Nabii Yeremia (kwa Kiebrania יִרְמְיָהוּ, Yirməyāhū) ni mmojawapo kati ya manabii wakubwa wa Israeli ambao Biblia inatunza kitabu cha ujumbe wao pamoja na habari za maisha yao.

Picha ya Yeremia ilivyochorwa na Michelangelo kwenye Cappella Sistina.

Alitoa unabii wake hasa chini ya wafalme Yehoyakimu na Sedekia wa Yuda, akitabiri maangamizi wa Yerusalemu na uhamisho wa umati wa watu wake. Kwa ajili hiyo aliteseka sana, hivi kwamba Kanisa limemuona kama mfano wa Yesu kama mtu wa mateso.

Pia alitabiri Agano Jipya la milele, ambalo likaja kufanyika katika Yesu Kristo, ambapo Mungu Baba Mwenyezi ataandika mioyoni mwa wana wa Israeli sheria yake, aweze kuwa Mungu wao nao wawe taifa lake.

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 1 Mei[1].

Maisha yake

hariri

Mtu mpole sana, aliitwa na Mungu akiwa bado kijana, akapewa kazi ngumu ya kutabiri maangamizi ya Yerusalemu viongozi wasipoacha siasa yao ili kumtegemea Mungu tu.

Habari zake zinapatikana katika kitabu chake, ingawa humo hazikupangwa kitarehe.

Toka mwanzo Yeremia alitaka kukataa wito wa unabii, na hata baadaye akafikia hatua ya kukata tamaa alipodhulumiwa. Lakini Mungu alimuita kwa mpango wa milele, Yeremia asiweze kukataa (15:10-21; 20:7-18).

Katika muda wa utume wake (626-585 hivi K.K.) kipindi kizuri ni kile tu ambacho mfalme Yosia alifanya urekebisho (622-609 K.K.).

Kipindi hicho mji mkuu wa Ashuru uliangamizwa alivyotabiri kwa furaha nabii Nahumu (612 hivi K.K.).

Lakini kisha kufa Yosia mambo yakaharibika haraka sana, ikambidi Yeremia awakaripie wafalme na wananchi wasifanye dini kisingizio cha kuendelea na maovu badala ya kutubu (7:1-15; 19:1-13).

Aliwakaripia vilevile manabii wa uongo waliotumainisha watu bure (20:1-6).

Ndipo alipoanza kupigwa, kufungwa na kuhukumiwa, akawa mfano wa Yesu, yeye ambaye peke yake katika Agano la Kale aliishi bila ya ndoa kwa agizo la Mungu; lakini hakuuawa (26:1-19).

Kwa hofu akajificha, ila hakuacha kutabiri maangamizi kwa maandishi kwa njia ya karani wake Baruku (36).

Basi, mfalmeNebukadreza II wa Babeli akazidi kuwa na nguvu: mwaka 602 K.K. akamtiisha mfalme Yehoyakimu wa Yuda, na mwaka 598 K.K. akazingira Yerusalemu na kuwahamishia Babeli mfalme Yekonia na viongozi wengi.

Hapo Yeremia akawaandikia wasikate tamaa ila wasitarajie kurudi upesi kwa kuwa watabaki uhamishoni miaka 70 (29:4-23).

Lakini katika mpango wa Mungu hao ndio wa kutegemewa, sio walioachwa Yerusalemu (24).

Nabukadreza alipohusuru mji huo mara ya pili, mfalme na viongozi wengine walikataa shauri la Yeremia la kusalimu amri, wakamfunga pabaya sana mpaka siku ya Yerusalemu kutekwa (37-38).

Kwa kawaida Yeremia alitabiri kinyume cha matazamio madanganyifu ya watu, lakini walipokata tamaa akawatuliza na kutabiri heri.

Kilele cha mafundisho yake ni kwamba Mungu atafunga na Israeli yote Agano Jipya ambalo litaandikwa mioyoni (31:31-34).

Baada ya Yerusalemu kuteketezwa (587 K.K.) Yeremia alichagua kubaki nchini pamoja na mafukara badala ya kuhamia Babeli (39:8-40:6), ila ukatokea uasi akalazimishwa na Waisraeli wenzake kuwafuata Misri: huko akawaonya wasifuate Upagani lakini wakakataa tena kumsikiliza (42-44).

Sala yake (Yer 15:16)

hariri

Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu, maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Marejeo

hariri

Marejeo mengine

hariri
  • Ackroyd, Peter R. (1968). Exile and Restoration: A Study of Hebrew Thought in the Sixth Century BC. Philadelphia: Westminster Press.
  • Bright, John (1965). The Anchor Bible: Jeremiah (toleo la 2nd). New York: Doubleday.
  • Meyer, F.B. (1980). Jeremiah, priest and prophet (toleo la Revised). Fort Washington, PA: Christian Literature Crusade. ISBN 0-87508-355-2.
  • Perdue, Leo G.; Kovacs, Brian W., whr. (1984). A Prophet to the nations : essays in Jeremiah studies. Winona Lake, IN: Eisenbrauns. ISBN 0-931464-20-X.
  • Rosenberg, Joel (1987). "Jeremiah and Ezekiel". Katika Alter, Robert; Kermode, Frank (whr.). The literary guide to the Bible. Cambridge, MA: Harvard University Press. ISBN 0-674-87530-3.

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nabii Yeremia kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.