Enzi ya barafu

(Elekezwa kutoka Zama za Barafu)

Enzi ya barafu ni kipindi cha historia ya dunia ambapo halijoto kwenye uso wa dunia ilikuwa duni kwa muda mrefu, yaani miaka elfu kadhaa au zaidi.

Kushuka kwa halijoto kwa muda mrefu kunasababisha kukua kwa barafuto kwenye ncha za dunia na milimani.

Kugunduliwa kwa enzi ya barafu

hariri
 
Mwamba mkubwa kando ya mto Elbe katika tambarare ya Ujerumani ya Kaskazini. Mwamba huu wa graniti unalingana na miamba ya milima ya Skandinavia iliyopo takriban kilomita 1,000 kaskazini ya hapo.
 
Hii ni kona ya ngao ya barafu huko Greenland mwaka 2005 (angalia watu wanaokaa upande wa kulia kwa ulingano wa urefu); ngao ya barafu wakati wa enzi ya barafu ilikuwa kubwa mara kadhaa zaidi.

Uwepo kwa enzi ya barafu ulianza kutambuliwa tangu karne ya 18. Wataalamu wa Ulaya walianza kujiuliza kuhusu kuwepo kwa miamba mikubwa katika mazingira pasipo na milima na mwamba. Mfano ni miamba mikubwa katika maeneo jirani ya milima ya Alpi au miamba ya graniti katika tambarare ya Ujerumani kaskazini ambako ardhi yote ni mchanga na udongo isipokuwa kuna mawemawe na miamba mikubwa ya namna jinsi zinavyojenga milima yenyewe. Wataalamu walianza kutambua ya kwamba miamba hii ilitokea mazingira tofauti na mahali inapopatikana sasa. Swali likaulizwa: ilifikaje hapo ilipo?

Mnamo mwaka 1742 mhandisi Pierre Martel (1706–1767) wa Geneva alitembelea bonde la Chamonix. Hapo alisikia ya kwamba wenyeji walikumbuka ya kwamba katika zamani za vizazi vilivyopita barafu ya barafuto ya mlimani iliwahi kufika chini zaidi kuliko wakati wake na vipande vikubwa vya miamba bondeni vilionyesha upeo wa barafu ya zamani. Hivyo miamba ilisukumwa na barafu ile hadi mahali ilipopatikana. Taarifa ilichapishwa: ni mara ya kwanza ya kwamba hoja hii ilitolewa kwa wasomi wa Ulaya. Wengine walimfuata baada ya kutembelea na kuchungulia kuwepo kwa miamba katika mabonde mengine ya Alpi na pia Andes ya Amerika Kusini.

Mhandisi Daniel Tilas (17121772) wa Uswidi alifikiri mnamo 1742 ya kwamba miamba ya graniti ilibebwa na vipande vikubwa vya barafu iliyoelea juu ya bahari hadi mahali inapopatikana katika nchi kando ya Bahari Baltiki.

Mnamo 1818 mtaalamu Mswidi wa botania Göran Wahlenberg (17801851) alieleza nadharia yake ya kwamba Skandinavia yote iliwahi kufunikwa na barafu iliyosukuma miamba hadi Ujerumani ya Kaskazini na nchi za Baltiki.

Mwanajiolojia Mdenmark Jens Esmark (17631839) alikuwa wa kwanza kuwaza ya kwamba vipindi vya upanuzi wa barafuto viliwahi kutokea kote duniani. Aliandika ya kwamba sababu ya kutokea kwa vipindi hivi ilikuwa mabadiliko ya halihewa duniani katika milenia zilizopita akajaribu kutoa maelezo kuwa mabadiliko hayo yalisababishwa na badiliko la mwendo wa dunia kuwa mbali au karibu zaidi na jua.

Mnamo 1832 Mjerumani Albrecht Reinhard Bernhardi (17971849) aliuliza kama barafu ya nchani iliweza kuenea hadi sehemu ya kusini katika nyakati za kale.

Mjerumani mwenzake mwanabotania Karl Friedrich Schimper (18031867) alitunga neno "Eiszeit" (enzi ya barafu) kwa vipindi vilivyopita ambapo halijoto duniani ilishuka na barafuto kubwa zilisukuma miamba kutoka mlimani hadi sehemu za tambarare inapopatikana sasa.

Wakati ule sehemu kubwa ya wataalamu walipinga mawazo yale maana hayakulingana na mafundisho kuhusu historia ya sayari yetu jinsi ilivyofundishwa na wengi.

Majadiliano yaliendelea kwa miaka kadhaa hadi miaka ya 1870 wataalamu wengi walikubaliana ya kwamba nadharia ya enzi ya barafu inaeleza vema kuwepo kwa miamba katika maeneo ambako aina hii ya mawe haipatikani kiasili.

Enzi za barafu

hariri

Leo hii sayansi inaona ya kwamba vipindi vya "enzi ya barafu" vilitokea mara kadhaa katika historia ya dunia yetu. Vipindi virefu zaidi dunia ilikuwa bila barafu ya kudumu kwenye ncha na kwenye milima ya juu.

Ndani ya kipindi cha enzi ya barafu kuna ngazi mbalimbali. Vipindi vya barafu nyingi zaidi hubadilishana na vipindi poa vya barafu kidogo. Majina ya Kiingereza ni "glacial period" na "interglacial period".

Sasa hivi dunia inaaminiwa kuwa ndani ya enzi ya barafu katika kipindi poa. Kipindi cha barafu nyingi kiliishia takriban miaka 11,000 iliyopita. Ngao ya barafu ilifunika sehemu kubwa ya Ulaya ya kaskazini na sehemu za Ujerumani, Uingereza, Poland na Urusi. Unene wa ngao ya barafu ulifikia kilomita kadhaa.

Ngao za barafu kwenye aktiki (hasa Greenland) na kwenye antaktiki bado ziko.

Sayansi haiwezi kutabiri kama tutakuwa tena na kipindi kali zaidi au kama enzi hii ya barafu inaelekea kwisha kabisa.

Wakati wa kipindi cha barafu nyingi iliyopita sehemu kubwa ya Amerika Kaskazini na Ulaya zilifunikwa na ngao nene za barafu.

Mabara yote yaliathiriwa na enzi za barafu katika historia. Sababu yake ni kwamba kila bara ilibadilisha mahali pake duniani katika mwendo wa miaka milioni kadhaa. Ulaya iliwahi kukaa kwenye eneo la tropiki na Afrika iliwahi kuwa karibu na ncha ya dunia.

Dalili za enzi ya barafu ilitambuliwa hasa katika Afrika Kusini. Ardhi katika eneo la Karoo linaonyesha tabia nyingi ya mashapo ya barafuto.

Mabadiliko ya enzi za barafu na uhai duniani

hariri
 
Ulaya takriban miaka 12,000 iliyopita, wakati wa kipindi kilichopita cha barafu nyingi

Mabadiliko ya enzi za barafu na vipindi vya barafu nyingi au vipindi poa vinaathiri kabisa uhai wote duniani, kuanzia mimea, wanyama hadi binadamu.

Kuongezeka kwa baridi husababisha maji mengi kuwa barafu. Ngao ya barafu ilifunika Skandinavia na Kanada yote pamoja na sehemu za Ujerumani, Uingereza, Poland, Urusi na Marekani. Maji yaliyokusanyika hapa kwa umbo la barafu yalisababisha kushuka kwa uwiano wa bahari kiwango cha mita 120. Wakati ule iliwezekana kutembea kwa miguu kutoka Asia hadi Amerika ya Kaskazini kupitia eneo ambalo leo ni mlango wa Bering, au kutembea kutoka Uingereza hadi Ulaya Bara, kutoka Bara Hindi hadi Sri Lanka na kadhalika. Kipindi kile kilirahisisha pia uenezi wa spishi nyingi za wanyama.

Kuongezeka kwa joto kuanzia miaka 11.000 iliyopita kunasababisha kuyeyuka kwa barafu na kuongezeka kwa maji ya bahari - kwa hiyo uwiano wa bahari unapanda juu. Visiwa ambavyo vina kimo cha mita chache tu vitafunikwa na maji. Pia sehemu za nchi bara zitafunikwa na maji na sehemu ya nchi kavu zitaonekana kama visiwa vipya.

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  • Cracking the Ice Age from PBS
  • Montgomery, Keith (2010). "Development of the glacial theory, 1800–1870". {{cite web}}: Invalid |ref=harv (help) Historical Simulation
  • Raymo, M. (Julai 2011). "Overview of the Uplift-Weathering Hypothesis". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-10-22. {{cite web}}: Unknown parameter |deadurl= ignored (|url-status= suggested) (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Eduard Y. Osipov, Oleg M. Khlystov. Glaciers and meltwater flux to Lake Baikal during the Last Glacial Maximum. Ilihifadhiwa 12 Machi 2016 kwenye Wayback Machine.
  • Black, R.. "Carbon emissions 'will defer Ice Age'", BBC News: Science and Environment, 9 January 2012.