Silvesta Guzzolini

Silvesta Guzzolini (Osimo 1177Fabriano 26 Novemba 1267) alikuwa padri mmonaki wa mkoa wa Marche, Italia aliyerekebisha utawa wa Wabenedikto kwa kuanzisha tawi linaloitwa Wasilvesta.

Mt. Silvesta alivyochorwa na msanii asiyejulikana katika karne ya 15.
Sanamu yake katika St. Sylvester's College, Kandy, Sri Lanka.

Papa Klementi IV alimthibitisha kuwa mwenye heri, halafu Papa Klementi VIII alimtangaza mtakatifu mwaka 1598.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 26 Novemba.[1][2]

Maisha

hariri

Mwana wa ukoo maarufu wa Osimo, alitumwa kusoma sheria katika chuo kikuu cha Bologna, halafu Padua.

Lakini alijisikia wito, hivyo akabadili masomo akachukua teolojia na Biblia. Uamuzi huo haukumpendeza baba yake, ambaye kwa sababu hiyo alikataa kusalimiana naye miaka 10.

Silvesta akawa padri mkanoni huko Osimo akajitosa katika uchungaji kiasi cha kusababisha kijicho cha askofu wake, hasa baada ya kumkosoa kwa mwenendo wake mbaya.[3]

Basi, mwaka 1227 alikwenda kuishi upwekeni katika ufukara wa hali ya juu mpaka alipopewa nafasi nyingine huko Grotta Fucile, karibu na Fabriano, alipoanzisha monasteri.[3]

Huko alifanya toba kali, akila tu majani mabichi na kunywa maji, pamoja na kulala ardhini. Hata hivyo wengi waliamua kumfuata hata ikambidi kuchagua kanuni ya kitawa, ikawa ile ya Benedikto wa Nursia.

Baadaye alijenga monasteri kwenye Montefano, upande wa pili wa eneo la Fabriano, na nyingine 11 sehemu mbalimbali za Italia, hata za kike.[3]

Mwaka 1248 alipewa na Papa Innocent IV, huko Lyon, hati ya uthibitisho kwa shirika lake.

Silvesta alifariki akiwa mkongwe tarehe 26 Novemba 1267.[4]

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
WikiMedia Commons