Takataka ya angani

Takataka ya angani ni jumla ya vitu vilivyo na asili katika kazi ya binadamu, vilivyopo kwenye anga-nje na ambavyo havina manufaa tena.

Uchafu wa anga karibu na Dunia kwa mtazamo wa juu-chini. Wingu la katikati ni vitu vilivyo kwenye obiti ya chini ya Dunia, na pete pembeni ni vitu kwenye obiti ya geostationary.

Mifano na ufafanuzi

hariri

Mifano ni satelaiti ambazo hazifanyi kazi tena, zilizovunjika, sehemu za roketi, vipande vya metali vilivyokuja kama sehemu za roketi, na mengine mengi. Vitu hivi vyote hutazamwa kama takataka hasa katika obiti yaani njia za satelaiti za kuzunguka Dunia kwa sababu vipande vile vinaendelea kuzunguka Dunia kwenye obiti hizo. Takataka hiyo ni hatari kwa satelaiti, kituo cha anga na pia wanaanga waliopo kwenye obiti kwa sababu migongano inatokea.

Hatari za takataka ya angani

hariri
 
Shimo kwenye ukuta wa chomboanga Spaceshuttle lililotokana na kupigwa na takataka mwaka 2008.

Hatari inatokana hasa na kasi kubwa ya vitu vilivyopo kwenye obiti ambayo ni takriban km 27,000 kwa saa [1]. Hii ni mara 10-20 kasi ya risasi ya bunduki.

Hadi sasa mgongano wa satelaiti mbili umetokea mara moja tu, moja ilikuwa satelaiti iliyokufa tayari na nyingine ilikuwa satelaiti mpya[2]. Lakini satelaiti zimewahi kupigwa na vipande vidogo mara kadhaa.

Kituo cha Anga cha Kimataifa (ISS) kina ukuta maradufu; kompyuta duniani hukadiria njia yake pamoja na njia za vipande vikubwa vya takataka; kama vipande vikubwa vinaonekana kukaribia ISS, kituo kinashushwa au kupandishwa kidogo kwa kutumia nozeli za gesi; kama hali hatarishi inaonekana wanaanga wanaweza kuhamia kwenye chomboanga cha Soyuz kilichopo muda wote kwenye ISS kwa hali ya dharura. Kama mwanaanga angepigwa na kipande kidogo cha takataka akiwa nje ya kituo, hatari ya kufa ni kubwa.

Vyanzo vya takataka ya angani

hariri
 
Ngazi ya juu ya roketi Delta II ya Marekani iliyopeleka satelaiti kwenye obiti, ikabaki angani.

Vyanzo vya takataka ya angani ni pamoja na:

 • satelaiti zilizokufa
 • ngazi za juu za roketi zilizopeleka satelaiti hadi obiti na kubaki humo baada ya kutengana na satelaiti yenyewe
 • vipande vidogo kama skrubu na bolti vinavyoachana na roketi wakati wa kutengana na satelaiti
 • vipande vya satelaiti na roketi vinavyotokana na milipuko (body break up)[3]
 • vipande vya satelaiti vinavyotokana na majaribio ya kijeshi, kama vile kuharibu satelaiti kwa roketi kutoka duniani kama jaribio la kulenga, au kwa bomu
 • vipande vinavyotokea baada ya kugongana kwa takataka na kuvunjika

Idadi ya vipande vya takataka ambavyo ni vikubwa kuliko sentimita 1 hukadiriwa kuwa karibu milioni moja [4]; vipande vidogo zaidi ya sentimita hukadiriwa kuwa milioni nyingi.

Historia

hariri
 
Satelaiti ya Vanguard 1 ya 1958, itakayoendelea kuzunguka Dunia kwa miaka 200

Takataka ya angani ilianza kwa satelaiti zisizo na kazi tena. Mfano wa zamani zaidi ni satelaiti ya Vanguard I. Satelaiti hiyo ilipelekwa na Marekani kwenye anga-nje mwaka 1958. Kazi yake ilikuwa kurusha ishara za redio duniani. Vifaa vyake zake vilifanya kazi hadi mwaka 1964, baadaye ishara zake zilizimika. Tangu miaka 60 haina kazi tena lakini bado inazunguka Dunia, pamoja na sehemu ya roketi iliyoibeba hadi obiti yake[5].

Wakati ule, miaka 60 iliyopita, hakuna aliyeyaita mabaki hayo takataka. Hadi leo mambo yamekuwa tofauti. Leo hii kuna zaidi ya satelaiti 6,000 zinazozunguka Dunia yetu kwenye anga-nje. Zaidi ya nusu ya idadi hiyo haina kazi tena. Fueli imekwisha, betri zimekufa, mitambo ndani yake imeharibika, ni mibovu lakini bado iko tu.

Hatua za kuondoa takataka kwenye anga-Nje

hariri

Vitu vyote vinavyozunguka Dunia kwenye obiti ya chini vinakutana na molekuli za hewa ambazo zinasababisha msuguano. Kiwango chake ni kidogo lakini kila chombo au pia kipande cha takataka kinachogusana na molekuli za hewa kitapungua mwendo wake kidogo. Kwa hiyo polepole kasi inapungua na chombo kinaanza kushuka chini na hatimaye, baada ya miaka kadhaa, kuingia katika angahewa lenyewe. Hapo msuguano huwa mkubwa na kusababisha joto kali. Kama satelaiti si kubwa sana itaungua kabisa hewani kama kimondo. Kama ni kubwa vipande kadhaa vinaweza kubaki na kuangukia uso wa Dunia.

Kadri umbali wake ni mkubwa muda wa kubaki kwenye obiti unaongezeka hadi karne au zaidi.

Satelaiti kwenye obiti za mbali zinaandaliwa ya kupelekwa katika obiti ya takataka ambayo ni mbali zaidi. Hapo taasisi inayomiliki chombo cha aina hiyo itatumia fueli ya mwisho kukirusha tena kwenye obiti ya mbali itakapoendelea kwa milenia bila kuumbuka satelaiti mpya.

Ufuatiliaji

hariri

Kuna taasisi mbalimbali zinazotunza orodha za vitu vilivyorushwa angani. Umoja wa Mataifa [6] Ofisi ya NORAD ya jeshi la Marekani ina orodha ya safari zote za kuelekea angani na vitu vilivyo kwenye obiti ya Dunia, pamoja na sehemu kubwa kiasi za taka, kama sehemu za juu za roketi.

Marejeo

hariri
 1. Why is small debris a problem?, tovuti ya Space Debris 101, ya aerospace.org, iliangaliwa Machi 2021
 2. Iannotta, Becky. "U.S. Satellite Destroyed in Space Collision", Space.com, February 22, 2009. Retrieved on February 12, 2009. Archived from the original on February 13, 2009. 
 3. Three breakups of derelict rocket bodies , tovuti la Debris Quarterly News linalotolewa na NASA, Volume 23, Issue 4 November 2019
 4. Space debris by the numbers, tovuti ya ESA Januari 2019;
 5. Vanguard 1 - Satellite Information, tovuti ya Heavens Above, kupitia archive.org
 6. United Nations Register of Objects Launched into Outer Space, tovuti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa Mambo ya Anga-Nje (UN-Office for Outer Space Affairs UNOOSA), iliangaliwa Machi 2021

Tovuti za nje

hariri