Kuhusu lugha ya Kimbunga tazama Kimbunga (lugha)

Kimbunga (kwa Kiingereza: tropical cyclone, hurricane, typhoon) ni dhoruba kali inayoanza juu ya bahari katika maeneo ya tropiki yenye upepo wenye kasi ya zaidi ya km/saa 117. Kimbunga ni dhoruba aina ya tufani yaani kina mwendo wa kuzunguka.

Kimbunga ya "Katrina" juu ya Ghuba ya Meksiko - picha kutoka chombo cha angani tar. 28 Agosti 2005
Picha ya rada ya kimbunga upande wa kaskazini ya ikweta inaonyesha mwendo wake
Kimbunga Idai mnamo 15-03-2019, wakati wa kufika kwenye mwambao wa Msumbiji (ziwa inayoonekana katikati juu ni Ziwa NYassa)

Tabia za vimbunga

hariri

Vimbunga huwa na eneo la shinikizo duni kwenye kitovu chake (low-pressure center). Upepo mkali unazunguka haraka kitovu hiki karibu na uso wa bahari au uso wa nchi (closed low-level atmospheric circulation, strong winds). Mvua za radi zinazunguka kitovu pamoja na mwendo wa kimbunga chote na kuleta mvua nzito (spiral arrangement of thunderstorms that produce heavy rain)[1].

Huanza juu ya bahari ya kitropiki kwenye maji yenye halijoto juu ya 26°C. Hewa joto yenye mvuke nyingi inaanza kupanda juu na kuzunguka. Mzunguko huo unaongezeka kasi kuwa dhoruba. Kasi ikifikia mwendo wa 117 km/saa inaitwa kimbunga.

Vimbunga vinatokea katika bahari zote zenye maji ya moto kaskazini na kusini kwa ikweta. Mzunguko hufuata mwendo wa saa kama kimbunga kinatokea kusini kwa ikweta; ni kinyume cha mwendo wa saa kama kinatokea kaskazini kwa ikweta.

Hatari za kimbunga

hariri

Kimbunga kinaweza kusababisha hasara kubwa kikikubana na meli baharini na zaidi mwambaoni kinapofikia nchi kavu au visiwa. Nguvu ya upepo husukuma maji mengi ya bahari inayoweza kufikia mita kadhaa juu ya uwiano wa kawaida wakati wa kufika mwambaoni. Wimbi kubwa linaleta mafuriko wa ghafla yanayoweza kuvunja nyumba na kupeleka maji ya bahari mita mia kadhaa barani; penye mdomo wa mto wimbi la bahari linaendelea kuenea kwa kufuata njia ya mto.

Hatari zinazofuata ni hasa kasi ya upepo pamoja na kiasi kikubwa cha mvua.[2][3] Kasi ya upepo inaweza kuinua vitu vizito kama miti, mapaa ya nyumba[4] au magari na kuvirusha mbali. Watu huuawa na mali kuharibiwa. Wingi wa mvua husababisha mafuriko yanayofuata njia ya kimbunga juu ya nchi kavu, wakati mwingine kwa kilomita mia kadhaa kutoka mwambao[5].

Huko Amerika ni hasa visiwa vya Karibi na nchi jirani za Ghuba ya Meksiko pamoja na kusini mwa Marekani zinazoathiriwa kila mwaka.

Barani Afrika ndiyo Msumbiji pamoja na nchi jirani iliyoona mara kwa mara uharibifu kutokana na dhoruba. Mwaka 2019 kimbunga kilichoitwa Idai[6] kiliharibu mji mkubwa wa Beira na kusababisha vifo hadi Zimbabwe na Malawi[7]. Kimbunga hiki kilifuatwa na kimbunga kilichoitwa "Kenneth" kilichosababisha maafa kwenye visiwa vya Komori na kufika barani kaskazini mwa Msumbiji karibu na mji wa Pemba na kuathiri pia maeneo ya kusini mwa Tanzania[8].

Majina ya Vimbunga

hariri

Kila sehemu ya dunia kimbunga kina jina lake na majina haya yameanza kutumiwa kimataifa:

Vimbunga hutokea mara kwa mara katika majira ya joto. Wataalamu wameanza kuvipa majina kwa kurahisisha maelewano. Katika eneo la kila bahari kuna utaratibu wa pekee wa kutolea majina kwa vimbunga kufuatana na mapatano ya wanasayansi.

Atlantiki inaona takriban vimbunga kumi au zaidi kila mwaka. Hupewa majina kufuatana na alfabeti. Imekuwa kawaida tangu mwaka 1979 kutumia majina ya kiume na ya kike kwa kupokezana (zamani vilipewa majina ya kike tu, lakini wanawake walilalamika).

Wataalamu wanatumia orodha sita ya majina hivyo jina linaweza kurudia baada ya miaka sita.

Kimbunga ya "Katrina" kilichoharibu mji wa New Orleans nchini Marekani katika Agosti 2005 kilikuwa kimbunga cha 11 cha mwaka 2005. Kilifuata kimbunga "Jose" na kufuatwa na "Lee" halafu "Maria". Kama kimbunga kinasababisha uharibifu mkubwa sana jina lake huondolewa katika orodha maana yake jina hili halitarudia. "Katrina" imebadilishwa kuwa "Katia" katika orodha ya mwaka itakayotumika mwaka 2011 (ikitokea itakuwa kimbunga kinachofuata "Jose" ya 2011).

Marejeo

hariri
  1. Ciclones Tropicales (pdf), kijitabu cha Idara ya Meteorolojia ya Kitaifa, Marekani, iliangaliwa Machi 2019
  2. UCAR Center for Science Education. "Hurricane Impacts". University Corporation for Atmospheric Research - UCAR- Center for Science Education website. Iliwekwa mnamo 2019-06-05.
  3. Sonia Madaan (2017-09-27). "Causes and Effects of Hurricanes". Earth Eclipse (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2019-06-05.
  4. Prime Roofing (2018-11-19). "Hurricane Coming? A Guide on How to Protect Your Roof". Prime Roofing (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2019-06-05.
  5. Hurricane Safety Tips and Resources, tovuti ya Idara ya Meteorolojia ya Kitaifa, Marekani, iliangaliwa Machi 2019
  6. Kimbunga Idai: Msumbiji katika hatari kimbunga kingine kikali kikitua, tovuti ya BBC-Kiswahili tar 15-ß3-2ß19
  7. Kimbunga Idai: Serikali ya Tanzania imetoa msaada kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, tovuti ya BBC Kiswahili, 19-03-2019
  8. Taarifa kwa umma kuhusu Kimbunga Kenneth Archived 19 Agosti 2019 at the Wayback Machine., tovuti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, iliangaliwa 25-Aprili-2019
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kimbunga kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.