Mkoa wa Magharibi (Kenya)

Mkoa wa Magharibi (Western Province) ulikuwa mojawapo ya mikoa ya utawala ya Kenya nje ya Nairobi, ukiwa mkoa mdogo zaidi kati ya mikoa ya Kenya, lakini pia mkoa wenye msongamano mkubwa wa watu.

Eneo la Mkoa wa Magharibi nchini Kenya.
Mji mkuu wa Mkoa wa Magharibi wa Kenya ni Kakamega (click to enlarge map)
Wilaya nne za jadi za mkoa wa Magharibi, Kenya.

Ulipakana na Uganda na mikoa ya Kenya ya Nyanza na Bonde la Ufa.

Eneo lake lilikuwa km² 8,285 pekee na wakazi 3,569,400, hivyo ulikuwa na zaidi ya watu 400 kwa kila kilomita ya mraba.

Wakazi wa Magharibi ni hasa Abaluhya (Waluhya). Maadili ya Quakers ni maarufu sana hapa. Makao makuu yalikuwa Kakamega.

Mkoa ulienea kutoka vilima vya Bungoma mpakani wa Uganda hadi tambarare karibu na Ziwa Viktoria.

Mlima mkubwa wa pili wa Kenya, Mlima Elgon, uko ndani ya eneo hilo, kwenye mpaka wa Uganda. Msitu wa Kakamega ni kati ya misitu asilia ya mwisho wa Kenya.

Uti wa mgongo wa uchumi ni kilimo. Pamoja na kilimo cha kujikimu kuna pia mashamba makubwa ya chai na miwa.

Kilimo na maliasili ni msingi wa viwanda vikubwa kama vile kiwanda cha sukari cha Mumias au kiwanda cha karatasi cha Webuye. Hata hivyo idadi kubwa ya wakazi ni maskini na wanaume wengi wamekwenda Nairobi au kwenye hoteli za pwani kwa kazi ya ajira.

Jiografia

hariri

Mkoa wa Magharibi una maumbile mbalimbali ya mazingira, kuanzia vilima vya kaskazini mwa Bungoma hadi eneo tambarare linalopakana na Ziwa Victoria katika Wilaya ya Busia. Eneo la juu zaidi katika Mkoa wa Magharibi ni kilele cha Mlima Elgon, la chini zaidi ni mji wa Busia kwenye maji ya Ziwa Victoria.

Hali ya hewa

hariri

Hali ya hewa ni ya kitropiki, ikiwa na tofauti kutokana na kimo. Wilaya ya Kakamega huwa na joto na unyevu karibu mwaka mzima, ilhali wilaya ya Bungoma ni baridi kidogo lakini ina unyevu uo huo. Wilaya ya Busia ndio yenye joto zaidi, ilhali Wilaya ya Vihiga yenye vilima ndio baridi zaidi. Eneo zima hupata mvua kubwa mwaka wote, na mvua za masika katika miezi ya kwanza ya mwaka.

Uchumi

hariri

Kilimo ndiyo shughuli kuu ya kiuchumi katika mkoa huu.

Wilaya ya Bungoma ni eneo la sukari, ikiwa na mojawapo ya viwanda vya sukari kubwa nchini, pamoja na viwanda vidogovidogo kwa kusaga sukari. Mahindi pia yanalimwa kwa kujikimu kinyumbani, pamoja na mtama na mawele. Kilimo cha maziwa hufanyika sana, na vilevile ufugaji wa kuku. Kuna mtaji mdogo lakini muhimu wa kitalii, unaoegemea sherehe za tohara zinazofanyika kila baada ya miaka miwili.

Wilaya ya Kakamega ina mchanganyiko wa kilimo cha kujikimu na mazao ya fedha, huku ukuzaji wa miwa ukiwa kifua mbele mbele ya mazao mengine yanayokuzwa. Wilaya hii ina viwanda viwili vya sukari. Pia kuna mtaji muhimu wa utalii unaoegemea Msitu wa Kakamega.

Wilaya ya Busia hupokea mvua za mafuriko kutoka mto Nzoia, na shughuli ya kiuchumi iliyopewa kipa mbele ni uvuvi katika Ziwa Victoria. Kilimo cha kibiashara kiasi pia hufanyika, hasa miwa. Ukulima wa kujikimu wa mihogo umeenea sana.

Wilaya ya Vihiga ina mashamba makubwa ya chai, na ndio eneo la mashambani lenye watu wengi zaidi nchini Kenya. Uchimbaji mawe kwa ajili ya vifaa vya ujenzi ni shughuli muhimu katika wilaya hii yenye milima. Kilimo cha maziwa mojawapo ya shughuli zinazofanyika sana Vihiga.

Magharibi Kenya ina viwanda vingi vikubwa, vikiwemo vya sukari (viwanda 4). Kubwa zaidi kati ya hivi ni kile cha Mumias, chenye makao yake mjini Mumias, magharibi mwa Kakamega. Kiwanda hiki ndicho kinachotoa aina ya sukari maarufu zaidi nchini Kenya na ni mfano wa mafanikio ya kiuchumi. Pia katika Magharibi Kenya kuna kiwanda kikubwa zaidi cha karatasi Afrika (Pan Paper Mills kilichoko Webuye) na pamoja na viwanda vya kutengenezea kemikali. Hata hivyo, hali ya maisha kwa ujumla iko chini na huduma za kijamii kama maji ya bomba na umeme hazipatikani kwa wengi wa wakazi wa eneo hili.

Wilaya

hariri

Kulikuwa na wilaya nane mkoani:

Wilaya Makao makuu
Bungoma Bungoma
Busia Busia
Butere/Mumias Butere
Kakamega Kakamega
Lugari Lugari
Mlima Elgon Kapsokwony
Teso Malaba
Vihiga Vihiga

Wilaya baada ya 2007

hariri

Wilaya Kadhaa mpya ziliundwa mwaka wa 2007 nchini Kenya, pia katika eneo la Magharibi [1]

Wilaya Makao makuu
Bungoma Mashariki (Webuye) Webuye
Bungoma Kaskazini Kimilili
Bungoma Kusini Bungoma
Bungoma Magharibi (Sirisia) Chwele
Bunyala Budalangi
Busia Busia
Kisumu Butere Butere
Emuhaya Kima
Hamisi Hamisi
Kakamega Kaskazini (Malava) Malava
Kakamega Kusini Kakamega
Lugari Lumakanda
Mlima Elgon Kapsokwony
Mumias Mumias
Samia Funyala
Vihiga Mbale

Marejeo

hariri

0°30′N 34°35′E / 0.500°N 34.583°E / 0.500; 34.583