Mmonaki (kutoka Kigiriki μοναχός, monachos, "wa pekee") ni mwanamume au mwanamke anayefanya juhudi za pekee katika dini yake, akiishi peke yake au katika jumuia ya kitawa, ambayo nyumba yake inaitwa monasteri.

Wamonaki wa Ubuddha wakijadiliana katika Sera Monastery, Tibet
Abati wa monasteri ya Ubuddha anafundisha wanovisi, Uttaradit, Thailand.

Mwanzo wa umonaki wa Kikristo

hariri
 
Mt. Anthony Mkuu, anayetazamwa kuwa baba wa umonaki wa Kikristo

Tofauti na watawa walioishi katika mazingira ya kawaida, mwishoni mwa karne III huko Misri ulianza mtindo wa kukimbia ulimwengu hata kimakao.

Mmonaki alitafuta upweke kamili hasa jangwani ili kuishi na Mungu tu, ili moyo uweze kutulia kabisa bila ya kushikwa na mitindo na masharti ya maisha ya kawaida. Miundo mipya ya umonaki ilitegemea matatu: mwanzilishi, kanuni, upweke.

Mtindo huo wa maisha, ambao ndio mchango mkuu wa Afrika kwa Kanisa lote, ulistawi hasa baada ya Dola la Kirumi kuruhusu Ukristo (313). Maisha hayo magumu, yaliyoenea mapema hata nje ya Dola hilo, yaliamsha waamini wafuate Injili kwa juhudi kama wakati wa dhuluma, ulipohitajika ujasiri mbele ya hatari ya kuuawa. Hivyo umonaki ulionekana aina mpya ya kifodini kwa jinsi ulivyomtolea Mungu maisha yote.

Anayeheshimiwa kama baba wa wamonaki ni Antoni abati (251-356) ambaye akizingatia maneno mbalimbali ya Injili aliwagawia maskini utajiri wake mkubwa amfuate Mwokozi. Maisha yake yote akazidi kujitafutia mahali pa upweke kamili zaidi ili kumlenga Mungu tu.

Mfano wake ulivuta wanaume na wanawake wengi toka sehemu mbalimbali aliowaongoza bila ya kuacha upweke wake, isipokuwa kwa kutetea imani sahihi na umoja wa Kanisa. Mara baada ya kifo chake kitabu kilichoandikwa na Atanasi (295-373) juu yake kikaeneza mvuto wa umonaki hadi magharibi.

Maisha ya pamoja mashariki

hariri

Muda mfupi baadaye, na sehemu ileile, yalianzishwa maisha ya pamoja ambamo mali na vilevile mang’amuzi ya Kiroho yashirikishwe, hata kwa waamini wa ulimwenguni.

Pakomi (288-346) aliongokea imani kwa kuzingatia Wakristo walivyowatumikia wafungwa kwa upendo. Mang’amuzi hayo ya awali yalimuangazia kuwa Mungu ni upendo yakaathiri maisha na mafundisho yake yote. Hivyo baada ya kushika umonaki akajisikia wito wa kuishi kwa upendo na wengine akaanzisha maisha ya pamoja upwekeni Misri Kusini. Ndiye wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa, na ndani yake jina “ndugu” linashika nafasi ya “mmonaki”.

Kanuni hiyo ikaja kuathiri maisha ya wamonaki na kanuni zao mashariki na magharibi vilevile, na ndiyo inayoongoza umati wa wamonaki wa Ethiopia tangu mwaka 500 hivi. Mbali ya mafungo na sala ndefu, Pakomi alisisitiza kujikana kwa ajili ya wengine, yaani kuwa na utiifu, huruma na misaada ya kila aina: ndiyo njia ya upendo ambayo iliagizwa na Bwana na kufanya maisha ya pamoja yawe bora kuliko upweke kamili. Karibu na [[monasteri za kiume kulikuwa na nyingine za kike.

Pia Bazili Mkuu (330-379), baada ya kutembelea wamonaki sehemu mbalimbali, alianzisha maisha ya pamoja katika “jamaa” ambayo lengo lake kuu lilikuwa kushika kikamilifu udugu wa Kiinjili kama katika Kanisa la mwanzoni. Tofauti na monasteri ya Pakomi iliyofikia kuwa na maelfu ya watawa, jamaa hiyo haikuwa na idadi kubwa wala ngome; tena haikuwa jangwani, bali karibu na mji wa Kaisarea wa Kapadokia. Akiwa askofu huko alisisitiza uhusiano na Kanisa: watawa wa kiume na wa kike wawe chachu inayofanya Wakristo wenzao wafuate utakatifu wa wito wao; tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama vile kuhubiri na hasa kuhudumia wenye shida. Mtindo huo ulisisitiza ushirikiano kati ya ndugu kuliko uongozi wa abati na miundo mikubwa. Pia ulitia maanani masomo ya kidini.

Mpaka leo kanuni zake zinaongoza karibu wamonaki wote wa mashariki, na kwa njia yao makanisa ya Orthodoksi kwa kuwa kwao maaskofu kwanza ni wamonaki nao wanaelekeza Wakristo wote kufuata mifano yao.

Katika nchi ya jirani Mesrop (361-440) akaanzisha mtindo wa monasteri kuwa na shule karibu ili kuandaa watu watakaoendeleza elimu ya dini hasa kwa kutafsiri na kunakili vitabu. Mapema monasteri kubwa zikawa pia na seminari kuu au vyuo vikuu vya teolojia.

Huo umonaki wa Armenia ulidumisha utamaduni wa taifa hilo, ambalo lilikuwa la kwanza kupokea Ukristo jumla pamoja na mfalme wake (300) halafu likaushika moja kwa moja hata lilipopitia vipindi vigumu sana.

Maisha ya pamoja magharibi

hariri
 
Mmonaki aina ya Wabenedikto
 
Lebo ya Munich inakumbusha maana ya jina lake kama mji ulioanzishwa na Wabenedikto

Tangu karne ya IV umonaki ulienea magharibi pia: huko Italia, Ufaransa na Hispania kulikuwa na monasteri za kike na za kiume zilizosimamiwa na maaskofu watakatifu. Kati yao wa kwanza kupitia umonaki ni Martino wa Tours (316-397).

Hasa maandishi ya Yohane Kasiano (360-435) yalieneza hekima ya wamonaki wengi wa mashariki alioongea nao.

Agostino wa Hippo (354-430), babu wa Kanisa muhimu kuliko wote, baada ya kuongoka na kutembelea baadhi ya monasteri, alirudi Afrika Kaskazini aanzishe maisha ya pamoja. Kwanza aliishi na walei wenzake, halafu akiwa askofu aliishi na mapadri wake, akawashirikisha utajiri wake wa akili na roho ili wafanye vizuri utume. Katika kanuni yake, iliyotumika kwa wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe la utawa, si jambo lake mojawapo tu. Hata yeye aliathiri sana maisha ya kitawa ya magharibi kote.

Benedikto wa Nursia (480-547) ndiye aliyeunda umonaki wa magharibi kwa namna ya kudumu hasa kwa njia ya kanuni aliyoitunga polepole, kutokana na mang’amuzi yake, Kanuni ya Mwalimu asiyejulikana na mafundisho ya Bazili na mababu wengine wa jangwani.

Kanuni yake iliunganisha vizuri maelekeo mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi upwekeni na kuishi kwa umoja. Sifa yake nyingine ni mchanganuo mzuri wa sala na kazi mbalimbali ambazo ziliokoa elimu ya zamani na kufufua uchumi wa Ulaya Magharibi baada ya makabila ya Kijerumani kuvuruga kote. Yeye alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana abati ana nafasi ya pekee na ya kudumu kwa wamonaki, ambao aliwafafanua kuwa watu “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati mmoja”. Kwake monasteri ni shule ya utumishi wa Bwana, ambapo abati ndiye mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo za misusuko, Benedikto alidai udumifu katika monasteri.

Kutokana na kila monasteri kujitegemea, Wabenedikto wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na kanuni. Ushirikiano kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na mitindo yake.

Kati ya aina nyingine za umonaki wa magharibi inakumbukwa hasa ile ya Wakristo wa Kiselti (Ulaya visiwani). Hao hawakuwa na majimbo bali walimtegemea askofu-abati wa monasteri ya jirani na kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya mara kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa Kolumbani (540-615).

Hatimaye wakaja kukubali kanuni ya Benedikto pamoja na desturi za Kanisa la Roma.

Wamonaki wengine pia walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf. Augustino wa Canterbury (+605), aliyetumwa Uingereza na Papa Gregori I (540-604), mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, halafu Bonifas (672-754), mtume wa Ujerumani na mfiadini.

Marekebisho ya karne IX-XII

hariri
 
Monasteri ya Jasna Góra (Polandi).

Ni kawaida ya binadamu kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kuchoka, kuanza safari kwa kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi vya bidii na vya ulegevu.

Kanisa lenyewe, ingawa ni takatifu, linaathiriwa na ukosefu wa wanae. Ila Roho Mtakatifu haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili kulirekebisha.

Utawa unahusika kabisa na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili pia. Hasa katika karne ya IX-XII Kanisa la magharibi lilitambua wazi haja ya urekebisho katika umonaki na katika maisha yake yote.

Kati ya matawi mapya ya Kibenedikto yaliyotokana na juhudi hizo yanakumbukwa hasa lile la Cluny (ambalo lilikwepa kuwa mikononi mwa watawala likakazia [[liturujia kuliko kazi za mikono), lile la Camaldoli (lililofufua ukaapweke) na lile la Citeaux (ambalo lilirudia maisha magumu katika ufukara na kazi).

Wamonaki wa matawi hayo wakaja kushika nafasi muhimu katika kurekebisha Kanisa, hasa Petro Damiani (1007-1072), papa Gregori VII (1028-1085) na Bernardo wa Clairvaux (1090-1153).

Wakati huohuo Bruno (1035-1101) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na juhudi hadi leo (Wakartusi).

Utawa kati ya Wakristo wa madhehebu mengine

hariri

Pamoja na kudumisha moja kwa moja umonaki kati ya Waortodoksi, Roho Mtakatifu ameongoza Waprotestanti kadhaa kuanzisha upya maisha ya kitawa baada ya Martin Luther kuyafuta kama kitu kinyume cha Injili katika karne ya 16.

Kuanzia mwaka 1836 katika nchi mbalimbali watu wa madhehebu hayo walianza tena kuishi kijumuia kwa kufuata pengine mapokeo ya Kibenedikto na ya Kifransisko.

Maarufu zaidi ni Jumuia ya Taizé, ambayo ilianzishwa na ndugu Roger Schutz (1915-2005) na kupokea Wakatoliki pia; lengo lake hasa ni umoja wa Wakristo na kuinjilisha vijana.

Viungo vya nje

hariri