Yasinta Marescotti
Yasinta Marescotti, T.O.R. (Vignanello, Dola la Papa, leo Wilaya ya Viterbo, 1585 - Viterbo, 30 Januari 1640), alikuwa mwanamke mmonaki wa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko maarufu kwa vipaji vyake nchini Italia.
Anaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu bikira. Kwanza alitangazwa mwenye heri na Papa Benedikto XIII mwaka 1726, halafu mtakatifu na Papa Pius VII tarehe 14 Mei 1807.
Maisha
haririMtoto wa wazazi wa koo mashuhuri, Marcantonio Marescotti na Ottavia Orsini, alipobatizwa aliitwa Clarice.
Tangu utotoni alitumwa pamoja na dada yake Ginevra na mdogo wake Ortensia kwenye monasteri ya Mt. Bernardino ili kulelewa na masista Wafransisko wa Utawa wa Tatu.
Walipomaliza masomo yao, Ginevra, aliamua kujiunga na utawa, lakini Clarice alikuwa anavutwa na malimwengu kiasi cha kutofaidika na malezi ya kimonaki wala na muujiza uliomuokoa na kifo akiwa na umri wa miaka 17.
Alipofikia miaka 20 Clarice alitamani kuolewa na sharifu Capizucchi, lakini huyo alimchagua Ortensia. Hapo alizira, akajiunga na umonaki kwa jina jipya la Yasinta bila nia ya kuachana kweli na anasa.
Hivyo alikuwa na akiba binafsi ya chakula, alivaa kanzu ya gharama kubwa na kutembeleana na watu alivyotaka,kinyume cha nadhiri, ingawa alifuata ratiba ya sala kwa imani, akimheshimu Bikira Maria.
Aliishi hivyo miaka 15, mpaka alipougua sana akatembelewa na padri muungamishi ili kupewa Ekaristi. Mgeni wake alipoona wingi wa vitu alivyokuwanavyo chumbani, alimkaripia na kumtisha kwamba atakwenda motoni mwa milele.
Yasinta alitubu akaungama makosa yake mbele ya jumuia nzima mezani, aligawa nguo zake maridadi, alivaa kanzu kuukuu, alivua viatu, alifunga mara nyingi akila mkate na maji tu, alikesha usiku na kujichapa vikali, na kufanya malipizi mengine hata kuhatarisha uhai wake.
Tauni ilipotokea mjini, alihudumia waathirika kwa bidii kubwa.
Yasinta alianzisha vyama viwili (wanachama waliitwa "Sacconi"): kimoja ili kuchangishia walionusurika, fukara walioona aibu kuombaomba na wafungwa; kingine ili kuwapatia nyumba wazee. Pia alihamasisha ibada kwa Yesu Ekaristi.
Tanbihi
haririTazama pia
haririViungo vya nje
hariri- Catholic Encyclopedia "St. Hyacintha Mariscotti"
- Hyacinth at Patron Saints Index Ilihifadhiwa 20 Februari 2007 kwenye Wayback Machine.
- Saints of January 30: Hyacintha Mariscotti Ilihifadhiwa 25 Februari 2020 kwenye Wayback Machine.
- Santi e beati: Giacinta Mariscotti (Kiitalia)
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |