Shirika la Reli Tanzania

Shirika la Reli Tanzania (kwa Kiingereza: Tanzania Railways Corporation, kifupi: TRC - 2007 - 2011 TRL [1]) ni kampuni ya umma inayoendesha usafiri kwenye mtandao mkubwa zaidi wa reli nchini Tanzania.

Njia za reli za TRC
Treni ya TRC katika kituo cha reli Daressalaam
Kituo cha reli Kigoma
Boriti ya chuma ya mwaka 1912 kwenye njia ya reli ya Kigoma mwaka 2012

Inaendesha hasa usafiri kwenye njia za reli zifuatazo katika Tanzania:

Hali ya shirika ilikuwa duni mno na kwa miaka mingi, njia ya kaskazini haikuwa na huduma ya abiria. Tangu mwaka 2017 hivi huduma zimeboreshwa tena.

TRC ni tofauti na kampuni ya TAZARA inayoendesha reli kati ya Dar es Salaam na Zambia.

Historia

TRC inatumia njia za reli zilizoanzishwa wakati wa ukoloni katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na kupanuliwa wakati wa utawala wa Kiingereza; tena baada ya uhuru. Njia hizo zilitumia upana wa mita 1 (milimita 1000). Mnamo mwaka 1976 reli ya TAZARA iliongezwa kama kampuni ya pekee ikitumia geji ya milimita 1,067. Tangu 2017 TRC ilianza kujenga njia mpya za geji sanifu zinazotumia upana wa milimita 1,435.

Reli ya Usambara

Reli ya kwanza katika Tanganyika ilianzishwa mwaka 1893 kwenye bandari ya Tanga. Tarehe 16 Oktoba 1894 sehemu ya kwanza ilifunguliwa kati ya Tanga na Pongwe eröffnet. Hadi mwaka 1905 njia hiyo iliendelezwa hadi Mombo ikajulikana kwa jina "Reli ya Usambara" (Usambarabahn)[2]. Reli hiyo ilianzishwa na "Kampuni ya Reli kwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani" (Eisenbahn - Gesellschaft für Deutsch-Ostafrika) iliyokuwa kampuni chini ya Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki yenye shabaha ya kujenga njia ya reli kutoka Bahari ya Hindi hadi Ziwa Viktoria. Lakini kampuni ilifilisika na mwaka 1899 serikali ya Ujerumani ilinunua mradi wote. Utawala ulichukuliwa na Shirika la Reli kwa Koloni za Kijerumani. Mwaka 1909 njia ya reli ilifika Bwiko (Mkomazi). Serikali ilitoa mkopo mpya na hivyo njia iliweza kujengwa hadi Moshi na tangu 8 Februari 1912 huduma ya reli ilipatikana kuanzia Tanga hadi Moshi.

Wajerumani walipanga kuendelea hadi Arusha, lakini mipango hii haikutekelezwa kutokana na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Reli ya Kati

Wajerumani walianza kupanga reli kutoka mji mkuu mpya wa Dar es Salaam kuelekea Maziwa Makuu mnamo mwaka 1891[3]. Mipango hii yote ilishindikana kutokana na matatizo ya kifedha. Hatimaye serikali ilifaulu kupata kibali cha bunge kwa mkopo uliowezesha kuanzisha ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ulioanzishwa mwaka 1906 na kukamilishwa mwaka 1907. Reli hiyo ilikuwa mkononi mwa Shirika la Reli la Afrika ya Mashariki (Eisenbahngesellschaft für Ostafrika). Mwaka 1908 serikali ilinunua hisa nyingi za shirika hilo na kutoa fedha kwa kuendeleza njia ya reli hadi Ziwa Tanganyika.

Huduma zilifunguliwa 1 Januari 1910 hadi Kilosa, 1 Novemba 1910 hadi Dodoma, 1 Agosti 1911 hadi Saranda, 15 Septemba 1911 hadi Tura na kufika Tabora tarehe 26 Februari 1912. Ujenzi uliendelea hatimaye hadi Ziwa Tanganyika ulipofika tarehe 1 Februari 1914. Kituo cha mwisho kilijengwa kwenye mwambao wa Hori ya Kigoma; mahali palichaguliwa km 5 kaskazini mwa mji wa Ujiji kutokana nafasi nzuri ya bandari pakaendelea kuwa mji wa Kigoma. Treni zilipita kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma katika muda wa saa 53.

Reli hiyo iliitwa mwanzoni Reli ya Kati (Mittellandbahn) na baada ya kuelekea hadi ziwani ikaitwa Reli ya Tanganyika.

Mwaka 1914 Serikali ya Ujerumani ilikubali mpango wa kuongeza kilomita 480 kutoka Tabora kwenda Rwanda ambayo ilikuwa pia sehemu ya koloni yao; njia hiyo ilitarajiwa kutoka Tabora, kupita upande wa kaskazini wa Igulwa (Bukombe) na kufika karibu na Rusumo (leo kituo cha mpakani Tanzania-Rwanda). Mipango hii ilishindikana kutokana na Vita Kuu ya Kwanza.

Wakati wa Vita Kuu, koloni ya Kijerumani ilivamiwa na majeshi ya Uingereza na Ubelgiji. Tangu mwaka 1916 mataifa hayo yalishika njia zote za reli. Waingereza walijenga njia kutoka Voi hadi reli ya Usambara karibu na Moshi kwa juhudi zao za vita, hivyo kuunda njia ya reli baina ya Kenya na Tanganyika.

Utawala wa Kiingereza

Mwaka 1919 serikali ya Uingereza ilianzisha mamlaka ya Huduma za Reli na Mabandari ya Tanganyika (Tanganyika Railways and Port Services TR&PS). Mamlaka hiyo iliongeza njia zifuatazo:

  • njia ya reli kutoka Tabora hadi Mwanza ilifunguliwa mwaka 1928; ilitumia sehemu ya mipango ya reli ya Rwanda iliyoandaliwa na Wajerumani.
  • Njia ya reli ya Usambara ilifika Arusha kwenye mwaka 1930
  • Mnamo mwaka 1948 njia ya kando ikafunguliwa kutoka Msagali (Mpwapwa) hadi Hororo, lakini ilifungwa tena mwaka 1951
  • 1950 njia ya reli kutoka Kaliua hadi Mpanda ikafunguliwa.

TR&PS iliunganishwa mwaka 1948 na reli za Kenya na Uganda kuwa East African Railways and Harbours Administration (kuanzia mwaka 1969: East African Railways Corporation EARC).

Shirika la Overseas Food Corporation lilianza mwaka 1949 kujenga reli katika kusini ya nchi iliyojulikana kama Southern Province Railway; njia zake zenye urefu wa kilomita 250 ziliunganisha Mtwara, Lindi, Nachingwea na Masasi. Baada ya kufilisika kwa mradi wa karanaga katika mwaka 1951, reli hiyo ilikabidhiwa kwa mamlaka ya East African Railways. Ikaendelea hadi 1963 ilipofungwa kwa sababu mapato hazikulingana na gharama za uendeshaji[4].

Baada ya uhuru

Baada ya uhuru, mtandao wa njia za reli ulipanushwa tena. Mnamo mwaka 1963 njia mpya iliunganisha Reli ya Kati na reli ya Usambara. Mwaka 1965 njia mpya kitoka Kilosa kwenda Kidatu ilifunguliwa.

Mnamo 1977 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika na hii ilikuwa pia mwisho wa East African Railways Corporation EARC. Shughuli zake zilichukuliwa sasa na Tanzania Railways Corporation (TRC).

Mnamo 1997 idara ya usafiri wa maji ilitengwa katika TRC ikawa kampuni ya pekee kwa jina la Marine Services Company Ltd.[5]

Hali ya reli iliendelea kushuka polepole kutokana na utawala mbaya na ukosefu wa uwekezaji katika miundombinu. Majaribio kadhaa za kufufusha kampuni yalishindikana. Kiasi cha mizigo na abiria kilichobebwa kilifikia kilele kwenye mwaka 2003 (abiria 83,861 na tani za mizigo 1,442,713) lakini kuanzia hapa kikapungua kutokana na ubovu wa miundombinu.[6]

Mwaka 2006 shirika la TRC lilivunjwa likaisha kumiliki njia za reli pamoja na kuwajibika kwa usafiri hapa pamoja na mawasiliano kwa mabasi ya reli. Umilikaji wa njia za reli ulipewa kampuni mpya ya Reli Assets Holding Company Ltd RAHCO.

Huduma ya mabasi zilifungwa, pamoja na huduma ya abiria kwenye njia za kuelekea kazkazini.

Mwaka 2006 shughuli za kuendesha usafiri wa reli ilihamishwa kwa shirika jipya la "Tanzania Railways Limited" (TRL) iliyokuwa mradi wa pamoja wa serikali ya Tanzania na kampuni ya RITES kutoka nchini Uhindi. Tangu mwaka 2011 Jamhuri ya Maungano ya Tanzania imeshika hisa zote (100%) za TRL[7].

Mtandao wa reli ulibaki mkononi mwa serikali ikimilikiwa na RAHCO kama wakala wa serikali.

Mnamo mwaka 2017 TRL na RAHCO ziliunganishwa tena na TRC ilifufushwa. Kuanzia hapo huduma zilianza kuboreka tena. TRC ilianzisha pia mfumo mpya wa Reli ya SGR Tanzania inayotumia geji za upana wa milimita 1,435.

Njia za reli

TRC imerithi njia zenye upana wa mita 1 kwa urefu wa kilomita 2,600. Usafiri wote ni kwa injini za diseli.

Leo hii injinitreni na mabehewa ni bovu, hali ya njia ya reli pia kwa hiyo treni zinazoendelea kusafiri hutembea polepole na kwa kuchelewa. Ratiba ya safari kati ya Daressalaam hadi Kigoma ni masaa 40 kwa kilomita 1252 inayolingana na mkasi wa 30 km/h. Zamani kulikuwa na terni 3 za abiria kila wiki, lakini mwaka 2011 hali halisi ilikuwa treni 1 pekee.

Mabehewa ya kwenda Mwanza yanasafiri pamoja na treni ya Kigoma na kuwa treni ya pekee huko Tabora.

TRL na TAZARA

Upana wa njia ya TRL ni tofauti na TAZARA kwa hiyo mabehewa hayawezi kuingia kutoka njia ya kampuni moja kwa nyingine. Daressalaam na Kidatu kuna vituo vya huhamishia mizigo kati ya makampuni haya.

Mipango ya njia mpya Tanga - Musoma - Uganda

Tangu mwaka 2011 kuna mapatano kati ya Tanzania na Uganda kuanzisha njia ya reli mpya kati ya Tanga na Kampala kupitia Arusha na feri kwenye Ziwa Viktoria.[8]

Kufuatana na mapatano haya kilomita 400 kati ya Tanga na Arusha zitaboreshwa na njia mpya ya kilomita 480 kutengenezwa kutoka Arusha kwenda Musoma. Kwenye bandari ya Musoma mizigo itahamishwa kwenye feri kwenda Uganda. sehemu ya mipango hii ni ujenzi wa bandari mpya huko Tanga - Mwambani na bandari mpya huko Kampala - Bukasa.

Njia hii mpya ingekuwa fupi kuliko njia zilizopo kwa sasa kati ya pwani la Bahari Hindi na Uganda lakini hadi mwaka 2021 hakuna hatua ziliuochukuliwa.

Mfumo mpya wa geji sanifu SGR

Tazama makala Reli ya SGR Tanzania

Marejeo

  1. Hadi 2007 Tanzania Railways Corporation (TRC)
  2. Makala "Eisenbahnen", katika Kamusi ya Koloni za Kijerumani (1920) - Deutsches Kolonial-Lexikon (1920), Band I, S. 529 ff.
  3. Kwa habari zinazofuata linganisha makala "Eisenbahnen", katika Kamusi ya Koloni za Kijerumani (1920) - Deutsches Kolonial-Lexikon (1920), Band I, S. 529 ff., kifungu 1.b.
  4. Burton, David (2014). The Groundnut Line: The Story of the Southern Province Railway of Tanganyika. Telford, Shropshire: David Burton.
  5. "Home". Marine Services Company Limited. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 10 Septemba 2011. Iliwekwa mnamo 2011-06-26.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  6. Statement of managing director RAHCO Eng. Benhadard Tito in a week of the Ministry of Transport to mark 50 years of Tanzania mainland independence, tovuti ya Rahco.co.tz kupitia archive.org
  7. "TRL - "Background"". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-11-16. Iliwekwa mnamo 2016-09-28.
  8. "Taarifa ya East African". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-10-17. Iliwekwa mnamo 2015-10-17.

Viungo vya Nje