Kupaa Bwana ni ukumbusho wa fumbo la Yesu Kristo kupaa katika utukufu wa mbinguni akiwa na mwili wake mzima ambao Ijumaa kuu ulisulubiwa hata akafa akazikwa kabla hajafufuka siku ya tatu (Jumapili) kadiri ya imani ya Ukristo.

Kupaa Kristo kadiri ya Garofalo, 1520.
Liturujia ya Kupaa Bwana katika Kanisa la Kiorthodoksi la Kisiria huko Mumbai, India.
Kupaa Kristo kadiri ya Gebhard Fugel, 1893 hivi.
Mwaka wa liturujia
Magharibi
Mashariki

Mafundisho ya imani hariri

Ni kwamba imani hiyo inafundisha kuwa siku arubaini baada ya kufufuka, Yesu alipaa mbinguni mbele ya wanafunzi wake. Hataonekana tena rasmi mpaka arudi siku ya mwisho. “Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni” (Mdo 1:11). “Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Kol 3:1).

Wakristo wanahusika na kupaa kwake, kwa sababu yeye ni kichwa chao, nao ni viungo vya mwili wake: hivyo amewatangulia kwa Baba awaombee Roho Mtakatifu wakafike kwake. Mwenyewe ameahidi, “Mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo” (Yoh 14:3). “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea” (Rom 8:33-34). “Yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee” (Eb 7:24-25).

Hivyo, utawala wa Yesu umeshaanza, nao utakamilika atakaporudi kuwahukumu wazima na wafu kwa kutenganisha moja kwa moja wema na wabaya. “Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti” (1Kor 15:25-26). Hapo katikati “watafanya vita na Mwanakondoo, na Mwanakondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme” (Ufu 17:14).

Utawala wa Yesu umeanza hasa katika Kanisa lake linalokusanya wale waliomuamini kuwa ni Bwana wakaokolewa. Mungu “alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake” (Kol 1:13). Yesu alisema, “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu… Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu” (Yoh 18:36,37). “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza” (Lk 17:20). “Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia” (Math 13:33). Baada ya kufufuka, aliwajibu Mitume waliomuuliza kuhusu wakati wa kurudisha ufalme: “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Mdo 1:7-8).

Asili na uenezi wa sherehe hariri

Adhimisho hilo katika liturujia ni la zamani sana. Ingawa hakuna uthibitisho wa kimaandishi kabla ya mwanzo wa karne ya 5, Agostino wa Hippo alisema linatokana na Mababu wa Kanisa wa kwanza, na kwamba linafanyika katika Kanisa lote tangu muda mrefu.

Kweli linatajwa mara nyingi katika maandishi ya Yohane Krisostomo, Gregori wa Nisa, katika Katiba za Mitume na mengineyo ya Makanisa ya Mashariki na Kanisa la magharibi.

Sherehe hiyo inaunganisha madhehebu mengi sana katika kumshangilia Yesu kufanywa Bwana wa wote na vyote.

Kwa kawaida sikukuu hiyo ilikuwa inafanyika siku arubaini baada ya Jumapili ya Pasaka kufuatana na hesabu ya Matendo ya Mitume 1:3, lakini siku hizi mara nyingi inasogezwa kutoka Alhamisi hadi Jumapili inayofuata ili kuwawezesha waamini wote kushiriki pale ambapo siku yenyewe ni ya kazi, si sikukuu ya taifa.

Sherehe hiyo iligusa wasanii wengi kutoa michoro, nyimbo[1] n.k.

Tanbihi hariri

  1. The feast has been associated with specific hymns and other church music. The oldest hymn in German related to the feast is the Leise "Christ fuhr gen Himmel", first published in 1480. Johann Sebastian Bach composed several cantatas and the Ascension Oratorio to be performed in church services on the feast day. He first performed Wer da gläubet und getauft wird, BWV 37, on 18 May 1724, Auf Christi Himmelfahrt allein, BWV 128, on 10 May 1725, Gott fähret auf mit Jauchzen, BWV 43, on 30 May 1726 and the oratorio, Lobet Gott in seinen Reichen, BWV 11, on 19 May 1735.

Viungo vya nje hariri

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kupaa Bwana kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.