Maria Kresensya Hoess

Maria Crescentia Höss (Höß), T.O.R., (Kaufbeuren, Bavaria, Ujerumani, 20 Oktoba 1682 – Kaufbeuren, 5 Aprili 1744) alikuwa mwanamke mmonaki wa Utawa Hasa wa Tatu wa Mt. Fransisko.

Mt. Maria Kresensya.

Mwaka 1900, alitangazwa mwenye heri na Papa Leo XIII, halafu mwaka 2001 alitangazwa mtakatifu na Papa Yohane Paulo II.[1]

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kifo chake[2].

Maisha

hariri

Jina la kuzaliwa lilikuwa Anna Höss, mtoto wa sita kati ya nane wa Matthias Höss na Lucia Hoermann. Kati yao watatu tu walifikia utu uzima.

Anna alilelewa Kikristo sana, na tangu utotoni aliamua kuwa mtawa katika monasteri jirani ya Meierhof. Alikuwa akisali mara nyingi katika kikanisa chake, lakini ufukara wa baba yake haukumwezesha kutoa mahari iliyojitajika ili kukubaliwa.

Tofauti na monasteri za Waklara, zile za Utawa Hasa wa Tatu wa Mt. Fransisko zilikuwa chini ya askofu wa jimbo husika, na pengine zilikuwa na utendaji nje ya nyumba, kama vile kuhudumia maskini na wagonjwa. Lakini ile ya Kaufbeuren ililenga sala tu.

Mwaka 1703 Meya wa Kaufbeuren, akiwa Mprotestanti, aliisaidia monasteri kwa kununua kilabu cha jirani kilichokuwa kinavuruga utulivu wa masista akawapa jengo kama zawadi kwa sharti la kumpokea Anna jumuiani.[3]

Hivyo mnamo Juni mwaka huo Anna alipokewa, ila alitazamwa na wengi kama "mnyonyaji" kwa sababu ya kutoleta mahari. Paoja na hayo, Anna alipokea kanzu na jina la kitawa Maria Kresensya.

Mwanzoni alidhulumiwa kwa namna mbalimbali, kama vile kutukanwa, kuagizwa kazi duni zaidi, na kunyang'anywa chumba. Hivyo ilimbidi kuomba wenzake wamruhusu kulala katika pembe la vyumba vyao.

Hatimaye Kresensya aliruhusiwa kuweka nadhiri na kuwa mwanajumuia kamili. Hasa alipangiwa kazi za jikoni.

Mwaka 1707, alichaguliwa mkubwa mpya aliyempenda zaidi Kresensya, ambaye alipewa hivyo kazi muhimu ya bawabu, na mwaka 1717 ile ya mlezi wa wanovisi.[3]

Wakati huo alikuwa ameshaanza kuwa mwandishi wa barua nyingi, zenye mashauri kwa watu wa matabaka yote.

Ingawa maradhi yalizidi kumtesa, hata kupooza, mwaka 1741 alichaguliwa kuwa mkubwa wa nyumba, wadhifa aliokuwanao hadi kifo chake, tarehe 5 Aprili 1744.[3][4]

Katika miaka hiyo michache ya uongozi, Kresensya aliinua hali ya kiroho ya monasteri kwa imani yake kubwa kwa Maongozi ya Mungu, utayari wa kuhudumia jumuia, utunzaji wa kimya, ibada kwa Msulubiwa Yesu na kwa Ekaristi tena kwa heshima kwa Bikira Maria.

Alihimiza masista kutumia Injili ili kulisha maisha ya kiroho, akichuja sana waliotaka kujiunga, kwa kusema: "Mungu anataka monasteri iwe tajiri kwa maadili, si kwa mali".

Alijitahidi hasa kuwashirikisha wengine ari yake kwa heshima ya Roho Mtakatifu.

Alipotangazwa mtakatifu, monasteri ilibadilishiwa jina na kuitwa kwa lile la Mt. Kresensya.[5]

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri
  1. Homily of John Paul II at Vatican website
  2. Martyrologium Romanum
  3. 3.0 3.1 3.2 "St. Maria Crescentia Höss", Vatican News Service
  4. Father Robert F. McNamara. "St. Crescentia". Saints Alive. Irondequoit Catholic Communities. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-12-24. Iliwekwa mnamo 16 Januari 2009.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. Franziskanerinnen des Crescentiaklosters in Kaufbeuren (Kijerumani)

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  • Saint Maria Crescentia Hoss. Patron Saints Index.
  • Peter Stoll: Crescentia Höß of Kaufbeuren and her Vision of the Spirit as a Young Man. Universitätsbibliothek, Augsburg 2014 (full text)
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.