Martin Luther (10 Novemba 148318 Februari 1546) alikuwa Mkristo mwanateolojia kutoka nchi ya Ujerumani maarufu kama mwanzilishi wa Uprotestanti.

Martin Luther mwenye umri wa miaka 46

Kisha kushindana na Papa wa Roma, na kutengwa na Kanisa Katoliki, aliongoza Matengenezo ya Kiprotestanti yaliyosababisha mapema madhehebu mengi mapya kutokana na wazo kuu la kwamba Biblia inajitegemea na kumtosha kila anayesoma.

Aliandika vitabu vingi, kutunga nyimbo kadhaa na hasa kutoa tafsiri maarufu ya Biblia ya Kikristo katika lugha ya Kijerumani.

Athari yake imekuwa kubwa sana katika Kanisa na ulimwengu kwa jumla.

Maisha hariri

Utoto na ujana hariri

Alizaliwa mjini Eisleben katika familia ya Hans Luther na mke wake Margarethe. Hans Luther alitoka katika familia ya wakulima wadogo lakini alifaulu kupata mali katika migodi ya shaba ya Ujerumani ya Kati na kujenga maisha kama mchimba madini, mwenye tanuri ya kuyeyusha matapo na raia heshimiwa wa mji wake. Martin alikuwa mtoto wa kwanza akapokea jina kutokana na Mtakatifu Martin kwa sababu alizaliwa kwenye jioni ya sikuu ya mtakatifu huyu.

Babake alitaka kumsomesha sheria kwa sababu uanasheria ulikuwa nafasi kwa vijana raia kufikia vyeo vikuu katika jamii chini ya tabaka ya makabaila wakubwa waliotawala. Martin alitumwa kusoma shule katika miji mitatu alipojifunza Kilatini na misingi mingine ya elimu. Mwaka 1501 akiwa na umri wa miaka 17 aliingia katika Chuo Kikuu cha Erfurt. Jinsi ilivyokuwa kawaida kwa fani zote alianza masomo ya kimsingi katika idara ya sanaa iliyofundisha "sanaa huru saba" (sarufi ya Kilatini, kuhotubisha, mitindo ya falsafa, hisabati, jiometria, muziki na astronomia). Mwaka 1505 alimaliza kipindi hiki kwa "magister artium". Sasa baba alimtegemea kuendelea na masomo ya sheria.

Martin alianza masomo zake kwenye idara ya sheria hiko Erfurt mwaka uleule 1505. Baada ya wiki kadhaa alitembelea wazazi wake pale Mansfeld. Wakati wa kurudi alipatwa na [[|mvua ya radi|mvua kali ya radi]] akiwa njiani kwenye shamba pasipo na hifadhi. Katika hofu yake ya kupigwa na umeme wa radi alimwomba Mungu akaweka nadhiri kwamba akinusuriwa atamtolea Mungu maisha yake kabisa na kuwa mmonaki.

Utawani hariri

 
Chuo kikuu cha Wittenberg

Kwa sababu hiyo, ingawa hakuwa na wito huo, mwaka 1505 aliacha masomo ya sheria akajiunga na shirika la Waaugustino huko Erfurt akaweka nadhiri za kitawa, akasomeshwa elimu ya teolojia, akapadrishwa haraka mwaka 1507, akachukua digrii na kuwa dokta wa fani hiyo, akawa mwalimu wa teolojia ya Biblia katika chuo kikuu cha Wittenberg.

Katika nafasi hiyo alikazania ufafanuzi wa Maandiko matakatifu. Kanuni ya shirika pia ilikuwa inadai mmonaki asome na kutafakari Biblia, si kwa faida binafsi tu, bali pia kwa ajili ya wengine. Pamoja nayo, teolojia ya Luther iliathiriwa sana na mababu wa Kanisa, hasa Augustino. Pia alifaidika sana na waandishi wa kiroho wa karne ya 14 na 15, hasa Yohane Tauler, halafu Yohane wa Staupitz; kumbe alikuwa na mtazamo hasi kuhusu teolojia ya shule ya Karne za Kati.

Katika mafundisho yake alianza kujiuliza maswali kuhusu kiini cha imani. Alipoingia utawani alikuwa ametafuta amani ya kiroho kwa njia ya kujikana. Alisali amepiga magoti usiku kucha na kumuomba Mungu amhurumie, akafunga chakula muda mrefu, hata akajipiga kiboko akitaka kuzuia mawazo yenye dhambi. Lakini alishindwa kupata amani moyoni.

Hatimaye akasoma neno la Waroma 1:17: "Haki ya Mungu inadhihirishwa ndani ya Injili, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa: Mwenye haki ataishi kwa imani. (Kwa Kiswahili cha kisasa: Habari Njema inaonyesha wazi jinsi Mungu anavyowafanya watu wakubalike mbele yake; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho. Kama ilivyoandikwa: Mwenye kukubalika mbele yake Mungu kwa imani, ataishi)". Hapo Luther alianza kuelewa kwamba "Haki ya Mungu" si sheria yake inayomshtaki mwenye dhambi (alivyofundishwa mwenyewe), bali "haki ya Mungu" ni zawadi anayompa mtu mwenye dhambi na inayomwezesha kuishi kwa neema. Msalabani pa Kristo tunapata neema hii kwa imani tu.

Baada ya kuelewa hayo akajisikia amezaliwa upya. Hakuweza tena kufundisha maadili mema ya Kanisa kuwa njia ya kukubaliwa na Mungu. Hatuhesabiwi haki tukiacha mabaya na kujaribu kutenda mema, kwa sababu kila Mkristo amekuwa mtu mpya kwa ndani, lakini bado yumo katika mwili wenye dhambi. Anaweza kutambua hali hiyo na kupokea neema ya Mungu kama zawadi. Baada ya kuipokea ataishi upya akijaribu kumshukuru Mungu kwa maisha yake yote: kwa mawazo, maneno na matendo yake. Akianguka tena anapokea upya msamaha wa dhambi kwa njia ya kutubu.

Mawazo hayo yalimuongoza polepole padri Mkatoliki Luther kujiuliza juu ya desturi nyingi za Kanisa, lililoorodhesha matendo yaliyohesabiwa kuwa yanaleta neema, na juu ya mafundisho mbalimbali. Alidhani mawazo yake hayo si mapya, bali kwamba ndiyo mafundisho ya Mtume Paulo na ya Agostino wa Hippo. Maandiko yao yakawa mwongozo wake.

Chanzo cha kupinga mafundisho ya Kanisa hariri

Tatizo lilijiweka wazi Luther alipokutana na vyeti vya rehema kwa mara ya kwanza. Papa Julius II na Askofu mmoja Mjerumani walipatana kuendesha kampeni ya kuuza vyeti hivyo. Papa alihitaji hela kwa ajili ya ujenzi wa kanisa jipya la Mt. Petro kule Roma, ambalo mpaka leo ni kubwa kuliko yote duniani. Askofu alihitaji hela kulipia madeni yaliyobaki kutokana na kuwahonga waliomchagua kuwa askofu. Basi, walipatana kumuita mhubiri kwa jina Tetzel aendeshe kampeni ya kuuza vyeti vya rehema wakigawana mapato.

Mhubiri huyo alitangaza vyeti hivyo bila wasiwasi akisema vitawasaidia hata walioaga dunia. Mtu akimnunulia marehemu cheti kitamtoa mara moja katika moto wa toharani na kumrusha mbinguni. Katika huduma yake ya kipadri Luther alisikia Wakristo waliomuambia kwa furaha kuwa walisamehewa dhambi zao kwa kulipia vyeti vya rehema akaona jinsi watu wa kawaida walivyokimbilia kununua vyeti hivyo akashtuka. Hapo alianza kupinga mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu stahili za matendo mema.

Tarehe 31 Oktoba 1517, alitolea kimaandishi orodha ya "Hoja 95 dhidi ya rehema" (kwa Kijerumani: 95 Thesen wider den Ablass) za kupinga mafundisho juu ya vyeti hivyo na mengineyo, akakaribisha wataalamu wote kujadiliana naye. Orodha hiyo ilipigwa chapa na kusambazwa kote Ujerumani. Wakristo na mapadri wengi wenye elimu wakaelewa na kukubali hoja zake. Viongozi wa Kanisa wakaona hatari wakajaribu kumtisha anyamaze, lakini alijitetea kwamba hafundishi kinyume cha imani.

Miaka iliyofuata teolojia ya Luther ilikua haraka, ikisababisha mabishano mengine. Aliposhambuliwa alijitahidi kutetea msimamo wake na kujipatia watu wa kumuunga mkono dhidi ya waliotaka kumhukumu kuwa mzushi. Mengi yaliandikwa upande wake na dhidi yake, lakini mabishano pekee ya uso kwa uso yalifanyika huko Lipsia mwaka 1519, kati ya Andreas Bodenstein von Karlstadt na Luther upande mmoja, na mjumbe wa Papa, kwa jina Yohane Eck, upande wa pili.

Ni hapo kwamba upinzani wa Luther dhidi ya mafundisho juu ya rehema ukaenea kupinga yale juu ya mamlaka. Mwanzoni Luther aliona mamlaka ya Biblia, mababu wa Kanisa na mapokeo yake wanaunda umoja. Hata tarehe 13 Oktoba 1518, Luther alitamka rasmi, tena kwa nguvu, kwamba anakubaliana na Kanisa takatifu la Roma, ingawa hawezi kubadili msimamo bila kupata hakika ya kuwa amekosea. Tarehe 22 tena alisisitiza kuwa mafundisho yake hayapingani na ualimu wa Kanisa la Roma.

Kumbe katika kubishana na Eck, alipotambua kwamba msimamo wa Kanisa ulivyoelezwa na wawakilishi wake unapingana na Biblia alivyoielewa mwenyewe, umoja huo ulivunjika. Ni kwamba Eck alifaulu kumuonyesha mafundisho yake yalivyopinga msimamo wa Kanisa. Ndipo tu Luther alitambua jambo hilo, lakini alidai Mapapa na Mitaguso wamekosea mara nyingi, hivyo yeye anataka kufuata Biblia. Wakatoliki hawakuwa wanapinga nafasi ya kwanza ya Biblia katika imani, bali ufafanuzi wake binafsi. Lakini Luther aliposhindwa kuona msingi wa matamko ya Roma katika Biblia alianza kumfikiria Papa kama Mpingakristo, akaendelea kufundisha. Alipopelekewa barua ya Papa iliyomtishia kumtenga na Kanisa akaichoma moto mbele ya wanafunzi wake. Kwa hiyo tarehe 3 Januari 1521 akatengwa akatangazwa kuwa mzushi.

Baada ya kutengwa hariri

Hivyo Luther alitengwa na Kanisa, lakini wengi walimfuata. Mwaka huohuo Luther aliitwa mbele ya Bunge la Ujerumani ili ajitetee. Ni kwamba sheria za Dola Takatifu la Roma la Kijerumani zilidai mzushi akamatwe au hata auawe. Alipodaiwa na Bunge la Worms akane baadhi ya mafundisho yake, Luther akasimama mbele ya Mfalme mkuu na wakubwa wote akasema: "Nisipoonyeshwa kwa shuhuda za Biblia, na kwa hoja zinazoeleweka ya kwamba nimekosea, sitakana". Upande wake Kaisari Karolo V alitoa hotuba muhimu akijitambulisha kama mzao wa vizazi vingi vya watawala walioona daima ni wajibu wao kutetea imani katoliki «ili kuokoa watu» akasema naye ana wajibu huohuo. Alisisitiza kwamba mtawa mmoja anakosea anapodai kupinga Ukristo wa miaka elfu.

Hivyo Bunge hilo ulimhukumu Luther na kuagiza watawala wa maeneo wakomeshe kwa kila namna uzushi aliouanzisha. Hata hivyo, kwa kuwa hoja za Luther zilikubaliwa na wengi nchini, agizo hilo halikutekelezwa. Alitangazwa kuwa adui wa Kanisa na wa serikali lakini aliruhusiwa kurudi nyumbani. Maisha yake yalikuwa hatarini lakini mtawala wa eneo lake alimlinda.

Habari za Luther zilisikika kote Ulaya zikatokeza hamu ya urekebisho ya wengi, naye akashika nafasi muhimu zaidi na zaidi katika kubadili mafundisho na desturi vilivyoonekana kutegemea mamlaka ya binadamu tu na kupingana na Biblia kwa kiasi fulani. Ufafanuzi wa Injili uliotolewa na Luther ulifanya mapadri, wamonaki na wahubiri wengi zaidi na zaidi wauingize katika hotuba zao. Dalili za mabadiliko zilikuwa walei kupokea ekaristi kwa maumbo mawili, baadhi ya mapadri na watawa kuoa, taratibu za mafungo kuvunjwa, na pengine dharau dhidi ya picha takatifu na masalia.

Katika miaka iliyofuata alizidi kuandika vitabu vingi juu ya matengenezo ya Kanisa. Luther hakuwa na nia ya kuanzisha Kanisa jipya, bali alitaka kulirudisha lote kwenye msingi wa mafundisho ya Biblia alivyoyaelewa mwenyewe. Akaanza kupinga utajiri wa Kanisa na mamlaka ya Papa ilivyofundishwa wakati ule. Akapinga mafundisho ya utawa kuwa hali ya juu ya Ukristo. Watu wengi waliochoka hali mbaya ya Kanisa walisoma maandiko yake na kuwa na tumaini la matengenezo ya Kanisa zima. Ilipoonekana kwamba farakano litatokea, wengine wakaona afadhali kubaki ndani ya Kanisa kubwa. Mmojawao alikuwa mtaalamu mashuhuri Erasmo wa Rotterdam (Uholanzi).

Luther, akishirikiana na wenzake kadhaa wa Wittenberg, alitafsiri Biblia kwa Kijerumani ili watu wengi zaidi waweze kuisoma na kushika msimamo katika Kanisa. Kwa ajili hiyo aliomba viongozi wa serikali kuunda kotekote shule na kuwafundisha wavulana na wasichana, ambao wazazi wao walihimizwa sana kuwapeleka kusoma huko, akiwa na matumaini ya kwamba watu wenye elimu hawatafuata imani isiyo na msingi kama vyeti vya rehema.

Kwa sababu hakukuwa na mpango wala muundo kwa ajili ya kuratibu urekebisho huo, hali ilikuwa tofauti kati ya eneo na eneo. Hapo ilionekana haja ya kupanga ziara kwenye makanisa, na hizo zilihitaji idhini ya watawala. Hapo mwaka 1527 watetezi wa Luther walimuomba mtawala wa Sassonia aunde kamati maalumu, nayo ilianzisha aina ya utawala wa Kikanisa.

Ungamo la Augsburg ni mafundisho yaliyotungwa mwaka 1530 wafuasi wake walipodaiwa kujieleza mbele ya Bunge ili kurudisha umoja wa Kanisa. Lengo lake lilikuwa kuendeleza matengenezo, lakini pia kudumisha umoja huo. Katika sehemu ya kwanza (1-21) linafafanua mafundisho ya Kilutheri namna ya kuonyesha kwamba hayapingani na yale ya «Kanisa Katoliki au ya Kanisa la Roma». Sehemu ya pili inazungumzia mabadiliko yaliyoanzishwa na watengenezaji ili kurekebisha mambo kadhaa yaliyotazamwa kama «maovu» (22-28), ikieleza haja ya mabadiliko hayo. Ungamo hilo ni thibitisho tosha la nia ya Walutheri wa kwanza ya kubaki ndani ya Kanisa pekee linaloonekana.

Ni muhimu kujua kwamba Walutheri walisubiri hadi mwaka 1535 kubariki wachungaji wa kwao. Katika Ungamo la Augsburg walikuwa wametamka wako tayari kuwatii maaskofu ikiwa hao watakubali Injili ihubiriwe kadiri ya imani ya matengenezo yao. Kwa kuwa hiyo haikutokea, Walutheri walipaswa kuchaguaː ama kuendelea kutegemea upadrisho uliotolewa na maaskofu na hivyo kuacha kuhubiri namna mpya, ama kudumisha mahubiri hayo kwa kuweka wachungaji waliobarikiwa na wenzao, mbali na maaskofu. Hatimaye uamuzi ukawa huo wa pili, kwa kutegemea ufafanuzi fulani wa maneno ya Mtume Paulo.

Kwa jumla mafundisho ya Luther yalikubalika katika sehemu kubwa ya Ujerumani na nchi za jirani. Watawala wa nchi hizo waliona sababu mbalimbali za kufuata ushauri wake. Wengi waliona nafasi ya kutoka katika utawala wa Kanisa la Papa ulioendana na madai ya fedha. Pia walichoka utawala wa Waitalia walioongoza Kanisa. Wengine waliona nafasi ya kujichukulia mali ya Kanisa kwani, ikiwa hilo linatakiwa kuacha utajiri wake, mali hiyo itapatikana kwa matumizi mengine. Wengine walivutwa zaidi na mafundisho ya kiroho yenye nguvu.

Kanisa Katoliki pamoja na mfalme mkuu wa Ujerumani walijaribu kugandamiza wafuasi wa Luther, lakini watawala wengi wa maeneo mbalimbali walisimama upande wake. Nguvu ya serikali kuu ilidhoofishwa pia na vita dhidi ya Waturuki Waislamu walioshambulia mji wa Vienna, makao makuu ya ufalme wa Ujerumani. Mfalme alihitaji msaada wa watawala wote, wakiwemo wale waliomfuata Luther.

Huyo hakutaka kuleta farakano katika Kanisa, bali kulirudisha kwenye msingi wa Mitume wa Yesu. Kwa muda mrefu alikuwa na tumaini la kutokea Mtaguso Mkuu (mkutano wa Ukristo wote) utakaokubali mawazo yake. Alipoona matumaini hayo yameshindikana, alianza kutengeneza kanisa katika maeneo yaliyokubali mafundisho yake.

Alitunza desturi za kale zilizopatana na Biblia akafuta zile alizoziona kuwa kinyume. Akafuta ibada zilizoendeshwa kwa ajili ya marehemu kwa msingi wa kulipia: hivyo akaangusha nguzo muhimu ya kiuchumi ya Kanisa la kale. Alifuta kipaumbele kwa mapadri na watawa katika Ukristo. Akafundisha ya kwamba kila Mkristo ameshakuwa kasisi katika ubatizo wake. Akafuta sharti la wachungaji kutooa. Mwenyewe alitoka shirikani akamuoa sista aliyekimbia utawa akazaliana naye.

Akasisitiza Wakristo wote wapewe mafundisho juu ya imani akatunga Katekisimu. Akadai ibada ziendeshwe katika lugha za watu, si tena katika Kilatini, na mahubiri ya Biblia yawepo katika kila ibada. Aliona umuhimu wa wataalamu wa Biblia (walimu wa teolojia) kuwa na neno katika uongozi wa kanisa. Akadai wachungaji wawe wasomi waliopitia chuoni.

Juu ya sakramenti aliweka masharti mawili: kwanza ni ibada zile tu zilizoamriwa na Yesu mwenyewe, pili ziwe zinatajwa katika Biblia. Alieleza sakramenti kuwa alama ya nje (kama vile maji ya ubatizo, mkate na divai) inayounganishwa na neno la Mungu. Kwa sababu hiyo alifundisha sakramenti kuwa mbili tu (Ubatizo na Chakula cha Bwana), si saba tena. Akapinga sana Ekaristi (Misa) kuwa sadaka. Juu ya Kitubio kuwa sakramenti aliyumba: mwanzoni alikubali kwani imeamriwa na Bwana Yesu, baadaye alikataa kwani hakina alama ya nje.

Juu ya muundo wa Kanisa hakuwa na mawazo ya pekee. Kwake utaratibu wa nje ulikuwa jambo la pembeni, si lazima kwa wokovu. Kwake Kanisa lilikuwa hasa Mwili wa Kristo usioonekana na macho ambao umo ndani ya Kanisa linaloonekana. Akaona ni sawa Wakristo katika serikali wakilea Kanisa ambalo linajitawala chini ya usimamizi huo. Kumbe, katika maeneo yaliyofuata ushauri wake, Luther, bila kuwa na nia hiyo kweli, akafanya kanisa kuwa chombo cha serikali. Watawala wa maeneo mengi ya Ujerumani waliamua kutengeneza Kanisa kwenye msingi wa mafundisho ya Martin Luther.

Makanisa hayo huitwa ya Kilutheri. Kwa jumla husisitiza mafundisho ya Katekisimu zilizotungwa naye. Mafundisho yake yalipofanywa kuwa rasmi, katika Ujerumani makanisa ya Kilutheri yaliendeshwa kama idara za serikali za sehemu za Kilutheri chini ya uongozi wa wataalamu wa teolojia, lakini katika karne ya 20 kanisa na serikali zilitengana. Kumbe hali hiyo inadumu mpaka leo katika nchi za Skandinavia (Sweden, Norway, Denmark n.k.) ambapo wafalme waliamua kugeuza Kanisa zima la nchi zao kuwa la Kiinjili-Kilutheri. Ila Sweden Walutheri waliendelea na cheo cha uaskofu na desturi nyingi za Kanisa la kale, wakifanana zaidi na Waanglikana wa Uingereza. Baadaye madhehebu ya Kilutheri yalienea kule ambako Wajerumani na Waskandinavia walihamia, kama vile Marekani. Barani Afrika Walutheri wako hasa katika nchi zilizokuwa makoloni ya Ujerumani, kama vile Tanzania, Namibia na Kamerun, lakini pia Ethiopia.

Viongozi mbalimbali wakaiga mfano wa Luther, ila juhudi zao zikatofautiana: ndio mwanzo wa madhehebu mengine yanayoitwa ya "Kiinjili".

Luther aliendelea kutoa mafundisho kwa ajili ya Kanisa linalofuata maagizo ya Mitume jinsi alivyoelewa mwenyewe[1]. Katika juhudi zake za kumfuata Paulo aliweka pembeni hata baadhi ya vitabu vya Biblia, akidharau hasa Waraka wa Yakobo. Alipinga vikali Waprotestanti waliotofautiana naye juu ya masuala kadhaa, akishindwa kukubali kwamba nao wanaweza kuelewa Biblia namna yao[2].

Alipokufa mwaka 1546 mafarakano ya kudumu yalikuwa yameshatokea katika Kanisa, si tu kati ya Wakatoliki na Walutheri, bali pia kati ya Waprotestanti waliotafsiri Biblia kwa namna tofautitofauti.

Tathmini hariri

Vitabu vya Luther viliendelea kuwa na athari kubwa. Kati ya maandiko hayo mengi, muhimu ni hasa Katekisimu Ndogo, yaani mafundisho kwa ajili ya vijana Wakristo, na pia Katekisimu Kubwa kwa ajili ya wachungaji. Kwa jumla mafundisho yake yamekuwa muhimu katika madhehebu yote ya Kiprotestanti, si tu katika makanisa yanayoitwa ya "Kilutheri". Ndiye aliyefungua mlango walipopitia wengine waliojulikana baadaye kama Wabatisti, Wakalvini, Waanglikana n.k. lakini wote walitegemea sehemu za mafundisho yake. Hata Umoja wa Ndugu (Wamoravia) uliomtangulia, baadaye ulimfuata katika mafundisho kadhaa, kama vile juu ya sakramenti au juu ya neema ya Mungu.

Wakristo, wawe Waprotestanti au Wakatoliki, hawawezi kukwepa nafsi na ujumbe wa mtu huyo mwenye hisia kali za kidini. Kilichomkosesha raha ni suala la Mungu, ambalo lilimtawala na kumsukuma katika safari ya maisha yake. “Nitawezaje kuwa na Mungu mwenye huruma?”: swali hilo lilikuwa linachoma moyo wake na kuathiri utafiti wake na mapambano yake ya ndani. Kwa Luther teolojia haikuwa suala la elimu tu, bali mapambano na nafsi yake kuhusu Mungu na hatimaye na Mungu mwenyewe. Swali hilo lililomtesa kwa muda mrefu lilijibiwa aliposoma Waraka kwa Waroma, sura ya 3, mstari wa 24: "kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa." Alimkuta huyo Mungu mwenye huruma katika Injili ya Yesu. Aliandika, «Katika Kristo msulubiwa vinapatikana teolojia halisi na ujuzi wa Mungu».

Siku hizi Wakatoliki na Waprotestanti wanazidi kuelewana, kushirikiana na kuheshimiana. Wanatambua kwanza kinachowaunganisha ambacho ni zaidi ya kile kinachowatenga: kwanza imani ileile katika Mungu mmoja mwenye nafsi tatu, ufunuo wake, mafundisho makuu kuhusu wokovu n.k. Kuna ushirika halisi, ingawa si kamili, kati ya wale wote waliomuamini Yesu Kristo na kubatizwa.

Hivyo Wakatoliki wanamuangalia Luther tofauti na zamani. Kwa kipindi kirefu cha maisha yake alikuwa Mkristo na padri wa Kanisa Katoliki. Kwa jumla kwa Wakatoliki mafumbo ya imani yana pande mbili ambazo zisitenganishwe hata zikionekana kupingana: kumbe Luther alipenda kusisitiza mmoja na kukanusha mwingine. Hivyo kwa Wakatoliki mara nyingi alichokiri ni sahihi, alichokanusha si sahihi. Jinsi alivyopinga Upapa na sakramenti saba haiwezi kukubaliwa na Wakatoliki, lakini katika mambo kadhaa anaweza kueleweka. Tatizo lenyewe lililokuwa chanzo cha farakano lile, yaani vyeti vya rehema, miaka michache baadaye liliondolewa na Kanisa lenyewe. Mtaalamu mmoja alisema: “Luther asingetengwa na Kanisa Katoliki la leo, wala mwenyewe asingejitenga siku hizi".

Walutheri wa leo wanakumbuka kwa masikitiko kauli za kikatili za Martin Luther dhidi ya Wayahudi zilizochangia chuki dhidi yao iliyofikia kilele chake katika karne ya 20, Ujerumani wa Hitler ulipojaribu kuwamaliza wote. Wanalaumu pia dhuluma dhidi ya Wabatisti ambazo Martin Luther alizitetea kiteolojia. Tena wanasikitikia jinsi alivyohamasisha watawala kukomesha wakulima katika vita dhidi yao. Hatimaye hawawezi kukubali hoja zake za kumfanya Papa kuwa ndiye Mpingakristo, hata kama Mapapa walistahili lawama mbalimbali.

Tanbihi hariri

  1. "'Je, unadhani walimu wote wa zamani hawakujua? Je, babu zetu wote walikuwa wajinga? Je, wewe tu umeangazwa na Roho Mtakatifu siku hizi za mwisho? Je, Mungu aliacha taifa lake lipotee miaka mingi hivi?'... Mara ngapi moyo wangu ulidunda, uliniadhibu na kunikemea kwa hoja yake pekee na ya nguvu sana! 'Je, wewe tu una hekima, eti, wengine wote wanakosea na wamekosea muda mrefu hivi? Na ikiwa unakosea wewe na kuvuta watu wengi wakosee, wangapi watalaaniwa milele?" (Toleo la Weimar, 1883)
  2. «Sikubali mafundisho yangu yahukumiwe na yeyote, hata kama ni malaika. Asiyekubali mafundisho yangu hawezi kufikia wokovu». (Toleo la Weimar X, P. II, 107, 8-11)

Marejeo hariri

 
Tomus secundus omnium operum, 1562

Marejeo mengine hariri

  • Atkinson, James (1968). Martin Luther and the Birth of Protestantism, in series, Pelican Book[s]. Harmondsworth, Eng.: Penguin Books. 352 p.
  • Erikson, Erik H. (1958). Young Man Luther: A Study in Psychoanalysis and History. New York: W. W. Norton.
  • Dillenberger, John (1961). Martin Luther: Selections from his Writings. Garden City, NY: Doubleday. OCLC 165808. 
  • Friedenthal, Richard (1970). Luther, His Life and Times. Trans. from the German by John Nowell. First American ed. New York: Harcourt, Brace, Jovanovich. viii, 566 p. N.B.: Trans. of the author's Luther, sein Leben und seine Zeit.
  • Lull, Timothy (1989). Martin Luther: Selections from his Writings. Minneapolis: Fortress. ISBN 0-8006-3680-5. 
  • Lull, Timothy F.; Nelson, Derek R. (2015). Resilient Reformer: The Life and Thought of Martin Luther. Minneapolis, MN: Fortress. ISBN 978-1-4514-9415-0 – via Project MUSE. (subscription required (help)). 
  • Kolb, Robert – Dingel, Irene – Batka, Ľubomír (eds.): The Oxford Handbook of Martin Luther's Theology. Oxford: Oxford University Press, 2014. ISBN 978-0-19-960470-8.
  • Luther, M. The Bondage of the Will. Eds. J. I. Packer and O. R. Johnson. Old Tappan, N.J.: Revell, 1957. OCLC 22724565.
  • Luther, Martin (1974). Selected Political Writings, ed. and with an introd. by J. M. Porter. Philadelphia: Fortress Press. ISBN 0-8006-1079-2
  • Luther's Works, 55 vols. Eds. H. T. Lehman and J. Pelikan. St Louis Missouri, and Philadelphia, Pennsylvania, 1955–86. Also on CD-ROM. Minneapolis and St Louis: Fortress Press and Concordia Publishing House, 2002.
  • Maritain, Jacques (1941). Three Reformers: Luther, Descartes, Rousseau. New York: C. Scriber's Sons. N.B.: Reprint of the ed. published by Muhlenberg Press.
  • Nettl, Paul (1948). Luther and Music, trans. by Frida Best and Ralph Wood. New York: Russell & Russell, 1967, cop. 1948. vii, 174 p.
  • Reu, Johann Michael (1917). Thirty-five Years of Luther Research. Chicago: Wartburg Publishing House.
  • Schalk, Carl F. (1988). Luther on Music: Paradigms of Praise. Saint Louis, Mo.: Concordia Publishing House. ISBN 0-570-01337-2
  • Stang, William (1883). The Life of Martin Luther. Eighth ed. New York: Pustet & Co. N.B.: This is a work of Roman Catholic polemical nature.
  • Warren Washburn Florer, Ph.D (1912, 2012). Luther's Use of the Pre-Lutheran Versions of the Bible: Article 1, George Wahr, The Ann Arbor Press, Ann Arbor, Mich. Reprint 2012: Nabu Press, ISBN 1278818197 ISBN 9781278818191

Viungo vya nje hariri

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.