Usafiri wa anga-nje

(Elekezwa kutoka Usafiri wa angani)

Usafiri wa anga-nje ni kila aina za safari au usafiri inayofikia nje za angahewa ya Dunia kwenye anga-nje. Ilhali hakuna mpaka kamili baina ya angahewa na anga-nje kuna mapatano ya kutazama umbali wa kilomita 100 kama chanzo cha anga-nje Chombo cha kwanza kilichofikia juu ya km 100 kilikuwa roketi ya Kijerumani aina ya V-2 katika majaribio ya mwaka 1944.[1]

Roketi ya Soyuz TMA-5 ilirushwa uwanja wa anga Baikonur nchini Kazakhstan mnamo 14 Oktoba 2004 kikibeba wanaanga 3 kwenda ISS
Kituo cha anga cha Kimataifa ISS mnamo mwaka 2009

Chanzo cha usafiri wa anga-nje kilikuwa kuruka kwa chombo cha angani cha Kisovyieti Sputnik 1 mnamo 4 Oktoba 1957 iliyokuwa satelaiti ya kwanza iliyozunguka Dunia angani.

Kiumbehai wa kwanza aliyefikishwa hadi anga-nje alikuwa mbwa Laika kwa njia ya satelaiti ya Sputnik 2. Mtu wa kwanza katika anga-nje alikuwa Mrusi Yuri Gagarin aliyezunguka Dunia mara moja tarehe 12 Aprili 1961 kwa Vostok 1.

Marekani ilifaulu kupeleka watu wa kwanza hadi uso wa mwezi tarehe 20 Julai 1969: hao walikuwa Neil Armstrong na Buzz Aldrin.

Tangu mwaka 1986 Umoja wa Kisovyeti ilianza kujenga kituo cha angani MIR kilichofuatwa na Kituo cha Anga cha Kimataifa ISS tangu 1998. Katika vituo hivyo wanaanga na wanasayansi kutoka nchi mbalimbali waliweza kukaa angani kwa miezi na kufanya utafiti wa mazingira ya anga-nje.

Usafiri waanga-nje umeendelea kwa kupeleka vyombo vya angani hadi sayari nyingine. Shabaha ya safari hizi ni upelelezi na utafiti wa kisayansi. Voyager 1 ni chombo cha kwanza kilichotoka katika mfumo wa jua letu mnamo mwaka 2012.

Katika mazingira ya karibu zaidi ya Dunia kuna satelaiti nyingi zinazozunguka sayari yetu na kutekeleza kazi hata za kibiashara kama vile upimaji wa hali ya hewa, kurusha programu za runinga na redio, kutuma data za GPS au za simu.

Marejeo hariri

  1. "The V2 and the German, Russian and American Rocket Program", C. Reuter. German Canadian Museum. p. 170. ISBN 1-894643-05-4, ISBN 978-1-894643-05-4