Lumen Gentium
Lumen Gentium (katika Kilatini maana yake ni "Mwanga wa Mataifa") ni jina fupi la hati ya kidogma ya Mtaguso wa pili wa Vatikano inayohusu fumbo la Kanisa katika imani ya Kikatoliki.
"Lumen Gentium" ni maneno mawili ya kwanza ya hati hiyo iliyotolewa kwa lugha ya Kilatini.
Maaskofu na mapadri 2151 kati ya waliohudhuria mtaguso huo walikubali hati hiyo wakati 5 tu waliipinga, halafu Papa Paulo VI aliitangaza kwa Kanisa Katoliki tarehe 21 Novemba 1964.
Hutazamwa kuwa hati muhimu kuliko zote za mtaguso huo, ikijumlisha mafundisho ya kikatoliki ya miaka 2,000.
Mkazo wa hati hiyo ni mafundisho juu ya kanisa kuwa fumbo la "mwili wa Kristo" duniani na pia kuwa "taifa la Mungu safarini".
Inakazia tabia ya kiroho ya Kanisa kuliko umbo lake kama taasisi yenye mfumo wa kiutawala.
Kwa maneno ya Papa Paulo VI imejibu swali: “Kanisa, unasemaje juu yako?”.
Sura ya kwanza
haririSura ya kwanza inafafanua fumbo la Kanisa ambalo, kama sakramenti, lina mawili yasiyotenganika: kwa nje linaonekana kwa namna fulani, na kwa ndani mna neema isiyoonekana inayoletwa na yale yanayoonekana. Basi, ndani ya Kanisa la watu Mungu anaishi na kufanya kazi.
Kwa hiyo hati inaanza kwa kueleza jinsi Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanavyohusika na Kanisa.
Halafu unaonyesha kuwa Kanisa ni mwanzo wa ufalme wa Mungu, nalo linafananishwa na kundi la kondoo, shamba, jengo na hekalu la Mungu au bibiarusi anayeungana na Bwanaarusi wake kuwa mwili mmoja, yaani mwili wa Kristo: ndio ukweli wenyewe wa Kanisa.
Sura ya pili
haririBaada ya kuona ukweli huo wa ndani, sura ya pili inaelekea kutazama watu wanavyohusika na fumbo la Kanisa.
Kuanzia Agano la Kale Mungu hakupenda kuokoa watu mmojammoja bali aliwaunganisha wawe taifa lake lenye kujua ukweli na kumtumikia kitakatifu.
Katika taifa hilo wote wamejaliwa ukuhani unaotumika katika adhimisho la sakramenti, na unabii wenye karama mbalimbali.
Katika taifa hilo watu wote wanapaswa kuingia bila ya ubaguzi ili wawe kitu kimoja.
Ndiyo maana ya jina “Katoliki”: la mahali pote na nyakati zote.
Watu wote wanahusiana na Kanisa, ila kwa namna mbalimbali.
Kwanza wapo Wakatoliki, yaani waliojiunga nalo kikamilifu kwa kumkubali Roho Mtakatifu na miundo yote ya Kanisa.
Halafu wapo Wakristo wa madhehebu mengine waliokwishabatizwa na hivyo wameungana nalo ingawa si kikamilifu, kwa sababu hawakubali baadhi ya mafundisho na miundo yake.
Hatimaye wapo watu wengine pia, wenye dini mbalimbali au wasio na dini, ambao wote wanaitwa na Mungu wajiunge na Kanisa kwa kuwa linahitajika kwa wokovu, ingawa Mungu anaweza kuwaokoa wenye nia njema wasiopata habari njema.
Bila ya shaka kwa mtazamo wa mtaguso hali ya Wakatoliki ni bora zaidi, lakini hao wanapaswa kuwajibika zaidi na kuwashirikisha wengine wote ili kuwaokoa kutoka udanganyifu wa shetani na ulimwengu.
Ndiyo maana ya kazi ya kimisionari ambayo imeagizwa na Yesu na ni wajibu wa kila Mkristo.
Sura ya tatu
haririSura ya tatu inatoa mafundisho muhimu, tena mapya, kuhusu muundo wa uongozi wa Kanisa, hasa uaskofu.
Ni kwamba mtaguso wa kwanza wa Vatikano (1869-1870) ulifundisha sana kuhusu papa lakini haukupata nafasi ya kutoa hati juu ya maaskofu iliyopangwa itafuata: hiyo ni kwa sababu mtaguso ulisambaratika jeshi la Italia lilipoteka Roma tarehe 20 Septemba 1870.
Hivyo mtaguso wa pili wa Vatikano ulikusudia kukamilisha kazi hiyo.
Hasa umefundisha kwamba kama vile mitume walivyokuwa kundi moja na Petro na chini yake, maaskofu wote ni kundi moja na papa wa Roma na chini yake.
Kwa mpango wa Mungu kundi hilo ni la kudumu, maaskofu wakiwa waandamizi halisi wa mitume, na papa mwandamizi halisi wa Petro, mkuu wao.
Kwa namna ya pekee mtaguso umefundisha kuwa ibada ya kumweka wakfu askofu ni ngazi ya juu kabisa ya sakramenti ya daraja inayompa uwezo mpya, si baraka fulani tu ambayo padri anapewa afanye kazi ya juu (kama wengine walivyodhani awali).
Hivyo uaskofu unatia alama isiyofutika milele.
Kutokana na fundisho hilo, mtaguso umesisitiza kila mara umuhimu wa maaskofu katika maisha yote ya Kanisa.
Lakini mtaguso umesisitiza pia umoja wa maaskofu, ukidai kila mmojawao afanye kazi yake akishirikiana na kundi lote na achangie ustawi wa Kanisa zima, si jimbo lake tu.
Katika hilo askofu ndiye nguzo ya umoja wa waamini wake wao kwa wao tena kati yao na waamini wote duniani: hivyo linafanya jumuia ya kijimbo istahili kuitwa Kanisa, kwa kuwa ndani yake Kanisa lote limo kweli.
Kwa msingi huo askofu anawakilisha Kanisa lake maalumu katika Kanisa Katoliki, na kulifundisha, kulitakasa na kuliongoza kwa msaada wa mapadri wake na wa mashemasi, ambao wote wanashiriki ukuhani wake mkuu.
Mwishoni mwa sura hiyo Kanisa la Magharibi linaruhusu urudishwe ushemasi wa kudumu ambao uweze kutolewa kwa wanaume wenye ndoa pia.
Sura ya nne
haririMara baada ya sura inayohusu wale wachache waliopata daraja takatifu (wanaoitwa makleri), inafuata sura juu ya Wakristo wa kawaida (wanaoitwa walei).
Kwa karne nyingi hao walibaki kama wasikilizaji na watazamaji tu katika ibada na katika maisha yote ya Kanisa, lakini kuanzia karne XIX utume wao ulianza kuamka upya.
Mtaguso umesisitiza kwa nguvu wajibu na haki yao ya kutumia neema na vipaji walivyojaliwa na Mungu kwa ujenzi wa taifa lake na kwa wokovu wa ulimwengu.
Msingi wake ni ubatizo uliowafanya manabii, makuhani na wafalme; hivyo wamejaliwa huduma na karama mbalimbali ambazo wachungaji wanapaswa kuziheshimu wakiwaachia uhuru na nafasi katika utendaji.
Kwa namna ya pekee ni juu yao kulenga utawala wa Mungu kwa kushughulikia malimwengu.
Sura ya tano
haririBaada ya kuona hayo makundi mawili ya waamini, wanaotofautiana kwa alama walizotiwa rohoni na ubatizo na kipaimara tu, au na daraja takatifu pia, sura ya tano inahusu wito unaowaunganisha wote, yaani kupata utakatifu.
Karne za nyuma wengi walidhani hiyo ni kazi ya watawa tu, waliojichagulia “hali ya ukamilifu”, au sanasana mapadri, kutokana na ukuu wa huduma zao.
Kumbe sivyo: Wakristo wote wanapaswa kulenga utakatifu, kila mmoja kadiri ya wito wake maalumu na hali yake maishani.
Hati inaorodhesha aina mbalimbali za waamini na jinsi kila moja ilivyo na njia yake; halafu inakumbusha njia mbili bora za kufikia utakatifu, yaani kifodini na mashauri ya Kiinjili: kwa maisha na kifo chao wafiadini na watawa wanahimiza Wakristo wote kutafuta ukamilifu wa upendo.
Sura ya sita
haririKufuatana na yaliyotangulia, ni rahisi kuelewa kwa nini sura hii inazungumzia watawa.
Hao hawahusiki na uongozi wa Kanisa (isipokuwa kama wamepata pia daraja takatifu), ila wanahusika moja kwa moja na utakatifu na uhai wake.
Si kundi la tatu kati ya makleri na walei, bali ni walei au makleri waliojifunga kulenga utakatifu kwa kushika mashauri ya Kiinjili, yaani useja mtakatifu, ufukara na utiifu.
Mtaguso umesisitiza umuhimu wa mtindo huo wa maisha, na kwamba asili yake ni katika maneno na mifano ya Yesu Kristo: utawa hautokani na historia ya Kanisa tu, bali upo na ni lazima uwepo kwa mpango wa Mungu.
Hivyo uongozi wa Kanisa unapaswa kuuratibu na kuudumisha katika mitindo yake mingi.
Mtawa amewekwa wakfu kwa ubatizo, halafu anaimarisha hali hiyo kwa nadhiri ili achume kwa wingi zaidi matunda ya neema akiondoa mapingamizi yoyote yanayoweza kumzuia maishani.
Sura ya saba
haririBaada ya kuwaongelea watawa, wanaoshuhudia kwa namna ya pekee ulimwengu mpya ambapo hapana ndoa, sura ya saba inakuja kufundisha kuwa Kanisa lote hapa duniani liko safarini kuelekea mbinguni, huku likiwa na umoja na watakatifu.
Sura hiyo inasisitiza tena imani ya Kikatoliki kuhusu mambo ya mwisho ikiwahimiza waamini watazame juu na kuzingatia mifano bora ya wale waliokwishafikia heri ya milele.
Hao wanastahili kuheshimiwa na kuombwa waombee wenzao wa duniani, mradi yaepwe makosa mbalimbali yaliyowahi kujitokeza huku na huku.
Daima ionekane wazi kuwa Wakristo wanamuabudu Mungu tu na kwamba wakiheshimu watakatifu ni kwa sababu ni marafiki wa Mungu na wafuasi hodari wa Mwanae.
Waheshimiwe sio tu ili kupata msaada fulani, bali hasa kwa kufuata mifano yao ili kuwafikia katika liturujia ya mbinguni na kuwaabudu Mungu na Mwanakondoo.
Sura ya nane
haririMwishoni mwa hati hii yanapatikana mafundisho kuhusu Bikira Maria, akiwa ni mkuu wa watakatifu na mfano wa Kanisa lote.
Baada ya mabishano makali kati ya washiriki wa mtaguso, wingi wa kura ulikataa kutoa hati maalumu juu ya Maria peke yake, kwa kuwa hawezi kueleweka nje ya fumbo la Kristo na la Kanisa.
Hivyo mafundisho hayo yamepangwa katika sura ya nane ya hati hii.
Hayana nia ya kuamua mabishano kati ya wanateolojia, wala ya kufundisha mapya, bali kupanga upya mafundisho ya Maandiko matakatifu na ya Mapokeo.
Baada ya kumsifu sana bikira huyo, mtaguso umesisitiza juu yake pia kuwa Kristo ndiye mshenga pekee kati ya Mungu na watu, hivyo haiwezekani kumlinganisha Maria na yeye kama walivyowahi kufanya baadhi ya waamini.
Mchango wake kwa ukombozi wetu ulitokana na ukombozi ulioletwa na Yesu, tena ni kushiriki kazi yake tu.
Hivyo Maria azidi kuigwa na kuheshimiwa kwa namna ya pekee, hasa kwa njia ya liturujia, lakini kwa kukwepa neno lolote ambalo linapita kiasi au kumweka pembeni Kristo.
Wazo kuu la hati hii kuhusu Kanisa ni kwamba lenyewe hasa ni ushirika wa Mungu nafsi tatu na watu, ni ushirika wa watakatifu wa duniani, toharani na mbinguni, ni ushirika wa waamini wa aina mbalimbali, kama vile wenye daraja na walei, au watawa na wenzao wote.
Ushirika huo unatakiwa kuonekana wazi katika maisha ya Kanisa katika ngazi zote; hivyo litaonekana lilivyo kweli, yaani ishara na chombo cha kuwaunganisha watu wote katika umoja wa Utatu mtakatifu.