Ujiji ni mji wa kihistoria upande wa Magharibi wa Tanzania mwambaoni mwa Ziwa Tanganyika. Ni mahali pa kihistoria na mji wa kale katika magharibi ya Tanzania. Iko kilometa 5 tu kutoka kitovu cha Kigoma upande wa kusini wa uwanja wa ndege. Pamoja na Kigoma inafanya manisipaa ya Kigoma-Ujiji.

Ujiji 2012 Tamino
Kumbuumbu ya dr living stone Ujiji,Tanzania


Ujiji
Ujiji is located in Tanzania
Ujiji
Ujiji
Majiranukta: 4°54′41″S 29°40′28″E / 4.91139°S 29.67444°E / -4.91139; 29.67444
Nchi Tanzania
Mikoa ya Tanzania Kigoma
Wilaya Manisipaa ya Kigoma Ujiji

Historia

Ujiji huaminiwa imeundwa mwanzoni mwa karne ya 19, labda kidogo baada ya mwaka 1821 [1]. Ilikuwapo kwenye mwisho wa njia ya misafara kati ya pwani ya Bahari Hindi na Ziwa Tanganyika. Bidhaa kutoka pwani zilihifadhiwa huko katika ghala na kusambazwa kwa biashara ya kuvukia ziwa kwa mashua.

Wapelelezi Wazungu walianza kufika wakati wa Tippu Tip. Ni mahali ambapo Richard Burton na John Hanning Speke walifikia Ziwa Tanganyika mwaka wa 1858, na tena ambapo Henry Morton Stanley alimkuta David Livingstone mwaka wa 1871.

Wakati wa ukoloni wa Kijerumani umuhimu wa Ujiji ulipungua. Mwambao ulifaa kwa mashua ya kienyeji lakini kina cha maji hakikutosha kwa ajili ya meli mpya. Kwa sababu hiyo hori ya Kigoma, takriban kilomita 7 upande wa kaskazini, iliteuliwa kama bandari kuu na pia baadaye, tangu mwaka 1913, kituo kikuu cha reli ya kati kutoka Dar es Salaam. Kutokana na kuhamishwa kwa miundombinu muhimu Kigoma iliendelea kuwa mji mkubwa ilhali Ujiji ikarudi nyuma.

Masimulizi juu ya Kigoma Ujiji

Wakati miji kadhaa ya Afrika ikipata majina kutokana na ujio wa wageni, kuna baadhi ya miji ilipata majina yake kutokana na Waafrika wenyewe. Kutaja majina kutokana na wenyeji kulitegemea sana watu, hasa wale waliokuwa maarufu kwenye jamii. Kumbe ile miji iliyopata majina kutokana na wageni, sababu ilikuwa ni kujiwekea sifa kwa mataifa hayo na wakati mwingine mitazamo tu ya wageni hao ilisababisha mji fulani kupata jina.

Kwa upande wa miji kama Ujiji na Kigoma, watu huamini kuwa miji hiyo ilikuwa kipindi cha ukoloni. Ukweli ni kwamba Ujiji na Kigoma ilipata kukua kwa muda mrefu sana hata kabla ya ujio wa wageni kwenye maeneo hayo.

Kihistoria miji hiyo ilipata majina kutokana na watu maarufu waliopata kuishi na kujiwekea historia katika miji hiyo.

Watu wengi hudhani kuwa mji wa Kigoma na Ujiji ilianzishwa na ndugu wawili waliofahamika kwa majina ya Kajiji na Kagoma (Bugoye).

Ifahamike tu kwamba kabla ya mji wa Kigoma kuitwa Kigoma palikuwa panaitwa Lusambo_Gwa_Nyange na Ujiji palikuwa panaitwa Ubujiji.

Inaelezwa kuwa Kajiji alikuwa mkarimu, mpole na mwenye upendo kwa watu wote, na Kagoma alionekana kuwa tofauti kwa jamii. Kutokana na tabia hizo za ndugu hao wawili, wengi walimpenda sana Kajiji na kufanya maeneo aliyokuwa akiishi kupendwa na watu wengi. Kwa kuwa idadi ya watu ilikuwa ikiongezeka, basi walipokuwa wakienda kwa Kajiji wakasema tunaenda Ubujiji kulingana na lugha ya kikabila.

Wengi walikuwa wanapenda kwenda Ubujiji na kujikuta wakijazana kwenye mji huo. Hata wageni walipoingia kwenye karne ya 19, walikuta mji huo una idadi kubwa sana ya watu. Kwa kuwa wakati huo Waarabu hawakuwa na nguvu sana hawakutaka kubadilisha jina hilo na badala yake waliamua kuendeleza mji huo na jina hilo.

Mpaka ukoloni ukianzishwa bado eneo hilo lilikuwa na jina hilo, isipokuwa kukawa na mabadiliko katika orthografia na matamshi ya neno Ubujiji, ndipo tukapata jina Ujiji na hata kwenye maandiko ya wakati huo mji huo ulitambulishwa kama Ujiji.

Kwa upande wa Kagoma au Bugoye pia mambo yalikuwa hivyo, sema kwa upande wa Kagoma, mji ulipata kukua kutokana na ujio wa Wagoma katika mji wa Kagoma.

Ikumbukwe kuwa Wagoma ni moja ya makabila ya Kimanyema waliokuja Tanganyika kipindi cha ukoloni karne ya 18. Sultani wa Wagoma alikuwa akiitwa Sultani Simba.

Mara baada ya Wagoma hao kusikia mji huo unaitwa Kigoma, walijisikia raha sana kwani mji ulikuwa unafanana na jina la kabila lao, hivyo kujikuta wakiupenda na kuanza kuujenga. Ile sehemu aliyokuwa akikaa Kagoma au Bugoye palifahamika kwa jina la Ibugoye ambapo kwa sasa ndio pale Mwanga. Lakini kiuhalisia Wagoma walifikia maeneo ya Bangwe.

Kwa kuwa ardhi ya Ujiji ilikuwa yenye rutuba, Wagoma walipenda kulima maeneo ya Ujiji. Kwa hiyo mji wa Kigoma na Ujiji ni miji ambayo ilijipatia historia ya pekee barani Afrika, kwani miji hiyo imepata majina yenye asili yake hapahapa.

Ikumbukwe kwamba Wagoma ni kabila la Wamanyema, kwa sababu Wamanyema ni mkusanyiko wa makabila zaidi ya 18 yaliyoungana na kuwa kitu kimoja.

Pia Wamanyema walipofika Kigoma kuna ambao walipata majina katika miji kama Katonga, Kabwe, Mkabogo au Kabogo: hao wote walikuwa Wamanyema wenye asili ya Kongo.

Pia Waha waliokuwa Kigoma na Ujiji waliwapokea watani wao Wamanyema na kuanza kuishi pamoja mpaka sasa.

Marejeo

  1. [http://web.archive.org/20170517125039/http://www.ub.bildarchiv-dkg.uni-frankfurt.de/Bildprojekt/Lexikon/Standardframeseite.php Archived 17 Mei 2017 at the Wayback Machine. (makala "Udjidji" katika DKL
  Kata za Wilaya ya Kigoma Mjini - Mkoa wa Kigoma - Tanzania  

Bangwe | Buhanda | Businde | Buzebazeba | Gungu | Kagera | Kasimbu | Kasingirima | Katubuka | Kibirizi | Kigoma | Kipampa | Kitongoni | Machinjioni | Majengo | Mwanga Kaskazini | Mwanga Kusini | Rubuga | Rusimbi