Sabato (kwa Kiebrania: שבת, shabbāt, yaani pumziko kwa Kiswahili) ni siku ya pumziko ya kila juma katika Uyahudi kwa ujumla na hasa katika nchi ya Israeli.

Meza ya chakula cha kuanzisha Sabato ya Kiyahudi; mlo huanza kwa kubariki divai na mkate.

Msingi wa desturi hii ni masimulizi ya Biblia jinsi Mungu alivyomaliza kuumba mbingu na nchi akaona vema kupumzika siku ya saba.

Wayahudi tangu kale walijaribu kufuata mfano huu wakipumzika siku ile ya saba. Sabato husheherekewa kila Jumamosi kuanzia saa za jioni kwenye Ijumaa hadi jioni ya Jumamosi.

Wayahudi wakifuata dini huanza kwa sala ya jioni kwenye sinagogi halafu kwa chakula cha pekee.

Msingi wa Sabato katika Biblia

Msingi wa utaratibu wa sabato katika Biblia uko katika kitabu cha Kutoka sura ya 20:8-11 zinapoorodheshwa Amri Kumi alizopewa Musa juu ya Mlima Sinai:

Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya mlango yako. Maana kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya sabato akaitakasa.

Amri hii ilichukuliwa kama amri ya kutofanya kazi bali kupumzika.

Tabia ya pekee ya amri hii ni sharti la kuwapa hata wafanyakazi na watumwa nafasi hii ya kupumzika, hasa inavyotajwa katika Kumbukumbu la Torati 5:12-15 ambamo sababu si uumbaji bali ukombozi ambao Mungu kwa njia ya Musa aliwatoa Waisraeli utumwani Misri. Hivyo amri hii inatazamwa kama sheria ya kwanza ya kutunza haki za wafanyakazi.

Kadiri ya Kutoka 31:13-17 adhimisho la Sabato lilitolewa na Mungu kwa Waisraeli kama ishara ya agano la kudumu kati yake na wao.

Mapokeo ya Talmudi

Tangu kale wataalamu Wayahudi walijadili swali hili: je kazi ipi iko chini ya masharti ya amri ya Sabato. Majadiliano haya yanaonekana katika maandiko ya Agano Jipya, kwa mfano pale ambapo Yesu aligongana na Mafarisayo kuhusu suala la uponyaji siku ya Sabato (Mk 3 na penginepo).

Wataalamu Wayahudi waliendelea kujadiliana hadi kuorodhesha katika Talmudi aina 39 za shughuli ambazo ni marufuku siku ya Sabato. Kwa mfano ni marufuku kuwasha moto, kuandika, kutekeleza kazi yoyote kwa chombo, kununua au kuuza kitu, kugusa hela.

Wayahudi Waorthodoksi hutunza masharti hayo hadi leo. Wataalamu wameendelea kuangalia mapokeo ya Talmudi katika mazingira ya kisasa. Sharti ya kutowasha moto imeendelezwa kwa kutowasha taa hata za umeme ikaendelezwa hata kutobonyeza swichi yoyote siku ya Sabato. Lakini inaruhusiwa kutumia mitambo inayofuata saa au programu na kuwasha taa au mashine bila mtu kugusa. Vilevile hawaendeshi gari kwa sababu kuwasha injini ni sawa na kuwasha moto.

Wayahudi huria hawachukui amri hizi vikali vile. Kwa mfano Myahudi huria asingeandika chochote kinachohusika na kazi yake lakini hana shida kuandika barua isiyo ya kikazi. Atajaribu kuepukana na tendo la kununua kitu dukani lakini kama kuna haja atafanya hivyo.

Wayahudi wote wafundisha ya kwamba sheria zote za Sabato zaweza kuvunjwa kama uhai wa binadamu uko hatarini.

Wakristo na Sabato

Katika Ukristo Sabato imehamishwa kwenda siku ya Jumapili isipokuwa kati ya madhehebu madogo kama Waadventista Wasabato.

Chanzo cha badiliko hilo kinaonekana katika taarifa ya Matendo ya Mitume 20:7 inayoonyesha ya kwamba wakati wa Mtume Paulo Wakristo walikutana siku ya kwanza ya juma. Sababu yake ilikuwa kukumbuka ufufuko wa Yesu aliyetoka kaburini siku hii ya kwanza yaani Jumapili.

Agano Jipya halielezi badiliko hili lilitokeaje, lakini linahusianishwa na matukio mawili ya Kanisa katika karne ya 1: polepole Wakristo wa mataifa waliwapita wale wa Kiyahudi kwa idadi na bidii, nao hawakujali tena mambo mbalimbali ya Agano la Kale; amani kati ya Wakristo na Wayahudi ilizidi kupungua, na baada ya maangamizi ya Hekalu la Yerusalemu (70 BK) hao wa mwisho waliwakataza hao wa kwanza wasiendelee kushiriki ibada zao sinagogini.

Barua kwa Wakolosai 2:16 inawahimiza Wakristo hao wasijisikie kubanwa na masharti ya Kiyahudi wala kusumbuliwa na mtu kuhusu Sabato na siku nyingine za kalenda ya Kiyahudi.

Sababu ya kiteolojia inayotajwa tangu mwanzo wa karne ya 2 (baada ya kipindi cha Biblia kutungwa) ni kwamba ufufuko wa Yesu ilikuwa mwanzo wa uumbaji mpya na hivyo katika kipindi cha Agano Jipya ile sikukuu ya agano la kwanza haisimami tena. Kwa sababu hiyo Dominika kama Siku ya Bwana inaitwa siku ya nane, ambapo kwa kumfufua Yesu, Mungu alianza juma jipya la uumbaji mtukufu zaidi.

Kwa muda mrefu Jumapili iliheshimiwa kama siku ya ibada ya Kikristo lakini bila masharti ya kuacha kazi. Sharti hili lilikaziwa tu katika nchi za Ulaya hasa tangu karne ya 18 na 19.

Siku za juma (wiki)
Jumapili - Jumatatu - Jumanne - Jumatano - Alhamisi - Ijumaa - Jumamosi