Karantini (kwa Kiingereza: quarantine) ni uzuiaji wa watu au wanyama wasitolewe kutoka eneo moja hadi jingine ili kuzuia uenezaji wa magonjwa ya kuambukiza (infectious diseases). [1]

Mgonjwa wa ebola kwenye chumba cha karantini, Kinshasa mwaka 1979

Ufafanuzi wa karantini hariri

Mara nyingi karantini inamaanisha kuzuia miendo ya watu ambao wanaweza kuathiriwa na ugonjwa wa kuambukiza ilhali ugonjwa kwao haukuweza kuthibitishwa bado. Istilahi ya karantini hutumiwa pia kama mgonjwa anazuiliwa kukutana na watu wengine ili kuzuia uenezaji wa ugonjwa hatari.[2]

Karantini inaweza kutumika kwa wanadamu, lakini pia kwa wanyama wa aina mbalimbali, na wote kama sehemu ya udhibiti wa mpakani na ndani ya nchi.

Asili ya jina hariri

 
Bendera hii ilipaswa kuonyeshwa na meli kama ishara ya karantini

Asili ya neno karantini iko katika lahaja ya Venisi, ni kifupi kwa Kiitalia "quaranta giorni" yaani "siku arobaini". Wakati wa epidemiki ya tauni katika Ulaya ya karne za kati, mabaharia na abiria kutoka meli walipaswa kusubiri siku 30 kwenye kisiwa kidogo nje ya mji kabla hawajaruhusiwa kuingia mjini penyewe. Kama mtu kwenye meli angekuwa na viini vya tauni, ugonjwa ungeanza katika kipindi hicho na kuonekana kwake tu bila kuambukiza watu kwenye nchi kavu. [3]

Kisheria hariri

Kuweka watu karantini huathiri mara nyingi haki za raia, haswa kama watu hulazimishwa muda mrefu kukaa mahali fulani wakizuiliwa kukutana na wengine, hata na familia zao. Hivyo nchi nyingi huwa na sheria zinazounda utaratibu na mamlaka kuhusu hatua za karantini.

Historia hariri

 
Kijiji nchini Romania katika karantini, kilicholindwa na askari baada ya kutokea kwa kipindupindu.

Kati ya taarifa za kwanza kuhusu karantini ni maelezo katika Biblia, Kitabu cha Walawi 13,2: Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king'aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa ... makuhani mmojawapo; 3 na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili;… na kusema kuwa yu mwenye unajisi. 4. … ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo; 5 kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena [4]

Zamani ambapo usafiri wa mbali ulifanywa kwa meli, ilikuwa kawaida kuzuia abiria na mabaharia kufika mji wa bandari kama watu kwenye meli walikuwa na dalili za ugonjwa; mfano ni kisiwa cha Changu, karibu na mjini Zanzibar. Kama abiria kutoka meli yenye wagonjwa au aliyeonyesha ya ugonjwa fulani alitaka kuingia mjini, alitakiwa kusubiri kwenye kisiwa kidogo kwa muda wa kutosha hadi ilipokuwa dhahiri yeye si mgonjwa, hawezi kuwaambukiza wengine.

Mifano ya kisasa hariri

Epidemiki ya Ebola katika Afrika ya Magharibi ilimalizika mnamo 2016 kwa kuweka wagonjwa wengi iwezekanavyo kwenye karantini, yaani kuwazuia katika vituo maalumu au nyumbani kwao ili wasipate kukutana na ndugu au watu wengine.

Jamhuri ya Watu wa Uchina ilitangaza karantini juu ya jiji la Wuhan lenye wakazi milioni 9 na halafu wote wa mkoa wa Hubei (idadi ya watu milioni 55.5) baada ya kuenea kwa virusi vya corona katika Januari 2020.

Marejeo hariri

  1. "quarantine" noun Merriam Webster definition www.merriam-webster.com, accessed 27 January 2020
  2. "History of Quarantine" Centers for Disease Control and Prevention
  3. Ronald Eccles; Olaf Weber, eds. (2009). Common cold (Online-Ausg. ed.). Basel: Birkhäuser. pp. 210. ISBN 978-3-7643-9894-1. 
  4. Mambo ya Walawi 13

Viungo vya Nje hariri

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
 
Simple English Wiktionary
Wikamusi ya Kiswahili ina maelezo na tafsiri ya maana ya neno:
  Makala hii kuhusu mambo ya tiba bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Karantini kama sababu yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.