" Hansel na Gretel " (kwa Kijerumani: Hänsel und Gretel) ni kati ya ngano zilizosimuliwa katika vijiji vya Ujerumani wakati wa karne ya 19. Akina Grimm waliisikia walipokusanya urithi wa ngano katika eneo la Kassel, Ujerumani wakaichapisha katika Ngano za Watoto na Kaya mnamo 1812. Akina Grimm waliendelea kuhariri hadithi katika miaka iliyofuata hadi toleo lao la mwisho la mwaka 1857.

Bibi Mchawi jinsi alivyokaribisha watoto, Mchoro na Arthur Rackham, 1909
Gretel jinsi alivyomsukuma bibi mchawi katika tanuri

Masimulizi yake yalitumiwa kwa kazi za sanaa mbalimbali kama vile opera ya Hänsel und Gretel (1893) ya Engelbert Humperdinck. Kuna pia filamu kadhaa zilizopigwa kwenye msingi wa nago na pia ya opera.

Masimulizi hutunza kumbukumbu ya umaskini mkali jinsi ulivyotokea katika karne zilizotangulia.

Hadithi

hariri

Hansel na Gretel ni kaka na dada wadogo, watoto wa mpasua mbao maskini. Wakati wa njaa kubwa wazazi hawana chakula cha kutosha tena. Mama wa kambo anaamua watoto wapelekwe msituni na kuachwa peke yao. Watoto wanajifunza mpango wa wazazi kwa kuwasikiliza kwa siri na mara mbili wanafaulu kurudi nyumbani kwa kuacha mawe madogo njiani wanapopelekwa. Mama wa kambo anasikitika lakini wanapokewa. Hatimaye baada ya kurudi kwa njaa kali, baba anawaambia tena watoto waje wamsindikize akienda msituni kukata miti na safari hii anafaulu kuwaacha sehemu wasipofahamu.

Watoto wanajikuta msituni wanatembea ovyo hadi kufika kwenye nyumba ya ajabu iliyoundwa na keki na pipi. Wakiwa na njaa kali wanavunja keki kidogo kutoka dari na kula. Kumbe mlango unafunguliwa na bibi mzee anatoka nje na kuwakaribisha watoto waingie ndani. Nyumba hiyo ni makazi ya bibi mchawi anayemfunga Hansel katika kizimba ya chuma. Anamlazimisha Gretel kuwa mhudumu wake. Anamlisha Hansel chakula kizuri kwa sababu anataka kumnenepesha na kumla. Ilhali bibi mchawi hawezi kuona vizuri anafika kila asubuhi kwenye kizimba akitaka kushika kidole cha Hansel aone kama ameshanenepa. Gretel anajua mpango wake akimpa Hansel mfupa na bibi mchawi akiushika mfupa anashangaa Hansel hajanenepa bado. Hatimaye anachoka anaamua atamla kama amenenepa au la.

Wakati bibi mchawi anaandaa tanuri kwa kumpika mtoto, anaamua ni vema kumla Gretel pia. Anamwambia afunue mlango wa tanuri na kuangalia kama moto unatosha. Gretel anajifanya kama hamwelewi na anamwomba bibi mchawi kumwonyesha anamaanisha nini. Wakati mchawi anafungua mlango wa tanuri na kumwonyesha jinsi ya kuweka kichwa chake katika nafasi, Gretel anamsukuma kutoka nyuma hadi mchawi anaangukia motoni. Gretel anafunga mlango na bibi mchawi anachomwa hadi kuwa majivu.

Gretel anafungua kizimba na kumweka Hansel huru. Kwa pamoja wanachungulia nyumba ya mchawi wanapokuta masanduku ya dhahabu na almasi.

Watoto wanajaza mifuko yao almasi na dhahabu wakiondoka na kutafuta njia ya kurudi nyumbani. Bata-maji mkubwa anawasaidia kufika. Hapo wanamkuta baba peke yake maana mama wa kambo ameshafariki. Baba aliyekuwa na huzuni kubwa juu ya tendo lake dhidi ya watoto anafurahi mno kuwaona tena. Watoto wanatoa utajiri wao, na sasa njaa yote imekwisha: wanaishi pamoja kwa furaha na bila matatizo yoyote.

Marejeo

hariri
    • Opie, Iona and Peter. 1974. The Classic Fairy Tales. Oxford UP. pp. 236-7.
    • Tatar, Maria. 2002. The Annoted Classic Fairy Tales. Norton. pp. 44-5.
    • Zipes, Jack (Ed.) 2002. The Oxford Companion to Fairy Tales. Norton. pp. 225-6.

Kujisomea

hariri
  • Delarue, Paul (1956). The Borzoi Book of French Folk-Tales. Alfred A. Knopf, Inc.
  • Goldberg, Christine (2008). "Hansel and Gretel". Katika Haase, Donald (mhr.). The Greenwood Encyclopedia of Folktales and Fairy Tales (kwa Kiingereza). Greenwood. ISBN 978-0-313-04947-7.
  • Jacobs, Joseph (1916). European Folk and Fairy Tales. G. P. Putnam's sons.
  • Lüthi, Max (1970). Once Upon A Time: On the Nature of Fairy Tales. Frederick Ungar Publishing Co.
  • Opie, Iona; Opie, Peter (1974). The Classic Fairy Tales. Oxford University Press. ISBN 978-0-19-211559-1.
  • Tatar, Maria (2002). The Annotated Classic Fairy Tales. BCA. ISBN 978-0-393-05163-6.
  • Thompson, Stith (1977). The Folktale (kwa Kiingereza). University of California Press. ISBN 978-0-520-03537-9.
  • Wanning Harries, Elizabeth (2000). "Hansel and Gretel". Katika Zipel, Jack (mhr.). The Oxford Companion to Fairy Tales (kwa Kiingereza). Oxford University Press. ISBN 978-0-19-968982-8.
  • Zipes, Jack (1997). "The rationalization of abandonment and abuse in fairy tales: The case of Hansel and Gretel". Happily Ever After: Fairy Tales, Children, and the Culture Industry (kwa Kiingereza). Routledge. ISBN 978-1-135-25296-0.
  • Zipes, Jack (2013). "Abandoned Children ATU 327A―Hansel and Gretel". The Golden Age of Folk and Fairy Tales: From the Brothers Grimm to Andrew Lang. Hackett Publishing. ku. 121ff. ISBN 978-1-624-66034-4.
  Makala hii kuhusu kitabu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hansel na Gretel kama Mwandishi wake, hadithi au matoleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.