Qasem Soleimani (kwa Kiajemi: قاسم سلیمانی ‎, 11 Machi 1957 - 3 Januari 2020) alikuwa meja jenerali wa Iran katika Kikosi cha Kiislamu cha Walinzi wa Mapinduzi (IRGC). Kuanzia mwaka 1998 hadi kifo chake mwaka 2020, alikuwa kamanda wa Kikosi cha Quds katika IRGC.

Soleimani[dead link] mnamo 2019.

Maisha hariri

Alizaliwa 1957 Qanat-e Malek, mkoa wa Kerman, baba yake alikuwa mkulima. Alisoma shule ya sekondari. Baada ya kipindi cha kufanya kazi ya ujenzi wa nyumba aliajiriwa na idara ya maji mjini Kerman.

Mwaka 1979, baada ya mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran alijiunga na wanamgambo Waislamu waliokuwa watangulizi wa IGRC. Mwaka 1980, wakati Iran iliposhambuliwa na Irak chini ya Saddam Hussein, Soleimani alikuwa mwanajeshi katika IGRC akaendelea haraka kusimamia divisheni na kufikia cheo cha luteni jenerali[1][2].

Baada ya vita aliendelea kuhudumia akiwa kamanda wa IGRC katika mkoa wa Kerman alipoongoza mapambano dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya. Mwaka 1999, wakati wa maandamano ya wanafunzi wa vyuo vya Iran waliodai demokrasia, alitia sahihi kwenye barua ya viongozi wa IGRC iliyotaka serikali kuchukua hatua dhidi ya wanafunzi na kudokeza vinginevyo IGRC ingeingilia kati.[3]

Tangu kuteuliwa mkuu wa kikosi cha Quds, Suleimani alizunguka katika nchi jirani alipojenga uhusiano wa karibu na wanamgambo walioshiriki na Iran, hasa Washia na maadui wa Marekani. Wakati ule hakujulikana sana kitaifa na kimataifa isipokuwa kati ya wataalamu wa habari za kijeshi.

Mwaka 2001, baada ya mashambulio ya Al-Qaeda dhidi Marekani, wakati ambako Wataliban wa Afghanistan waliamua kumficha na kumlinda Osama bin Laden na kundi lake, Iran ilishirikiana na Marekani kushambulia Wataliban. Soleimani aliongoza timu ya Wairani waliowasiliana na Marekani. Ushirikiano huu ulikwisha baada ya hotuba ya rais George W. Bush iliyotaja Iran kuwa sehemu ya "axis of evil".[4]

Suleimani alijitahidi hasa kuimarisha uhusiano na Hisbollah wa Lebanoni, wanamgambo Washia waliowahi kuanzishwa na IGCR. Wakati wa vita ya Israeli dhidi ya Hisbollah mnamo 2006 alikuwepo Lebanoni na kushauri Hisbollah. [5]

Baada ya uvamizi wa Iraq na Marekani mnamo mwaka 2003 Soleimani aliwasiliana na vikundi vingi akilenga kwanza kuunganisha makundi ya Washia, halafu pia kujenga ushirikiano na makundi ya Wakurdi na Wasunni Warabu dhidi ya Wamarekani na pia dhidi ya Wasunni wenye itikadi kali walioshikamana na Al-Qaeda ambao wanatazama Washia kama wazushi wa dini wanaostahili kuuawa. Soleimani alihusika kukusanya na kufundisha wanamgambo Washia na kuwapatia silaha, kama Kata'ib Hezbollah walioshambulia Wamarekani kuanzia mwaka 2006.[6]

Mwaka 2011 Soleimani alipandishwa cheo na kuwa meja jenerali [7].

Alianza kuwa mashuhuri tangu kuripotiwa katika media ya Iran kuanzia mwaka 2012. Wakati ule alianza kushauri serikali ya Syria dhidi ya wapinzani wake katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Alituma vikosi vya IGRC Syria waliopambana na wapinzani wa serikali. Katika mapambano ya kuvamia mji wa Aleppo, Soleimani alikuwa kamanda aliyesimamia vikosi vya jeshi ya Syria pamoja na Hisbollah wa Lebanoni, vikosi vya IGRC kutoka Iran na wanamgambo kutoka Iraq dhidi ya watetezi wa Aleppo.

Wakati wa uenezi wa Daesh aliongoza pia mapambano dhidi yao nchini Iraki mnamo 2014–15.

Mashambulio yake dhidi ya jeshi la Marekani yalisababisha kutangazwa kwake kama adui na gaidi na serikali ya Marekani.

Mwaka 2020 aliuawa na bomu la Marekani alipowasili Baghdad kwa ndege.

Sifa na ukosoaji hariri

Kwa uongozi wa kisiasa, Soleimani alikuwa chombo muhimu cha kueneza athira ya Iran katika Mashariki ya Kati. Kwa kuingilia na kuokoa serikali ya Assad pale Syria, aliunganisha Lebanoni na Hisbollah yake (rafiki wa Iran tangu miaka mingi) na Irak, nchi nyingine ta Washia wengi. Hivyo aliwezesha usafirishaji wa silaha kwenda Hisbollah inayotumiwa kama tishio dhidi ya Israeli, adui mkuu katika itikadi ya watawala wa Iran. Kwa raia wengi wa Iran Soleimani alikuwa askari safi asiyehusika na ufisadi na aliyeshinda tishio la Daesh (ISIS) iliyoua Washia wengi[8].

Wasyria wengi wanaopinga serikali walimwona Soleimani kama mhusika mkubwa katika mapigano ambako vikosi vilivyokuwa chini ya mamlaka yake viliua makumi elfu, kufukuza lakhi za watu kutoka nyumba zao na kuokoa utawala wa rais Assad.

Nchini Irak wanamgambo waliokuwa chini ya Soleimani walitumiwa kukandamiza maandamano dhidi ya ufisadi katika serikali kwenye Novemba 2019.

Huko Yemen alihusika katika usaidizi wa Iran kwa Wahuti katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Hivyo habari za kuuawa kwake zilileta maandamano ya kuonyesha huzuni[9], lakini katika sehemu za Syria na Irak pia dalili za furaha[10].

Tanbihi hariri

  1. Weiss, Michael (2 July 2014). Iran's Top Spy Is the Modern-Day Karla, John Le Carré's Villainous Mastermind. The Daily Beast. Iliwekwa mnamo 14 July 2016.
  2. The enigma of Qasem Soleimani and his role in Iraq. Al Monitor (13 October 2013). Iliwekwa mnamo 14 July 2016.
  3. Letter of 24 Senior Commanders of the Holy Defense to the President of the Republic July 27, 1999,Translated by George Maschke
  4. The Shadow Commander Dexter Filkins, tovuti ya The New Yorker, September 23, 2013
  5. Soleimani: Mastermind of Iran's Expansion (14 October 2019).
  6. [hhttps://www.al-monitor.com/pulse/originals/2013/03/soleimani-iraq-syria-difference.html Iran's Man in Iraq and Syria], Mushreq Abbas katika tovuti ya al-monitor.com, 12 Machi 2013
  7. Alfoneh, Ali (March 2011). "Iran's Secret Network: Major General Qassem Suleimani's Inner Circle". Middle Eastern Outlook 2. Archived from the original on 24 July 2012. Retrieved 18 February 2013.  Unknown parameter |url-status= ignored (help)
  8. Gallagher, Nancy; Mohseni, Ebrahim; Ramsay, Clay (October 2019), "Iranian Public Opinion under "Maximum Pressure", A public opinion study", The Center for International and Security Studies at Maryland (CISSM), archived from the original on 3 January 2020, retrieved 6 January 2020  Unknown parameter |url-status= ignored (help)
  9. Soleimani: Huge crowds pack Tehran for commander's funeral. tovuti ya BBC ya tar. 6 January 2020, iliangaliwa Januari 2020
  10. Fear and joy on the streets of Baghdad after Soleimani killing, tovuti ya france24.com ya tar. 3.1.2020, iliangaliwa Januari 2020
  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Qasem Soleimani kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.