Nzi-nyuki
Bombomyia discoidea nchini Afrika Kusini
Bombomyia discoidea nchini Afrika Kusini
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Diptera (Wadudu wenye mabawa mawili tu)
Nusuoda: Brachycera (Diptera wenye vipapasio vifupi)
Familia ya juu: Asiloidea
Familia: Bombyliidae
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Nusufamilia 16:

Nzi-nyuki (kutoka kwa Kiing. bee flies) au weleaji-sufu (kutoka kwa Kijerumani Wollschweber) ni nzi wa familia Bombyliidae katika oda Diptera walio na nywele nyingi kama nyuki na kuweka mabawa kwa pembe ya karibu 45º wakipumzika. Spishi nyingi zina “ulimi” mrefu sana ili kufyonza mbochi katika maua. Mabuu wao ni vidusia wa lava wa wadudu wengine kwa kawaida.

Maelezo

hariri

Ukubwa wa nzi-nyuki unaanza kutoka mdogo sana (mm 1) hadi mkubwa kiasi (mm 25) na upana wa mabawa wa mm 3-40. Umbo la mwili kwa ujumla ni imara na spishi nyingi zimefunikwa kwa nywele nyingi. Wako weusi, kijivu au kahawia kabisa au rangi hizo zimeunganishwa na mistari au mabaka meupe na/au njano. Spishi nyingi huiga spishi maalum za nyuki[1][2].

Kichwa kina umbo la tufe na kuwa na uso wa mbenuko na macho makubwa ambayo mara nyingi hugusana kwa madume. Vipapasio vina pingili kuu tatu. Pingili ya tatu ni kubwa kuliko nyingine na hubeba nywele ndefu zilizofunikwa na nywele fupi (arista) au pingili fupi moja hadi tatu nyingine (stylus). Sehemu za mdomo hutoholewa kuwa neli ya kufyonza mbochi kwenye maua. Urefu wake unatofautiana sana. Kwa mfano, Anthracinae wana sehemu fupi za mdomo, ambazo labiamu yao huishia kwenye labelo kubwa nono. Walakini, katika nusufamilia nyingi neli ni ndefu zaidi na katika Bombyliinae zaidi ya mara nne ya urefu wa kichwa.

Miguu ni mirefu na myembamba na miguu ya mbele pengine ni mifupi na myembamba zaidi kuliko miguu ya kati na ya nyuma. Kwa kawaida miguu hubeba nywele ngumu kwenye ncha za tibia. Mabawa ni mangavu, mara nyingi kama kioo au yenye rangi sawa au kwa milia. Katika mkao wa kupumzika mabawa huwekwa wazi na kimlalo katika umbo la V inayoonyesha pande za fumbatio.

Fumbatio kwa ujumla ni fupi na pana yenye karibu umbo la tufe, la mcheduara au la koni na inajumuisha pingili sita hadi nane zinazoonekana. Pingili zilizobaki ni sehemu za muundo wa sehemu za nje za uzazi. Fumbatio ya majike mara nyingi huisha na michomozo kama miiba, inayotumiwa kwa kutaga mayai. Katika Anthracinae na Bombyliinae kuna nafasi wazi katika pingili ya nane, ambamo mayai huchanganywa na mchanga kabla ya kutagwa.

 
Eristalis tenax, nzi mweleaji anayefanana na nzi-nyuki.

Nzi weleaji wa familia Syrphidae mara nyingi huiga Hymenoptera pia, na baadhi ya spishi ni vigumu kutofautisha na Bombyliidae kwa mtazamo wa kwanza, hasa na nzi-nyuki wasio na neli ya mdomo ndefu au miguu mirefu na myembamba. Bombyliids kama hao bado zinaweza kutofautishwa porini kwa sifa za kianatomiki kama vile:

- Kwa kawaida huwa na uso uliopindika au unaoteremka sawasawa. Nzi weleaji mara nyingi huwa na mikunjo inayoonekana ya kutikulo ya uso na/au michomozo ya uso kama kinundu.
- Mabawa hayana "kingo za uwongo za nyuma" na mara nyingi huwa na maeneo meusi makubwa yenye mipaka mikali, au ruwaza tata za madoa. Mabawa ya nzi weleaji mara nyingi huwa wangavu au yana miinamo laini ya rangi, na vena zao huungana nyuma na kuwa "ukingo wa uwongo" badala ya kufikia ukingo wa kweli wa nyuma wa bawa.
- Fumbatio na thoraksi huwa kwa nadra na maeneo makubwa ya kung'aa yaliyoundwa na kutikulo bila nywele, ambayo nzi weleaji huwa nayo mara nyingi.

Mabuu ya nzi-nyuki wengi ni wa aina mbili. Wale wa aina ya kwanza wana umbo lililorefuka na la mcheduara na wana jozi ya spirakulo kwenye fumbatio na, labda, jozi kwenye thoraksi. Wale wa aina ya pili wamerunda na wana kichwa kilichoundwa vizuri na jozi moja ya spirakulo iliyowekwa kwenye fumbatio.

Biolojia

hariri

Wapevu hupendelea hali kavu na za jua, mara nyingi maeneo ya mchanga au mawe. Wana mabawa yenye nguvu na hupatikana kwa kawaida wakielea juu ya maua au kupumzika kwenye ardhi tupu iliyoangaziwa na jua (tazama video). Nzi-nyuki hula mbochi na chavua ambayo hukidhi mahitaji yao ya protini. Wanachangia kwa kiasi kikubwa katika uchavushaji mtambuka wa mimea na kuwa wachavushaji wakuu wa spishi fulani za mimea ya mazingira ya jangwa.

Kama vile nzi weleaji, nzi-nyuki wanaweza kuongeza au kupunguza kasi ya ghafla, mabadiliko ya kasi ya mwelekeo takriban bila momenta, udhibiti wa kiwango cha juu wa mkao wakati wa kuelea katikati ya hewa na vile vile mbinu ya tahadhari ya mahali pa kulisha au kutua. Nzi-nyuki mara nyingi hutambulika kwa umbo lao mnene, kwa tabia yao ya kuelea na kwa urefu mahususi wa sehemu zao za mdomo na/au miguu wanapoegemea mbele kwenye maua. Tofauti na nzi weleaji, ambao hutua juu ya ua kama vile nyuki na wadudu wengine wanaochavusha, spishi zile za nzi-nyuki zilizo na neli ndefu ya kulishia kwa ujumla hula zikiendelea kuelea angani, kiasi kama vile Sphingidae, au zikigusa ua kwa miguu yao ya mbele ili kutulia mkao wao bila kutua kikamilifu au kusitisha kubembea cha mabawa.

Spishi zilizo na neli fupi zaidi ya kulishia hutua na kutembea kwenye vichwa vya maua, hata hivyo, na zinaweza kuwa ngumu zaidi kutofautishwa na nzi weleaji porini. Kama ilivyobainishwa, spishi nyingi za nzi-nyuki hutumia vipindi vya muda vya kawaida wakiwa wamepumzika juu ya au karibu na ardhi, huku nzi weleaji hufanya hivyo kwa nadra. Kwa hivyo inaweza kuwa ya kuelimisha kutazama nzi wanaojilisha moja kwa moja na kuona kama wanasogea chini mpaka usawa wa ardhi baada ya dakika chache. Kuchunguza kwa karibu mara nyingi ni rahisi zaidi na nzi moja anajilisha kuliko na nzi kwenye ardhi, kwa kuwa nzi hao ni wepesi sana wa kuruka mara ya kwanza kuona maumbo yanayosogea au vivuli vinavyokaribia.

 
Xenox tigrinus wakipandana

Tabia ya kupandana imeonekana tu katika spishi chache. Inaweza kutofautiana kutoka kujaa wa kawaida au unyanyasaji wa katikati ya hewa bila kuomba, kama ilivyo kawaida katika Diptera nyingi, hadi tabia ya uchumba inayohusisha ruwaza ya kurukaruka inayozingatia muktadha na sauti ya mpigo wa mabawa ya dume, akiwa na au bila mawasiliano ya mara kwa mara ya neli ya kulishia kati ya dume na jike. Madume mara nyingi hutafuta maeneo wazi madogo au makubwa zaidi ardhini, pengine karibu na mimea inayochanua maua au maeneo ya kutagia ambayo yana uwezekano wa kuvutia majike. Wanaweza kurudi kwenye mkao au sehemu ya ardhi waliyochagua baada ya kila kipindi cha kujilisha au baada ya kufukuza wadudu wengine wanaoruka juu, au badala yake wanaweza kuchunguza eneo walilochagua huku wakielea kwa mita moja au zaidi juu ya sehemu yao wazi.

Majike wenye mayai yaliyokomaa hutafuta makazi ya vidusiwa na wanaweza kutumia dakika nyingi kukagua kwa mfano viingilio vya mashimo madogo kwenye udongo. Katika baadhi ya spishi tabia hii inajumuisha kuelea na kugusa udongo mara kwa mara kwa miguu ya mbele kwa chini ya sekunde moja karibu na ukingo wa mlango wa shimo, labda ili kugundua dalili za kibiokemia kuhusu mjenzi wa shimo kama vile utambulisho, ujio wa hivi karibuni n.k. Ikiwa shimo litapita uchunguzi basi nzi-nyuki anaweza kutua na kuingiza sehemu ya nyuma ya fumbatio lake kwenye udongo na kutaga yai moja au zaidi pembezoni au karibu nayo. Katika nusufamilia tisa, ikijumuisha Bombyliinae na Anthracinae zinazoonekana mara kwa mara, majike mara nyingi hawatui kabisa wakati wa ukaguzi wa mashimo ya vidusiwa na wataendelea kutoa mayai yao kutoka angani kwa kupepesuka kwa fumbatio haraka huku wakielea juu ya mlango wa shimo.

Villa sp. akikusanya chembe za mchanga

Tabia hii ya ajabu imefanya spishi kama hizo kupata jina la kawaida la nzi wabomuaji. Inaweza kuonwa kwenye klipu ya video ya mtandaoni ya Roy Kleuker kwenye YouTube[3]. Nzi wa kike wenye mkakati huu wa ajabu wa kutaga mayai kwa kawaida huwa na muundo wa akiba unaojulikana kama stoo ya mchanga kwenye ncha ya nyuma ya fumbatio, ambayo hujazwa na chembe za mchanga zilizokusanywa kabla ya kutaga mayai[4][5]. Chembe hizi za mchanga hutumika kupaka kila yai muda mfupi kabla ya kutolewa kutoka angani, ambayo inachukuliwa kuboresha lengo la jike na pia nafasi ya kuishi ya yai kwa kuongeza uzito, kupunguza kasi ya ukaushaji wa yai, kuzuia dalili za kibiokemia ambazo zinaweza kusababisha tabia ya kidusiwa kama kusafisha kiota au kukitelekeza, au mchanganyiko wa zote tatu.

Licha ya idadi kubwa ya spishi za familia hii, biolojia ya mabuu wa spishi nyingi haieleweki vizuri. Ukuaji wa baada ya hatua ya kiinitete ni wa aina ya hipermetamofisisi, mabuu wakiwa vidusia au vidusia wa vidusia. Hitilafu ni mabuu ya Heterotropinae, ambao biolojia yao ni sawa na ile ya Asiloidea nyingine, ambao wana mabuu mbuai bila hipermetamofosisi. Vidusiwa wa nzi-nyuki ni wana wa oda tofauti za wadudu, lakini wengi wamo miongoni mwa oda za kiholometabolismu. Miongoni mwao ni Hymenoptera, hasa familia za juu za Vespoidea na Apoidea, mbawakawa, nzi wengine na nondo, lakini pia panzi, nzige, senene na vitukutuku[6]. Viwanja vya vibumba vya mayai ya nzige vilivyosongamana, kama vile vya nzige-jangwa, huathirika mno vyenye viwango vya udusio vya hadi 10-20%.

Tabia ya mabuu wa nzi-nyuki wanaojulikana ni sawa na ile ya mabuu wa Nemestrinidae: hatua ya kwanza ya buu ni planidio, huku hatua nyingine zikiwa na tabia ya kidusia. Mayai hutagwa kwa kawaida katika kidusiwa wa siku zijazo au kwenye kiota ambamo kidusiwa hukua. Planidio huingia katika kiota na hubadilika kuwa fomu ya kidusia kabla ya kuanza kujilisha.

Spishi kadhaa za Afrika ya Mashriki

hariri
  • Anastoechus bahirae
  • Anthrax dentata
  • Anthrax johanni
  • Atrichochira pediformis
  • Beckerellus melanopus
  • Bombomyia discoidea
  • Bombylella rufiventris
  • Bombylius acrophylax
  • Bombylius basifumatus
  • Bombylius cinereipilus
  • Bombylius erythrocerus
  • Bombylius fraudator
  • Bombylius mollis
  • Bombylius tripudians
  • Bombylius uniformis
  • Caecanthrax inauratus
  • Canariellum neavei
  • Diatropomma carcassoni
  • Diatropomma annettae
  • Diatropomma claudia
  • Exhyalanthrax afer
  • Exoprosopa selenops
  • Heteralonia azaniae
  • Heteralonia suffusa
  • Hyperusia apiformis
  • Legnotomyia striata
  • Oestranthrax speiserianus
  • Oestranthrax pix
  • Palintonus austeni
  • Paxyanthrax cunamae
  • Petrorossia albula
  • Petrorossia letha
  • Phthiria fumata
  • Plesiocera ochracea
  • Pusilla longirostris
  • Sisyrophanus stylifer
  • Systoechus aurifacies
  • Systoechus somali
  • Thyridanthrax perspicillaris
  • Tomomyza pictipennis
  • Zyxmyia megachile

Marejeo

hariri
  1. Alan Weaving; Mike Picker; Griffiths, Charles Llewellyn (2003). Field Guide to Insects of South Africa. New Holland Publishers, Ltd. ISBN 1-86872-713-0.
  2. Hull, Frank Montgomery, Bee flies of the world: the genera of the family Bombyliidae Washington, Smithsonian Institution Press 1973. Downloadable from: https://archive.org/details/beefliesofworl2861973hull
  3. Archived at GhostarchiveKigezo:Cbignore and the Wayback MachineKigezo:Cbignore: Roy Kleukers (22 Juni 2013). "Gewone wolzwever Bombylius major, eieren droppend in een kolonie zandbijen" – kutoka YouTube.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)Kigezo:Cbignore
  4. Yeates David K (1997). "The evolutionary pattern of host use in the Bombyliidae (Diptera): a diverse family of parasitoid flies". Biological Journal of the Linnean Society. 60 (2): 149–185. doi:10.1111/j.1095-8312.1997.tb01490.x.
  5. zoolstud.sinica.edu.tw/Journals/48.2/141.pdf Boesi, R., Polidori, C. and Andrietti, F. 2009. Searching for the Right Target: Oviposition and Feeding Behavior in Bombylius Bee Flies (Diptera: Bombyliidae). Zoological Studies 48: 141-150.
  6. The evolutionary pattern of host use in the Bombyliidae (Diptera): a diverse family of parasitoid flies