Mumia (kutoka Kiarabu مومياء mumia; pia: mumiani; kwa Kiingereza: mummy) ni maiti wa binadamu au mzoga wa mnyama iliyokauka bila kuoza. Hali hiyo inaweza kutokea kiasili katika mazingira maalumu au kwa kutumia mbinu fulani. Mchakato wa kuoza huzuiwa na baridi kali, katika mazingira yabisi (pasipo na unyevu hewani) na mwendo wa hewa, kwa kukosa oksijeni au kwa kutumia kemikali fulani.

Jina hariri

Jina la mumia lilitumiwa mwanzoni kwa kimiminika cha lami likawa jina la maiti aliyekaushwa kwa kutumia lami yaliyopatikana hasa Misri ya Kale likaendelea kutumiwa kwa maiti wote waliokauka bila kuoza.[1]

Neno la Kiswahili linatokana na Kiarabu مومياء mumia. Kiasili neno hili lilitaja lami ya kumiminika [2] iliyotumiwa kama dawa na pia kwa kuzuia kuoza kwa maiti waliotakiwa kuhifadhiwa kulingana na imani mbalimbali katika dunia ya kale.

Ilhali "mumia" ilikuwa kiasili miminika ya lami pekee, neno hili lilitumiwa baadaye pia kwa maiti waliokaushwa na kupatikana katika makaburi ya Misri ya Kale. Desturi ya kukausha na kutunza maiti kwa kutumia dawa mbalimbali ilikwisha baada ya mwisho wa dini ya Misri ya Kale kutokana na uenezaji wa Ukristo na baadaye Uislamu nchini. Lakini katika tabianchi yabisi ya Misri maiti wa zamani walikaa wakapatikana kwa wingi. Walionekana nyeusinyeusi hivyo watu waliona walitibiwa na "mumia" na kile cheusi kutoka makaburi kilitumiwa pia kama dawa.

Baadaye matabibu wa Misri waliona kwamba ilifaa pia kutumia vipande vya maiti hao kama dawa.[3].

Baadaye tena wataalamu wa Ulaya, waliojifunza mengi kutoka tiba ya Waislamu, walipokea maelezo hayo wakaanza kununua maiti waliokaushwa kutoka Misri. Ilhali matumizi ya maiti kama dawa yalipungua katika nchi za Waislamu kuanzia karne ya 16 yaliendelea katika nchi za Ulaya hadi karne ya 19[4].

Mumia za Misri hariri

 
Mumia ya mtoto wa Misri ya Kale, isiyofunguliwa.

Utamaduni wa Misri ya Kale unajulikana kwa dini yake iliyofundisha ni muhimu kutunza mwili ili mtu aweze kuzaliwa upya akiingia peponi baadaye. Wamisri walitumia mbinu mbalimbali kwa kutunza miili ya marehemu. Utumbo na ubongo vilitolewa na kutunzwa katika vyombo vya pekee baada ya kuvikausha katika chumvi. Mwili uliofunguliwa ulipakwa chumvi kwanza, baadaye na mchanganyiko wa nta, utomvu wa miti wenye harufu nzuri na lami. Baadaye mwili uliviringishiwa bendeji za kitambaa kilicholoweshwa kwa dawa mbalimbali, pamoja na lami. Shughuli hizo zote zilitekelezwa na mafundi maalumu waliosimamiwa na makuhani. Wamisri ambao familia zao hazikuwa na uwezo wa kugharamia shughuli hizo zote waliandaliwa kwa mbinu sahili zaidi. Maskini walizikwa kwenye mchanga wa jangwa ambako mara nyingi maiti wao pia walikauka kabisa.

Wamisri walihifadhi pia miili ya wanyama hasa wanyama waliotazamwa kuwa ishara ya miungu yao na kufugwa mahekaluni. Kwa jumla ni zaidi ya mumia milioni moja ya wanyama, hasa paka, zinazojulikana[5].

Mumia za nchi nyingine hariri

Wamisri wa kale hawakuwa peke yao kuwa na utamaduni wa kujitahidi kutunza miili ya marehemu. Hasa katika mazingira ambako tabianchi ni yabisi sana kuna mifano ya miili inayohifadhiwa vema bila kuoza. Hasa Amerika Kusini kabla ya kufika kwa Wahispania, watu kama Wainka walijua mbinu za kutunza miili ya marehemu [6]

Mumia asilia hariri

 
Mumia asilia ya mtoto, utamaduni wa Wainka, mnamo mwaka 1500 BK.

Mumia asilia hutokea

 • kama mwili unatunzwa penye mchanga au mwamba unaonyonya kimiminika: hapo vimiminika kutoka maiti hupotea haraka na hivyo bakteria zinazoozesha mwili hazina mazingira ya kustawi[7]
 • mumia zilipatikana mara kadhaa kama mtu walikufa katika migodi ya chumvi[8]
 • pale ambako mtu alikufa au alizikwa penye baridi, kwa mfano katika barafuto au kwenye taiga[9]
 • kama kuna upepo baridi mahali mwili unapokaa, kwa mfano ndani ya mapango kadhaa[10]
 • kama ardhi ya kaburi ina kemikali au asidi ndani yake zinazoua bakteria

Tanbihi hariri

 1. Wiedmann,Alfred: Mumie als Heilmittel, Zeitschrift des Vereins für rheinische und westfälische Volkskunde, 1906, uk. 1-38, online hapa
 2. Mumia naturalis persica, bitumen, mineral tar, tazama makala MŪMIYĀɔ, The Encyclopedia of Islam, Vol. 7, Mif–Naz, Edited by C. E. Bosworth, E. van Donzel, W.P. Heinrichs and Ch. Pellat, Assisted by F.Th. Dijkema (pp. 1–384), P. J. Bearman (pp. 385–1058) and Mme S. Nurit, 1993. ISBN 90-04-09419-9 Brill
 3. Tabibu Mmisri Ibn Rodhwan aliandika mnamo mwaka 1047 BK akaeleza inafaa kukata vipande vya "mumia" (maiti zilizokaushwa kwa kutumia lami kutoka makaburi ya kale) na kuvichanganya na nafaka, divai na viungo vingine halafu kupata kimiminika kinachotokea kama dawa; tazama Wiedmann, Mumie uk. 6
 4. Wiedmann, Mumie, uk.37-38
 5. Egyptian Animals Were Mummified Same Way as Humans, jarida la National Geographic, September 15, 2004, iliangaliwa Juni 2019
 6. Bernardo T. Arriaza, Russell A. Hapke, Vivien G. Standen; Making the Dead Beautiful: Mummies as Art, 1998 by the Archaeological Institute of America
 7. Wade, Nicholas (15 March 2010). "A Host of Mummies, a Forest of Secrets". New York Times. Retrieved 9 November 2013.
 8. Ancient salt mining and salt men: the interdisciplinary Chehrabad Douzlakh project in north-western Iran, katika jarida la "Antiquity A Review of World Archaeology", Issue 333, Volume 86, September 2012
 9. Greenland Mummies , tovuti ya The World Mummies, iliangaliwa Juni 2019
 10. The Czech's Capuchin Crypt, Mummified monks and the accidentally interred, in a 17th-century crypt. , tovuti ya atlasobscura

Marejeo hariri

 • Aufderheide, Arthur C. (2003). The Scientific Study of Mummies. Cambridge: Cambridge University Press. ISBN 0-521-81826-5.
 • Barber, Elizabeth Wayland. 1999. The Mummies of Ürümchi. 1999. London. Pan Books. Also: W. W. Norton & Company. ISBN 0-393-04521-8.
 • Budge, E.A.Wallis. 1925. The Mummy, A Handbook of Egyptian Funerary Archaeology. Dover Publ. Inc., New York, Dover Ed. 1989, (512 pgs.) ISBN 0-486-25928-5.
 • Davis-Kimball, Jeannine, with Behan, Mona. 2002. Warrior Women: An Archaeologist’s Search for History’s Hidden Heroines. Warner Books, New York. First Trade Printing, 2003. ISBN 0-446-67983-6.
 • Ilkerson, Bill. 2006. Wrap-It-Up: How My Lost Child Will Survive Us All. Portland. Eye of Raw Texts. ISBN 0-439-56827-7.
 • Mallory, J. P. and Mair, Victor H. 2000. The Tarim Mummies: Ancient China and the Mystery of the Earliest Peoples from the West. Thames & Hudson. London. 2000. ISBN 0-500-05101-1.
 • Heather Pringle. 2001. Mummy Congress: Science, Obsession, and the Everlasting Dead. Penguin Books. ISBN 0-14-028669-1.
 • Taylor, John H. 2004. Mummy: the inside story. The British Museum Press. ISBN 0-7141-1962-8.

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mumia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.