Mashirika ya ombaomba

(Elekezwa kutoka Ombaomba)

Mashirika ya ombaomba ni aina za utawa zinazosisitiza ufukara na utume kando ya wajibu mkuu wa sala.

Dominiko Guzman
Fransisko wa Asizi

Historia

hariri

Kama kawaida bidii kwa urekebisho wa Kanisa Katoliki zilizofanyika hasa katika karne ya 11 na karne ya 12 zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei hawakuridhika.

Pia hija na vita vya msalaba vilifanya wengi wajionee nchi ya Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake. Ndiyo sababu walistawisha mifumo mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya Kanisa la mwanzoni.

Dhidi ya mwenendo wa mapadri na wamonaki, walisisitiza ufukara na unyofu hata wengi walifikia hatua ya kuliasi Kanisa Katoliki. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu kadhaa waukinai.

Juu ya misingi hiyo katika karne XIII yalianzishwa mashirika mbalimbali (hasa Wafransisko na Wadominiko, lakini pia Waaugustino, Wakarmeli na Watumishi wa Maria) yaliyoitwa ya ombaomba kwa jinsi yalivyokazia ufukara.

Dominiko Guzman

hariri

Dominiko Guzman (1170-1221) akiwa padri aliguswa na uenezi wa uzushi akajitahidi kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu wote kama mhubiri halisi wa Injili alishika ufukara wa Yesu na mitume wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya kuchukua chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya kazi ya kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa lengo hilo utawa wake ulipunguza miundo ya kimonaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya kusoma na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia ukweli ambao wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha. Ndio utume unaolingana zaidi na maisha ya sala na kusoma.

Fransisko wa Asizi

hariri

Hata kuliko yeye, rafiki yake, Fransisko wa Asizi (1181-1226) alishikwa na hamu ya kulingana na Yesu kwa kufuata nyayo zake inavyofundishwa na Injili. Alifanya vilevile kazi ya kuhubiri, lakini bila ya kuzingatia elimuwala kubishana na wazushi, bali kwa kuelekeza njia ya toba kwanza kwa matendo halafu kwa maneno machache na manyofu. Kwa ajili ya Yesu alijinyima hata upweke alioupendelea, akawakaribia watu hasa wale wadogo zaidi.

Wafuasi wake hawakujifunga kuishi daima mahali fulani na watu walewale, bali walifungamana na jamaa ya kimataifa ambayo mkuu wake aweze kuwatuma popote. Hivyo iliwabidi wawe tayari kukabili mazingira yoyote na kushirikiana na ndugu mbalimbali. Tena udugu haukuishia shirikani bali ulitakiwa kuenea kwa watu na viumbe vyote. Kutokana na upya wa mtindo huo wa maisha, hata miundo yake ilipaswa kuwa mipya iweze kudumisha umoja wao.

Ufransisko ulilingana kikamilifu na madai ya urekebisho ya walei, pia uliwapendeza viongozi wa Kanisa walioona ulivyowarudishia utiifu wa waamini: hivyo ulienea kasi ajabu, hata kati ya wanawake na watu wa ndoa.

Wanawake

hariri

Watawa wa kike hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa hao ndugu wadogo. Klara wa Asizi (1193-1253), “mche mdogo” wa Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa. Tapo hilo ni maarufu kwa marekebisho yaliyofuatana hadi leo kuhusu ufukara.

Tangu karne XII wanawake wengine pia walichangia sana ustawi wa utawa, wa maisha ya Kiroho na wa Kanisa kwa jumla hata kwa maandishi yao. Kati yao Katerina wa Siena (1347-1380), wa utawa wa tatu wa Mt. Dominiko, ametangazwa kuwa mwalimu wa Kanisa.

Viungo vya nje

hariri