Historia ya Masedonia Kaskazini
Historia ya Masedonia Kaskazini inahusu eneo ambalo siku hizi linaunda Jamhuri ya Masedonia Kaskazini.
Masedonia ya Kale
haririKatika karne za kabla ya Kristo Masedonia ilikuwa eneo la kaskazini la Ugiriki. Wakazi wake wanaaminiwa walisema lahaja za Kigiriki, lakini mara nyingi hawakutambuliwa na Wagiriki wenyewe kama wenzao, jinsi tunavyojua kutoka waandishi wa Ugiriki wa Kale.
Mnamo 500 KK kulikuwako ufalme ulioitwa Masedonia ambao ulihesabiwa kama sehemu ya utamaduni wa Ugiriki wa kale na wafalme waliruhusiwa kwenye michezo ya Olimpiki ya madola ya Wagiriki.
Pamoja na sehemu nyingi za Ugiriki ufalme huo ulipaswa kukubali ubwana wa Milki ya Uajemi, lakini mfalme Filipo II wa Masedonia alifaulu, kuanzia mnamo mwaka 360 KK, kurudisha uhuru wa ufalme akaendelea kuifanya Masedonia kuwa dola kiongozi kati ya madola madogo ya Ugiriki.
Mwanawe Aleksanda Mkuu aliimarisha utawala wake juu ya Wagiriki wengine na kushambulia Milki ya Uajemi na hatimaye kuivamia na kuishinda kwa jeshi kutoka sehemu zote za Ugiriki.
Mnamo mwaka 325 KK mfalme wa Masedonia alitawala nchi zote kuanzia Ugiriki hadi Misri, Syria, Uajemi, mipaka ya Uhindi na Asia ya Kati.
Baada ya kifo cha Aleksanda mnamo 323 KK milki yake iligawiwa, na Masedonia ilikuwa tena ufalme wa pekee.
Ikaendelea kwa kujitegema hadi uenezi wa Dola la Roma ambapo ikawa jimbo la Kiroma tangu mwaka 147 KK.
Baadaye ufalme wa awali uligawiwa katika majimbo mbalimbali. Wakazi walibadilika polepole kutokana na uhamiaji ndani ya Dola la Roma.
Kufika kwa Waslavi
haririTangu karne ya 6 BK makabila ya Waslavi yalifika katika sehemu zilizowahi kuitwa Masedonia zamani. Sehemu kubwa ya eneo ilikuwa chini ya milki ya Wabulgaria, halafu, tangu 1018 sehemu ya jimbo la Bulgaria katika Milki ya Bizanti.
Mnamo 1392 Waturuki Waosmani walianza kuvamia Masedonia iliyoendelea kukaa chini ya Milki ya Osmani hadi mwaka 1912.
Masedonia ya sasa
haririSehemu kubwa ya Masedonia ya Kale leo hii iko ndani ya Ugiriki na pia Bulgaria. Leo hii wakazi wengi wa Masedonia ya kihistoria nje ya Ugiriki wanatumia lugha za Kislavoni wakati ndani ya Masedonia ya Kigiriki wanatumia lugha ya Kigiriki.
Jamhuri ya leo ina tabia ya pekee kwa sababu ilikuwa jimbo la kujitawala la Yugoslavia hadi 1991. Wanaolikalia ni hasa Waslavi wanaozungumzwa lugha iliyo karibu na Kibulgaria na pia Kiserbia. Si rahisi kujua watu wa sehemu hizi walianza lini kujisikia watu wa pekee na tofauti na majirani yaom hasa Wabulgaria. Inaonekana hii ilitokea hasa wakati wa karne ya 20. Kwa vyovyote, baada ya mwisho wa shirikisho la Yugoslavia, Masedonia nayo ilitafuta uhuru wake.
Mwanzoni palikuwa na matatizo kuhusu jina, kwa sababu ya upinzani wa Bulgaria na Ugiriki zinazodai kuwa "Masedonia" ni sehemu ya urithi wao wa kitaifa. Hivyo, kwa muda nchi ilijulikana rasmi kama "Masedonia iliyokuwa jamhuri ya Yugoslavia" lakini yenyewe iliamua kujiita "Jamhuri ya Masedonia" tu. Hatimaye kwa makubaliano na Ugiriki ilianza kutumia jina la "Masedonia Kaskazini" mnamo Februari 2019.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Masedonia Kaskazini kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |