Vita ya Ufaransa dhidi ya Ujerumani ya 1870
Vita ya Ufaransa dhidi ya Ujerumani ya 1870 ilianza kama ugomvi baina ya Ufaransa na Prussia ikaendelea kuunganisha madola ya Ujerumani chini ya uongozi wa Prussia kwa kuundwa kwa Dola la Ujerumani.
Vita hiyo ilichochewa na waziri mkuu wa Prussia, Otto von Bismarck, ambaye alitaka kuunganisha Wajerumani chini ya uongozi wa Prussia kwa kuwafanya wapambane dhidi ya adui wa pamoja. Upande wa Ufaransa, kaizari Napoleon III alikuwa amedhoofika kisiasa akatafuta mafanikio katika vita ili aimarishe nafasi yake ndani ya Ufaransa. Hivyo Ufaransa ilitangaza vita mnamo 19 Julai 1870. Vita viliisha na ushindi wa Ujerumani mnamo 10 Mei 1871.
Sababu za vita
haririUjerumani ilikuwa jumla ya madola 28; baada ya Vita ya Kijerumani ya 1866 madola madogo yaliwahi kuungana na Prussia katika Shirikisho la Ujerumani ya Kaskazini. Madola makubwa zaidi ya kusini, kama Bavaria na Württemberg, yaliendelea kujitegemea. Wafaransa waliogopa maungano ya madola yote ya Ujerumani.
Mnamo mwaka 1869 Hispania ilimtafuta mfalme mpya aliyetakiwa kuzaliwa katika familia ya kifalme. Wahispania walimkaribisha kuwa mfalme mmoja wa ndugu za mfalme wa Prussia aliyetoka katika tawi la Kikatoliki la familia yake. Wafaransa walipinga mpango huo kwa sababu waliogopa kuwa na mtawala wa familia ya Prussia kwenye pande mbili. Mwanamfalme kutoka Ujerumani alielea ugumu akakataa ofa ya Hispania, lakini serikali ya Ufaransa ilitaka tamko rasmi la mfalme wa Prussia kwamba mwana wa familia yake hatakubali kamwe kuwa mfalme wa Hispania. Hapo Prussia haikuwa tayari. Taarifa katika magazeti zilichochea hisia za kizalendo katika Ufaransa na Ujerumani hadi Ufaransa itangaza vita dhidi ya Prussia.
Matokeo
haririTofauti na matumaini ya Ufaransa, madola ya kusini ya Ujerumani yaliamua kujiunga katika vita upande wa Prussia. Kwa hyo jeshi la Wajerumani lililoongozwa na Prussia lilikuwa kubwa kuliko lile la Ufaransa. Vilevile Waprussia walikuwa na silaha bora, hasa mizinga mikubwa, kuliko Wafaransa.
Baada ya mapigano kadhaa, kundi kubwa la jeshi la Ufaransa lilipaswa kusalimu amri mjini Sedan. Kaizari Napoleon III alikuwa kati ya wafungwa wa vita.
Habari za kufungwa kwake zilipofika Paris, wapinzani wa Napoleon III waliandamana na kudai Ufaransa iwe tena jamhuri. Wabunge walifuata madai hayo na kuunda serikali mpya.
Vita iliendelea kwa miezi kadhaa kwa sababu Wajerumani walidai majimbo mawili ya Ufaransa yapelekwe upande wa Ujerumani, ambayo yalikuwa maeneo ambako wananchi wengi waliongea Kijerumani, hasa Alsace pamoja na mji wa Strasbourg.
Kwa hiyo mapigano yaliendelea hadi Januari 1871 ambapo pande mbili zilipatana kusimamisha vita hadi kufikia mapatano ya amani.
Ufaransa ililazimishwa kukubali uhamisho wa majimbo ya Alsace na Lorraine (Kijer. Lothringen) upande wa Ujerumani na kulipa fidia kubwa.
Mjini Paris yalitokea mapinduzi ambapo wananchi walichukua silaha na kuunda "commune" iliyoshindwa na jeshi la Kifaransa hadi Mei 1871.
Maungano ya Wajerumani
haririBaada ya ushindi wa kijeshi wawakilishi wa madola ya Ujerumani waliwasiliana juu ya ushirikiano wa karibu zaidi. Hatimaye madola ya kusini yalijiunga na Shirikisho la Ujerumani ya Kaskazini lililoendelea sasa kwa jina la "Dola la Ujerumani".
Tarehe 18 Januari 1871 watawala wa madola ya Ujerumani au wawakilishi wao, walikutana katika jumba la kifalme la Versailles nje ya Paris wakamtangaza mfalme Wilhelm IV wa Prussia kuwa Kaizari Wilhelm I wa Ujerumani.
Matokeo mengine
haririIli kupambana na Ujerumani, Napoleon III alirudisha Ufaransa askari zake waliomlinda Papa na Roma, hivyo jeshi la Italia liliweza kuteka mji huo tarehe 20 Septemba 1870 na kuufanya mji mkuu wa ufalme wa Italia, huku Papa Pius IX akijifungia Vatikano.