Jamii ya Marafiki

(Elekezwa kutoka Quaker)


Jamii ya Marafiki (kwa Kiingereza: Society of Friends), wakati mwingine pia Kanisa la Marafiki (Friend's Church) ni jumuiya ya kidini yenye mizizi katika Ukristo. Kimataifa hujulikana kwa jina la Kiingereza "Quaker" (tamka kweka).

Nyumba ya mikutano ya Urithi iliyoorodheshwa na Quaker, Sydney, Australia.

Makweka walio wengi hujitazama kuwa Wakristo lakini wanakubali pia wanachama wasio Wakristo wakitumia urithi wa dini nyingine kama Ubuddha au wasiojiona kufuata mafundisho maalumu. [1]

Wanapatikana kote duniani lakini vikundi vikubwa kiasi viko Kenya, Marekani, Bolivia, Guatemala, Ufalme wa Muungano (Uingereza) na Burundi. [2]

Mnamo mwaka 2017, kulikuwa na wafuasi wenye umri wa watu wazima 377,557, nusu yao waliishi Afrika.[3]

Historia

hariri

Jamii ya Marafiki ilianza mnamo mwaka 1650 huko Uingereza. Mtu, kwa jina George Fox, alitafuta njia ya kuwa Mkristo mwema hadi aliposikia sauti aliyoelewa ni sauti ya Mungu. Sauti ikimwambia kuwa Kristo atamwekea wazi ni nini anapaswa kufanya. Hapo Fox alianza kuhubiri eti, watu wote wanaweza kuongea na Mungu wenyewe - hawahitaji kasisi au mhudumu kuwafanyia. Aliwaambia kwamba ikiwa watasikiza ndani yao wenyewe watamsikia Kristo akiwaambia nini cha kufanya.

Pamoja na wengine alianzisha harakati ya kidini ambayo baadaye ilikuwa Jamii ya Marafiki. Fox alishtakiwa kuwa mzushi wa kidini; mbele ya mahakama alimwambia jaji atisike mbele ya Mungu (kwa Kiingereza "quake"), na hapa iko asili ya jina "quaker". Mwanzoni ilikuwa jina la kuwatania wafuasi wa Fox lakini waliipokea wenyewe kama jina la heshima.

Ukandamizaji

hariri

Serikali ya Uingereza ililenga kukandamiza kikundi hiki kipya kwa kuwapiga marufuku kwa muda wa miaka 20; wakati huo ilikuwa kinyume cha sheria kusali nje ya Kanisa rasmi la Uingereza. Wengi waliwekwa jela, wengine kulipishwa faini kali, wengine walihamia kwenye makoloni ya Amerika yaliyoendelea baadaye kuwa nchi mpya ya Marekani.

Marekani

hariri

Kweka kijana William Penn alipata kibali cha mfalme kuunda mji mpya kwenye pwani ya Amerika alianzisha koloni jipya la Pennsylvania huko. Ilikuwa kati ya maeneo ya kwanza ambako wafuasi wa dini na madhehebu yote walivumiliwa na kuruhusiwa kufuata dini zao. Penn alifuata pia nyingine ya pekee akitafuta maelewano ya amani na wenyeji Waindio.

Marafiki na utumwa

hariri

Jamii ya Marafiki ilikuwa jumuiya ya kwanza ya kidini katika historia iliyopinga utumwa jumla.

Chanzo chake kilikuwa azimio la marafiki 4 Waholanzi na Wajerumani pale Pennsylvania kwenye mwaka 1688. Walipinga kuwepo kwa watumwa katika koloni lao katika azimio la Aprili 1688[4]. Matamko yao yalianzisha majadiliano ndani ya jamii yao kama ni halali kwa Mkristo kuwa na watumwa.

Katika karne ya 18 Marafiki wa Uingereza walikazia zaidi upinzani dhidi ya watumwa. Mwaka 1783 Marafiki 300 walipeleka ombi bungeni kukomesha biashara ya watumwa. Kwa kushirikiana na Wakristo walianzisha Shirika kwa Ukomeshaji wa Biashara ya Watumwa. Shirika hilo liliendesha kampeni nyingi nchini Uingereza, ama makanisani, au wakati wa kampeni ya bunge, au katika mikutano ya hadhara.

Hatimaye kempeni hii ilifaulu mwaka 1807 kuleta azimio la bunge lililopiga marufuku biashara ya watumwa, ingawa bado si utumwa mwenyewe, kote katika Milki ya Britania.

Ibada za jumuiya hii huitwa "mikutano ya kuabudu".

Kwa jumla kuna mitindo miwili tofauti kati ya jumuiya zao

  • wanaofuata ibada kimya
  • wanaofuata ibada za ratiba

Walio wengi hufuata ibada za ratiba, hasa kwa sababu wamisionari wa kwenda Afrika walitoka katika urithi huu.

Ibada kimya

hariri

Huu ni urithi asilia unaofuatwa Ulaya, katika sehemu za Marekani na mahali pachache Afrika.

Wanaanza kwa kila mtu kukaa kimya. Hapo wanajaribu kumsikiza Mungu. Kama mmoja anahisi kuwa Mungu amemwambia kitu anasimama na kuwaambia wengine. Halafu wote hukaa kimya tena. Inawezekana mkutano wote ni kimya kama hakuna anayesimama. Kwa kawaida, muda wa mkutano wao ni kama saa moja.

Mtu yeyote anaweza kushiriki kwenye mikutano yao.

Quaker pia huwa na mikutano ya ibada kwa arusi na mazishi - wakati watu wawili wanafunga ndoa, au ikiwa mtu amekufa. Wakati watu wawili wanapofunga ndoa, mkutano ni juu yao na maisha ambayo wataishi pamoja. Wakati mtu amekufa, mkutano ni juu ya kukumbuka vitu juu ya mtu huyo na maisha waliyokuwa nayo.

Ibada za ratiba

hariri

Marafiki wengi katika Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, na Afrika wanafuata mitindo yenye ratiba, kwa hiyo mikutano yao hufanana na ibada za madhehebu mengine.

Wanaimba nyimbo na yupo mhubiri anayetoa mahubiri. Kuna pia kipindi cha kimya, lakini hakidumu kwa muda mrefu. Marafiki hao hukazia zaidi mafundisho ya Kikristo.

Marafiki hutafuta ukweli wa kidini ndani yao wenyewe. Wanategemea dhamiri yao kama mwongozo wa maisha ya kila siku.

Walio wengi hukubaliana imani hizi:

  • Kuna sehemu ya Mungu ndani ya kila mtu, kwa hiyo kila mtu ni muhimu. Hii ndiyo sababu Marafiki huthamini watu wote kwa usawa, na kupinga kitu chochote kinachoweza kuwadhuru au kuwatisha.
  • Mungu anaweza kupatikana katika maisha ya kila siku kama vile wakati wa mikutano ya kuabudu.
  • Kila mtu ana "mwanga wa ndani" ambayo humwambia anapaswa kufanya nini. Mwanga wa ndani unatoka kwa Mungu.
  • Kila mtu anapaswa kuelekea pale Mungu anapomtaka.
  • Mtu anapaswa kujaribu kutoumiza watu wengine.
  • Mtu aseme ukweli asiseme uwongo. Marafiki huona ukweli ni muhimu sana.
  • Marafiki hufundisha tusitumie pesa nyingi kwa ajili yetu sisi wenyewe, au kuvaa nguo zinazoonyesha utajiri.
  • Watu wanatakiwa kutunza uasilia na mazingira

Marafiki katika Afrika

hariri

Marafiki walio wengi wanaishi Afrika. Kenya huwa na jamii kubwa duniani waliokuwa 146,300 kwenye mwaka 2012[5], ilhali Marekani (nchi ya pili katika idadi ya marafiki hao) walikuwepo 76,360, wakiwa 35,000 pale Burundi na 22,300 Bolivia.

Marafiki wa Kenya walianzishwa mwaka 1902 wakati watatu walifika kutoka Cleveland, Marekani, wakielekea Kisumu kwa reli na kuanzisha kituo pale Kaimosi. Walitoka katika urithi wa ibada ya ratiba. [6]

Marafiki walizidi kuenea Kenya hasa maeneo ya magharibi. Kaimosi iliongezekwa hospitali ya misioni na taasisi ya Biblia. Marafiki waliendela kuenea hadi Uganda na Tanzania.

Kuna mikutano 14 nchini Kenya. Zinafuata mtindo wa ibada ya ratiba, Nairobi kuna kundi dogo la ibada kimya[7].

Afrika Kusini

hariri

Marafiki wa nchi hii walianzishwa kutoka Uingereza, wanafuata mtindo wa ibada kimya. Ni kundi moja dogo.

Marejeo

hariri
  1. "Quakers - the Religious Society of Friends". BBC. Iliwekwa mnamo 2009-09-05.
  2. "2012 map". Friends World Committee for Consultation - Section of the Americas. 2012. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-03-27. Iliwekwa mnamo 5/7/16. {{cite web}}: Check date values in: |accessdate= (help)
  3. "Finding Quakers Around the World" (PDF). Friends World Committee for Consultation. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-02-05. Iliwekwa mnamo 14 Machi 2019. {{cite web}}: More than one of |accessdate= na |access-date= specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. First Protest Against Slavery, Germantown, PA, April 18, 1688
  5. "Finding Quakers Around the World" (PDF). Friends World Committee for Consultation. 2012. Iliwekwa mnamo 2016-07-04.
  6. "Quakers and Peace in Africa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2011-07-24. Iliwekwa mnamo 2016-07-09. {{cite web}}: More than one of |accessdate= na |access-date= specified (help)
  7. The Future of Quakerism Belongs to Kenya
  Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.