaa na kulea watoto. Kazi za ofisini katu haruhusiwi kufanya."

Madhila haya yanayotumiwa kumtweza na kumdunisha mwanamke huku yakimpa kipaumbele mwanamume ni mengi. Jambo hili huletwa na tamaduni zilizopitwa na wakati.

Barani Afrika

hariri

Katika jamii nyingi za Afrika mwanamke haruhusiwi kurithi mali wala kumiliki ardhi, ila yeye hutazamwa kuwa mali. Jamii humlinganisha mwanamke na mahari yanayotolewa ili aolewe. Hii ndiyo sababu ndoa za mapema zimekita mizizi katika jamii nyingi za Kiafrika.

Vilevile wanawake hawaruhusiwi kula vyakula fulani kama mayai na firigisi kwa imani potovu ya kuwa wakila watadhuriwa. Kumbe vyakula hivyo walivyonyimwa ni muhimu sana mwilini. Hizi ni itikadi zisizo na msingi wowote.

Kulikuwa na kazi za wanaume na zile za wanawake ambazo zilimdunisha mwanamke na kumpa mwanamume cheo cha juu zaidi.

Nyingi kati ya biashara kubwakubwa huendeshwa na kina baba, huku kina mama wakiuza mboga na dagaa vichochoroni. Wengi wa viongozi wa nyanja mbalimbali za nchi nyingi za Afrika ni wanaume; bila kutaja ulingo wa siasa ambapo wanaume hawaambiwi chochote wala lolote. Wanawake wachache wanaojitokeza na kuwania nyadhifa za kisiasa au kiutawala hutwa vijego. Wao hubaguliwa na jamii na kutazamwa kuwa waasi wa mila na tamaduni.

Sheria duni zisizowalinda wanawake pia huchangia kuendeleza taasubi ya kiume. Wanawake wanapobakwa au kudhulumiwa na mabwana zao nyumbani, hawapati haki kamilifu kutoka sheria za nchi. Hivyo wao huingiwa na woga na kulazimika kuvumilia mateso hayo, japo shingo upande.

Hali ya sasa

hariri

Itikadi kama hizi bila shaka zimepitwa na wakati. Watu wameanza kubadili mwelekeo. Watu wamepata utambuzi fulani kuhusu masuala ya kijinsia. Mashirika na chuo kikuuvyuo vikuu vingi vimebuni vituo vya masuala ya kijinsia vinavyofanya utafiti kuhusu vizuizi vya usawa katika mahusiano ya kiuana na kuihamasisha jamii kuondoa vikwazo hivi katika familia, shule, vyuo, viwanda, maeneo ya kazi, maabadini na kadhalika.

Lugha inayotumika katika vitabu na vyombo vya habari pia imejiepusha na taasubi ya kiume. Jamii imehamasishwa kuwatambua na kuwaheshimu wanawake na kutowahusisha na uzembe, ujinga na maovu mengine kama ilivyokuwa desturi zamani.

Katika ulimwengu wa sasa suala la jinsia ni tata mno. Wengi wanazidi kupigania usawa kiasi cha kukanusha tofauti zilizopo kati ya jinsia hizo mbili na haja ya kwamba kila moja ichangie namna yake ustawi wa jamii kuanzia familia.

Utatuzi wa kweli wa ubaguzi wa jinsia si kuwafanya wanawake wawe wanaume. Wana vipawa vyao vya pekee ambavyo ni muhimu vithaminiwe na kukuzwa badala ya kuiga tu wanachofanya wanaume kama vile kupigania madaraka kwa gharama yoyote.

Upande wa dini

hariri

Ulingo wa dini nao umeathiriwa kwa kiasi tofautitofauti. Japokuwa waumini wengi ni wanawake, nafasi nyingi za uongozi huchukuliwa na wanaume. Wengi wa makasisi wa makanisa makubwamakubwa ni wanaume. Viongozi wa Uislamu pia ni wanaume.

Katika kutathmini hali hiyo, ni muhimu kutambua kiasi gani hiyo ni athari ya taasubi na kiasi gani ni sharti la dini yenyewe. Baadhi ya dini hizi zimemkataza mwanamke kuwa kiongozi katika dini hizo kwa misingi ya imani husika.

Kwa mfano, Wakatoliki na Waorthodoksi hawakubali kuwapa daraja takatifu wanawake kwa sababu Yesu aliteua Mitume wake wote 12 kati ya wanaume, ingawa hakubagua wanawake katika kumfuata.

Kwa msingi wa dini, kuna haja ya kuelewa zaidi kwa nini Mungu aliamua kuumba watu wa jinsia mbili, na ana mpango gani juu ya kila moja.

Kwa Wakristo wengi, Bikira Maria ndiye kiumbe bora (baada ya mwanae) na ni kielelezo cha kilele ambacho Mungu kwa neema yake anataka kuwafikishia binadamu kwa kutumikia wenzao kwa upendo mnyenyekevu.

Tazama pia

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Taasubi ya kiume kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.