Dhabihu ya wanadamu

Dhabihu ya wanadamu ni kitendo cha ibada cha kumuua mwanadamu kama sadaka kwa mungu fulani au mizimu.

Mchoro wa dhabihu ya wanadamu kwa Waazteki.

Ilifanywa katika tamaduni nyingi za kale, ila utekelezaji wake ulikuwa tofauti katika tamaduni tofauti. Wengine kama Wamaya, Waazteki na huko Dahomey wanajulikana kwa mauaji yao ya kimila, lakini wengine waliidharau.

Wahanga waliuawa kiibada kwa njia ambayo ilitakiwa kufurahisha au kutuliza miungu au mizimu. Wahanga walikuwa mara nyingi wafungwa na watoto wachanga. Kati ya Waazteki tumbo lilikatwa kwa visu na mioyo ilichomwa moto.

Katika mwendo wa historia dhabihu ya wanadamu imepungua kote ulimwenguni. Sasa dhabihu za aina hii ni za nadra sana. Dini nyingi zinalaani kitendo hicho na sheria za siku hizi zinaitazama kama jinai, walakini bado inaonekana mara kadhaa hadi leo, hasa katika maeneo ambako imani za kimila zinaendelea.

Finisia hariri

Utamaduni wa Finisia katika Mashariki ya Kati ya Kale ulikuwa na kawaida wa dhabihu ya watoto kwa mungu wao Moloki. Katika Biblia desturi hiyo inatajwa kama kielelezo cha ubaya.

Ulaya hariri

Waandishi wa Roma ya Kale walitunza habari za dhabihu ya wanadamu kati ya Wakelti katika Gallia (Ufaransa ya leo) na Hispania. Kufuatana na habari hizo ilikuwa kawaida kuzika watumwa na watumishi pamoja na machifu waliofariki.

Wagermanik wa Kale walifanya dhabihu ya maafisa Waroma wafungwa kwenye madhabahu ya miungu yao baada ya kushinda legioni za Varus mnamo mwaka 9 BK[1].

Waazteki hariri

Waazteki walijulikana sana kwa kufanya dhabihu za wanadamu kwa kiwango kikubwa; sadaka nyingi zilitolewa kwa mungu Huitzilopochtli waliyoabudu kama mungu wa Jua; waliamini kwamba walihitaji kumlisha kwa njia ya sadaka kwa hofu ya kwamba Jua linaweza kuzimika. Dhabihu za wanadamu ziliaminiwa kuzuia mwisho wa ulimwengu ambao unaweza kutokea kwa kila kipindi cha miaka 52. Waazteki walikuwa na mikataba na madola ya jirani ili wakutane kila mwaka katika vita waliyotumia kukamata wafungwa kwa ajili ya sadaka hizo.

Dola ya Inka hariri

Katika maeneo ya milki ya Inka wanaakiolojia wamekuta mumia ya watoto waliotolewa kama sadaka. [2]

Afrika ya Magharibi hariri

Dhabihu za wanadamu zilitokea mara kwa mara katika milki za Afrika ya Magharibi kama Dahomey na Benin hadi karne ya 19. Sadaka za aina hiyo zilikuwa kawaida hasa baada ya kifo cha mfalme au malkia. Kuna taarifa za kimaandishi zilizotaja idadi ya wafungwa mamia au hata maelfu waliotolewa sadaka kwenye nafasi hizo. Huko Dahomey kulikuwa na ibada ya kila siku ambapo watumwa kama 500 walitolewa sadaka.

Makala hariri

  • "Ibada ya India inaua watoto kwa mungu wa kike: Wanaume watakatifu wanalaumiwa kwa kuchochea vifo vya watu wengi", The Observer (gazeti la Uingereza) Dan McDougall huko Khurja, India, Jumapili Machi 5, 2006
  • Heinsohn, Gunnar: "Kuongezeka kwa Dhabihu ya Damu na Ufalme wa Kuhani huko Mesopotamia: Amri ya Urembo?" [3] (pia ilichapishwa katika Dini, Juz. 22, 1992)

Marejeo hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.