Amu Darya (kwa Kiajemi: آمودریا) ni mto mkubwa katika Asia ya Kati. Unaundwa na muungano wa mito ya Vakhsh na Panj. Katika nyakati za zamani mto huo uliangaliwa kama mpaka kati ya Iran na Asia ya Kati.

Amu Darya آمودریا
Amu Darya nchini Turkmenistan
Chanzo Maungano ya mito Pamir na Panj kwenye mpaka wa Tajikistan na Afghanistan
Mdomo Ziwa Aral
Nchi Afghanistan, Tajikistan, Turkmenistan, Uzbekistan
Urefu km 2,620
Kimo cha chanzo Panj m 4,130, Vakhsh 4,525, inapoungana m 326
Tawimito upande wa kulia mto Panj
Tawimito upande wa kushoto mito Vakhsh, Surkhan Darya, Sherabad, Zeravshan
Mkondo Wastani m3/s 2,525, duni m3/s 420, juu m3/s 5,900
Eneo la beseni km2 534,739
Beseni la Amu Darya.

Majina ya kihistoria

hariri
 
Daraja la pantoni kwenye Mto Amu karibu na Urgench.

Mazingira ya mto huu yalikaliwa kwa milenia na watu wa makabila na mataifa waliobadilikabadilika wakitunza kumbukumbu katika maandiko. Kwa hiyo kuna majina mbalimbali yaliyohifadhiwa.

Zamani za Waarya waliohamia Uhindi kutoka Asia ya Kati takriban miaka 4000 iliyopita, mto ulitwa nao "Vaksu".

Wagiriki na Waroma wa Kale waliujua kwa jina la Oxos katika Kigiriki na Oxus katika Kilatini.

Jina la kisasa lina asili ya Kiajemi: limefanywa na maneno Amu na Darya. "Amu" (Amul, leo Türkmenabad) lilikuwa jina la mji kando ya mto uliokuwa kituo muhimu kwenye barabara ya hariri. "Darya" ni neno la Kiajemi kwa mto au bahari.

Njia ya mto

hariri

Chanzo cha maji yake ni hasa theluji ya barafuto mbalimbali katika milima ya Pamir inayolisha matawimto yanayoingia katika Amu Darya. Mto unabeba maji yake kaskazini ambako njia yake inaingia katika maeneo yabisi na hatimaye jangwani hadi kufika kwenye beseni la Ziwa Aral. Ziwa hilo lililishwa kwa milenia na maji ya Amu Darya. Lakini miradi mikubwa ya umwagiliaji iliyoanzishwa katika karne ya 20 ilipunguza kiasi cha maji kwenye mto; Ziwa Aral lilianza kupungua hadi kupotea na zaidi ya asilimia 90 ya eneo lake. Hata mto wenyewe haufiki tena ziwani bali unaishia jangwani kabla ya ziwa.

 
Ramani ya eneo karibu na Bahari ya Aral. Mipaka ya Ziwa Aral ni za mwaka 1960. Hadi wakati ule asilimia 90 zimepotea.

Urefu wa mto wote ni km 2400 na beseni lake ni eneo jumla ya km2 534,739. Maji yote hutoka kwenye milima mirefu kusini ambapo hali ya hewa ya kila mwaka inaweza kuwa zaidi ya mm 1,000. Hata kabla ya kuanzishwa kwa miraddi mikubwa ya umwagiliaji, takriban asilimia 40 ya maji zilipotea jangwani kwa njia ya uvukizaji.

Historia

hariri
 
Vikosi vya Urusi kuvuka Amu Darya, 1873 hivi.

Watu walianza kujenga makazi ya kudumu kwenye karne ya 5 BK wakianza pia kulima.

Amu Darya iliitwa Oxus na Wagiriki wa zamani. Katika nyakati za zamani, mto Anu arya ulizingatiwa kama mpaka kati ya Irān na Turan (Asia ya Kati). [1]

Beseni la Am Darya lilikuwa mara nyingi kama mpaka baina ya tamaduni na milki kubwa. Kwa mfano milki ya Aleksander Mashuhuri ilipata hapa mpaka wake wa kaskazini-mashariki, na milki ya Chingis Khan ilikuwa hapa na mpaka wake wa kusini.

Barabara ya hariri kutoka China kwenda Mashariki ya Kati ilitumia bonde la Amu Darya na kuwezesha ukuaji wa miji tajiri.

Katika karne ya 19 Urusi uliingiza Asia ya Kati katika milki yake. Nafasi yake ilichukuliwa na Umoja wa Kisovyeti kwa miongo mingi ya karne ya 20. Katika mfumo wa uchumi wa kikomunisti maji ya Amu Darya yalitumiwa kubadilisha nyika yabisi za Asia ya Kati kuwa nchi ya kilimo. Miradi mikubwa ya umwagiliaji ilipeleka maji yake mbali, hasa kwa kuwezesha mashamba makubwa ya pamba. Mifereji wa Qaraqum, Karshi na Bukhara ilikuwa kati ya njia kubwa zilizojengwa za kupeleka maji ya mto hadi mashamba yale. [2] Katika itikadi ile hifadhi ya mazingira haikuwa na umuhimu sana. Mifereji haikufunikwa, hivyo kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya uvukizaji.

Baada ya kuporomoka kwa ukomunisti beseni la Amu Darya liligawiwa kwa nchi mpya tofauti na usimamizi wa miradi haukuwa mzuri. Upotevu wa maji uliongezeka kwa sababu saruji ya mifereji iliyozeeka ilianza kuvunjika na hivyo kupotea maji zaidi.

 
Amu Darya ikipita jangwani.

Tanbihi

hariri
  1. Hitilafu ya kutaja: Invalid <ref> tag; no text was provided for refs named Iranica
  2. Pavlovskaya, L.P. "Fishery in the Lower Amu Darya Under the Impact of Irrigated Agriculture". Karakalpak Branch. Academy of Sciences of Uzbekistan. Iliwekwa mnamo 2010-02-09.

Marejeo mengine

hariri
  • Curzon, George Nathaniel (2005). The Pamirs and the Source of the Oxus. ISBN 1-4021-5983-8.
  • Gordon, T. E. 1876. The Roof of the World: Being the Narrative of a Journey over the high plateau of Tibet to the Russian Frontier and the Oxus sources on Pamir. Edinburgh. Edmonston and Douglas. Reprint by Ch'eng Wen Publishing Company. Taipei. 1971.
  • Toynbee, Arnold J. 1961. Between Oxus and Jumna. London. Oxford University Press.
  • Wood, John, 1872. A Journey to the Source of the River Oxus. With an essay on the Geography of the Valley of the Oxus by Colonel Henry Yule. London: John Murray.
  Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Amu Darya kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.