Mwaozi Tumbe (pia: Mwana Ozi Tumbe) ni jina la mwanamke maarufu katika historia ya pwani ya kusini ya Kenya.

Habari zake zimesimuliwa kwa zaidi ya karne tatu, hivyo hakuna uhakika kuhusu sehemu kadhaa za hadithi zinazosimuliwa.

Inaonekana alikuwa binti Guo Kuu Mwatumbe, kiongozi wa Wachifundi na mfalme wa mwisho wa mji wa Tumbe. Leo hii Tumbe ni eneo la maghofu karibu na Msambweni (Kaunti ya Kwale), lakini hadi karne ya 17 ilikuwa mahali muhimu kati ya miji ya Washirazi kwenye pwani ya Kenya na Tanzania na mji mkuu wa Wachifundi.

Kwenye mwanzo wa karne ya 17 Wavumba chini ya Mwana Kyambi Kyandi Ivoo walipasha utawala wao juu ya miji ya Washirazi wengine, na Tumbe pekee chini ya mfalme Mwatumbe iliendelea kutetea uhuru wake.

Mwatumbe alifariki bila mrithi wa kiume. Binti yake Mwaozi alitegemea kushika nafasi hiyo lakini Wachifundi walimkataa kutokana na jinsia yake. Hapo sehemu ya masimulizi inaeleza kwamba Mwaozi alifanya mapatano ya siri na Ivoo wa Vumba, eti amsaidie kukamata Tumbe na kuiingiza katika himaya yake lakini alipaswa kumpa cheo cha malkia.

Kufuatana na urithi Mwaozi alifaulu kwa kupiga mayowe mara kadhaa wakati wa usiku na kuita mji kwamba unashambuliwa. Baada ya hii kutokea mara kadhaa watu wa mji walidhani hana akili timamu. Lakini binti huyo alituma habari kwa maadui Wavumba wawe tayari usiku fulani. Katika usiku ule alipiga tena mayowe lakini hakuna aliyechukua silaha maana walifikiri ilikuwa kama usiku zilizotangulia. Hivyo Wavumba waliingia mjini wakashinda, Tumbe ilikuwa sehemu ya himaya ya Ivo.

Sasa Mwaozi alimkumbusha Ivo atimize upande wake wa mapatano na kumfanya malkia wa Tumbe. Lakini Ivo alimwogopa akizingatia jinsi binti huyo alivyowatendea ndugu zake, alimjibu aje kwake Vumba. Alipofika alimkamata akamfunga akampeleka kwenye kisiwa cha Kisite alipomwacha. Kwenye kisiwa hicho pasipo watu alikufa njaa.

Kutoka hapa kuna namna mbalimbali ya masimulizi hayo lakini kwa jumla yanasema mvua ilikwisha kwenye pwani ya Washirazi na watu walikuwa na shida kubwa. Hivyo walikwenda kutafuta mifupa ya Mwaozi wakaizika pale Bogoa kwenye kisiwa cha Wasini. Jiwe la kaburi lake linaonyeshwa hadi leo. Wenyeji wanaendelea kukutana kaburini kila mwaka na kufanya sala ya kuomba mvua.

Marejeo hariri

  • Martin Walsh: The legend of Mwaozi Tumbe: History, myth and cultural heritage on Wasini Island, katika “Kenya Past and Present Issue 37, 2008” (makala online here kupitia Research Gate)
  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mwaozi Tumbe kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.