Uzembe (kwa Kilatini acedĭa, kutoka neno la Kigiriki ἀκηδία, linaloundwa na ἀ- "utovu wa" -κηδία "juhudi") ni kukosa uwajibikaji na umakinifu katika kutenda, pamoja na kutojali hali ya mazingira[1] .

Jacques Callot, Accidia (1620).
Dürer, Melencholia (1514).
Vilema vikuu

Katika maadili, unahesabiwa kati ya vilema vikuu (au mizizi ya dhambi) kwa kuwa unasababisha makosa mengine mengi kwa kumfanya mtu asitimize wajibu[2].

Wa kwanza kutambua shida hiyo walikuwa wamonaki.

Ufafanuzi

Thomas Aquinas katika Summa Theologica (Secunda Secundae, Q. 35) alichunguza sana uzembe na kuufafanua kama "huzuni kadiri ya dunia" inayoleta "kifo" (hadi kujua), kinyume cha "huzuni kadiri ya Mungu" iliyotajwa na Mtume Paulo (2Kor 7:10).[3]

Uvivu kwa jumla ni kosa la kuchukia kazi na juhudi, kupoteza muda au walau kutenda kwa ulegevu, kinyume cha moyo mkuu. Si ule ugumu wa kutenda unaotokana na afya mbaya, bali ni msimamo mbaya wa utashi na wa hisi ambao unaogopa na kukataa jitihada, unakwepa tabu ili kufurahia utamu wa kukaa tu bila kufanya chochote. Mvivu ni mnyonyaji anayekula jasho la wengine; ni mtulivu akiachwa bila kazi, lakini anawachukia wanaotaka aifanye. Kilema hicho kinaanza na utepetevu katika kazi, halafu kinazidi kusogea mbali na utendaji wowote wa maana.

Ukihusu wajibu wa dini ni ukinaifu wa mambo ya Kiroho unaosababisha yafanywe kwa ulegevu, yafupishwe au yaachwe kwa visingizio mbalimbali. Ndio chanzo cha uvuguvugu. Huzuni hiyo mbaya, kinyume cha ile ya majuto, inatulemea kwa kuwa roho yetu inashindwa kuitikia ipasavyo. Hapo tunafikia hatua ya kukubali ukinaifu wa mambo ya Kiroho, kwa kuwa yanadai juhudi na kazi nyingi juu yetu wenyewe. Roho ya ibada, yaani utayari wa utashi katika kumtumikia Mungu, inatuinua, kumbe uzembe unatufanya tuone nira ya Bwana haibebeki, tukakimbie mwanga wake unaotukumbusha wajibu wetu. “Kwa macho mabovu ni chukizo mwanga unaoyapendeza yale mazima” (Augustino).

Huzuni hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya kujitakia, si ule ukavu ambao unatupata katika majaribu ya Kimungu na kuendana na sikitiko halisi la makosa, uchaji wa Mungu kuhusu uwezekano wa kumchukiza, hamu ya ukamilifu na haja ya upweke, umakinifu na sala ya mtazamo mnyofu. Utakaso wa Kimungu wa hisi unatufanya “tusipate ladha wala faraja katika mambo ya Kimungu wala katika kiumbe chochote… ila kwa kawaida tunaendelea kumkumbuka Mungu, tukiogopa kutomtumikia kwa sababu hatuonji ladha katika mambo yake… Ndipo tunapoona kwamba kutohisi chochote na kuwa wakavu hakutokani na ulegevu na uvuguvugu, kwa sababu sifa maalumu ya uvuguvugu ni kutojali kabisa rohoni mambo ya Mungu… umelegea katika utashi na akili, wala haujali suala la kumtumikia Mungu. Kinyume chake, ukavu unaotakasa una ari ya kudumu ndani yake; hautulii bali unasikitika kwa kuwa haujitahidi inavyotakiwa katika kumtumikia Mungu” (Yohane wa Msalaba).

Kwa maneno mengine, jaribu hilo la Kimungu linatufanya tukose yaliyo ya ziada tu katika roho ya ibada, si kiini chake, yaani nia ya kumtumikia Mungu kwa bidii. Kumbe uzembe ni kupungukiwa kiini chenyewe cha roho ya ibada kutokana na kosa la ulegevu. Katika jaribu hilo la Kimungu tunasikitikia mtawanyo wa mawazo katika sala na kujitahidi kuupunguza. Kumbe katika uzembe tunaupokea, hata mawazo ya bure yakaenea karibu muda wote wa sala kwa kuwa ndivyo tunavyojitakia kwa kiasi kikubwa. Tunafuta utafiti wa dhamiri kwa kuwa unachosha; hatutambui tena makosa yetu na tunazidi kutumbukia uvuguvugu; polepole tabia mbovu tatu zinapata nguvu na kuzaa maovu.

Ukinaifu wa mambo ya Kiroho ni mbaya, tena ni dhambi kadiri unavyotokana na utashi kwa njia ya ulegevu. “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana… Pendo na lisiwe na unafiki; lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema… kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu” (Rom 12:1,9,11-12).

“Wanaougua uzembe wanakinai hata mambo bora ya Kiroho; wanayaepa kwa sababu hayawapi faraja yoyote ya kihisi… Hivyo kwa uzembe hawafuati njia ya ukamilifu, ambapo ni lazima kujikana kwa upendo wa Mungu. Wakivutwa na yale yanayowapendeza, wanapendelea matakwa yao kuliko ya Mungu. Wangemtaka Bwana akubali madai yao, kwa sababu kinachowasikitisha ni kupaswa kupokea kwa mikono miwili yale yanayompendeza Mungu; wakiyakubali ni shingo upande tu… Wanamshusha Mungu mpaka kwao, badala ya kuinuka hadi kwa Mungu. Wakinyimwa faraja, wanashughulikia ukamilifu wao kwa uvuguvugu na ulegevu tu. Wanaukimbia msalaba ingawa ndio chemchemi ya furaha za Kiroho zilizo safi na imara zaidi… Wakiingia njia nyembamba, ambayo Yesu Kristo alisema ndiyo inayoongoza kwenye uzima, wanaona ni tabu na huzuni tu” (Yohane wa Msalaba).

Pengine wanaoacha sala wanajitetea, “Tunapaswa kujinyima utamu wa sala na kukabili ugumu wa masomo na kazi”. Maneno hayo yakitamkwa na mtu mwenye bidii yana maana hii: “Tunapaswa kujinyima utamu wa sala, hasa faraja za kihisi, na kukabili ugumu wa masomo au kazi ya lazima kwa wokovu wa watu”. Kumbe yakitamkwa na mtu anayetaka kuficha uzembe wake hayana maana, kwa kuwa yeye hajinyimi utamu wowote wa sala, kwa sababu hausikii, na anajisingizia kuzuiwa na kazi ambazo kwa kweli ni za juujuu tu na zinampendeza. Mara nyingi uzembe unasababishwa na utendaji mwingi wa kibinadamu tu, usiofanywa kitakatifu, ambapo mtu analenga furaha yake badala ya Mungu na faida ya watu. Hata masomo yasiyoongozwa na upendo wa Mungu na wa jirani ni tasa Kiroho. Hatimaye ni kwamba mara nyingi sala ni kavu: ndiyo sababu ni vigumu kuwaongoza watu wadumu katika maisha halisi ya sala kuliko kuwavuta wasome na kusema juu yake.

Ukuu wa kilema hicho na matokeo yake

Uzembe ni dhambi ya mauti ukifikia hatua ya kuweka pembeni jukumu la lazima kwa utakatifu na wokovu (k.mf. Misa ya Jumapili). Ukiacha matendo ya dini yasiyo muhimu hivyo, ni dhambi nyepesi tu, lakini tusipopambana na ulegevu huo, utatuzidi na kutufanya vuguvugu. Polepole maelekeo mabaya yatachipuka upya na kutaka kutawala, yakijitokeza kwa dhambi nyepesi nyingi za makusudi, zinazoelekeza kutenda dhambi kubwa zaidi. Kama vile upungufu wa damu unakaribisha maradhi ya hatari, uzembe ni mzizi wa dhambi nyingine kwa sababu “hakuna mtu anayeweza kudumu muda mrefu katika huzuni pasipo furaha yoyote” (Aristotle). Basi, anayekosa furaha ya Kiroho kwa uzembe wake, hachelewi kujitafutia furaha za chini zaidi.

Matokeo yake ni ya kutisha: si udhaifu tu tena, bali uovu wa moyo; kinyongo kwa jirani; kukosa nia ya kutekeleza wajibu; kukata tamaa; usingizi wa roho unaofikia kusahau amri; hatimaye kutawanyika kujitafutia yasiyo halali, hali inayojitokeza kwa kuzamia mambo ya nje kwa njia ya udadisi, usemaji, mahangaiko, ugeugeu na utendaji mwingi usiozaa chochote. Hivyo mtu anaufikia upofu wa roho na udhaifu mkubwa zaidi na zaidi upande wa utashi. Kwa kuteleza kwenye genge hilo wengi wamesahau ukuu wa wito wa Kikristo, na ahadi walizomtolea Mungu.

Tanbihi

  1. "accidie" The Concise Oxford Dictionary of the Christian Church. Ed. E. A. Livingstone. Oxford University Press, 2006. Oxford Reference Online. Oxford University Press. 1 November 2011
  2. the hermitary and Meng-hu (2004). "Acedia, Bane of Solitaries". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 3 Januari 2009. Iliwekwa mnamo 22 Des 2008. {{cite web}}: Unknown parameter |deadurl= ignored (|url-status= suggested) (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. Summa, II-II, 35, 3.

Viungo vya nje