Novatiano
Novatiano (kwa Kilat. Novatianus, mnamo 200–258) alikuwa mtaalamu Mkristo na kasisi aliyepinga uchaguzi wa Kornelio kuwa askofu wa Roma akijitangaza Papa na kuanzisha farakano la Unovatio katika Kanisa.
Alifahamika kama mwanatheolojia na mwandishi mashuhuri, akiwa wa kwanza mjini Roma kutumia lugha ya Kilatini kwa kueleza imani ya Kikristo[1]. Kitabu chake kuhusu Utatu kilitazamwa kuwa andiko bora la wakati wake kwa Kilatini[2]. Wakati wa dhuluma ya Decius na baada ya kifo cha Papa Fabiano alikuwa kati ya viongozi wa Kanisa la Roma akiandika barua mbili kwa niaba ya Kanisa lote[3].
Mateso chini ya Kaizari Decius yalisababishwa na amri yake kwamba kila raia atoe sadaka mbele ya sanamu za miungu na asiyetii anapaswa kufa; Wakristo wachache walikataa wakafungwa ndani na wengine kuuawa; idadi kubwa ya Wakristo waliitikia amri ya serikali, wengine walijificha, wakakimbia au walihonga maafisa waliowapa hati ya kuthibitisha sadaka hata kama hawakutoa. Novatiano aliwaona hao wote kama wasaliti na wenye dhambi nzito ambayo haiwezi kusamehewa na binadamu. Aliendelea kuwa msemaji wa kundi la "wakali" katika Kanisa waliokataa kuwatambua kama Wakristo tena, wakiona ingemaanisha kudharau sadaka ya uhai wa mashahidi wa imani waliojitolea hadi kufa. Novatiano alifundisha kwamba Mungu anaweza kuwasamehe lakini Kanisa halina mamlaka kuchukua hatua hiyo, akikumbusha maneno katika Waraka kwa Waebrania 4:4-6. "Wapole" katika Kanisa waliona kwamba wakosaji wanaweza kusamehewa na kurudishwa katika jumuiya ya Kanisa; maaskofu kama Sipriani wa Karthago pamoja na makasisi wengi huko Roma walitafuta njia ya kati inayoruhusu kuwarudisha baada ya kipindi cha toba ya hadharani.
Baada ya kifo cha Kaizari Decius mwaka 251 madhulumu yalikwisha na Kanisa la Roma liliweza kumchagua askofu mpya. Katika uchaguzi huo Kornelio alipata kura nyingi akisimama upande wa njia ya kati, msimamo ambao Novatiano aliukataa.
Siku chache baada ya uchaguzi wa Kornelio, Novatiano alikutana na maaskofu watatu kutoka Italia Kusini waliokubaliana naye ambao walimweka wakfu kuwa askofu ingawa alikuwa hajapata kipaimara [4].
Maaskofu wote wawili (Kornelio na yeye) walituma barua kwa makanisa mengine na kujitambulisha. Karibu maaskofu wote wengine, wakiongozwa na askofu Sipriani wa Karthago, walikubaliana na Kornelio.
Novatiano aliendelea kuweka wakfu makasisi na maaskofu kwa ajili ya miji mingine na kwa njia hiyo alianzisha kanisa badala lililodumu kwa karne kadhaa. Wafuasi wake waliitwa Wanovatiano, mafundisho yao yalifahamika kama Unovatiano.
Tanbihi
hariri- ↑ Origins to Constantine, ed. by Frances M. Young, Margaret M. Mitchell ; assistant editor K. Scott Bowie. (The Cambridge history of Christianity; v. 1) ISBN 0 521-81239-9, uk 471 f
- ↑ James L. Papandrea: Novatian of Rome and the Culmination of Pre-Nicene Orthodoxy, Wipf and Stock Publishers, 2011, ISBN 1606087800, 9781606087800, uk 73f, online hapa
- ↑ Novatian, Encyclopedia Britannica, iliangaliwa Oktoba 2022
- ↑ Origins to Constantine, uk 475 f
Viungo vya Nje
hariri- "Novatianus". Encyclopædia Britannica. 19 (11th ed.). 1911. p. 832.
- Novatian, de Trinitate in Latin
- Novatian, On the Trinity in English
- Novatian, On Jewish meats in English
- Multilanguage Opera Omnia
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |