Unyofu (kutoka kitenzi kunyoka) ni adili linalojumlisha usahili na usemakweli. Pasipo usahili busara inaelekea kutumia uongo na kugeuka ujanja.

Katika Ukristo

hariri

Kadiri ya Yesu, busara inatakiwa kuendana na adili hilo (Math 10:16) kwa maana alipowapeleka mitume wake kama kondoo kati ya mbwamwitu aliwahimiza wawe na busara hasa kwa waovu, wasije wakadanganywa nao, na wawe na usahili hasa kwao wenyewe na kwa Mungu: hapo yeye kwa kipaji cha shauri atawaangazia busara katika nafasi ngumu na vipingamizi vikubwa. Ndiyo sababu aliwatabiria mara kwamba mbele ya watesi “si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu” (Math 10:20).

“Huyo mwenye haki, aliye mtimilifu, amekuwa ni kicheko!” (Ayu 12:4) kwa wajanja ambao wanaona usahili wake kuwa ujinga na upumbavu tu. Pengine usahili unaendana kweli na ujinga, lakini wenyewe ni jambo bora ambalo, tukitaka kulithamini ipasavyo (pamoja na ukweli na unyofu unaodumishwa nalo), tunapaswa kuzingatia kwanza kasoro zilizo kinyume chake.

Vilema vilivyo kinyume cha usahili

hariri

“Usahili unaitwa hivyo kwa kupingana na undumakuwili ambao mtu moyoni ana kitu fulani lakini kwa nje anaonyesha kingine. Hivyo usahili unahusiana na adili la ukweli… tofauti ni hii tu, kwamba ukweli unaitwa hivyo kadiri ishara zinavyolingana na kinachoashiriwa; kumbe usahili unaitwa hivyo kadiri usivyolenga mambo mbalimbali” (Thoma wa Akwino). Kwa hiyo usahili unahusiana na adili linalotia ukweli katika maneno, matendo na mwenendo, kwa kuwa unapingana na undumakuwili wa mtu kutaka pesa za wenzake kwa kujisingizia nia ya kuwatumikia; au kutamani utawala na heshima kwa kujisingizia nia ya kujenga nchi. Undumakuwili, unaomfanya aonyeshe sura mbalimbali kadiri ya watu anaohusiana nao, unasababisha uongo, udanganyifu wa kutaka kuonekana tofauti na alivyo, unafiki ambao mtu anaonyesha adili asilonalo, tena majigambo na dhihaka ambazo anawacheka watu ili kujikuza juu yao.

Ukweli na maisha ya kiroho

hariri

Adili la ukweli linategemea haki na kumfanya mtu aseme na kutenda daima kadiri ya ukweli. Si kwamba tunapaswa kumuambia yeyote ukweli wote, kuropoka maneno pasipofaa kwa kudai ni ari, kumbe ni utovu wa heshima. Bali tunapaswa kukwepa neno lolote kinyume cha ukweli tunaloshawishiwa kulitumia katika shida, ingawa kweli kadhaa ni vema kuzificha. Kama tumedanganya, tujishtaki kwa unyofu, badala ya kujitetea kwa visingizio ambavyo polepole vinafuta uaminifu na kufanya ushuhuda wetu, unaohitajika katika jamii, usiweze kukubalika.

Pengine ni vigumu kutunza siri tuliyokabidhiwa bila kuongopa. Lakini mara nyingi ni kosa letu tukiulizwa maswali yasiyofaa, kwa sababu tungejikusanya na kukaa kimya zaidi tungeulizwa kwa nadra tu. Hata hivyo, ikiwa Mkristo kwa kawaida ni msikivu kwa minong’ono ya kutoka juu, katika nafasi hizo ngumu Roho Mtakatifu atamuangazia la kujibu au la kuuliza, kama alivyowafanyia Wakristo waliopelekwa mahakamani kwa ajili ya imani. Wataalamu wa maadilidini wanatakiwa kukumbuka ukweli huo muhimu, badala ya kuruhusu maneno yanayolingana na uongo wa wazi. Ni afadhali kukiri kosa la uongo kuliko kupotosha maana ya uongo ili usilaumiwe inapotakiwa. Ni muhimu tudumishe unyofu aliotufundisha Bwana, “Maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu” (Math 5:37). Aliwaambia hivyo watu waliotaka kuthibitisha ushuhuda wao kwa kula kiapo bure, wakiingia hatari ya kuapa kwa uongo; inatosha tuzoee kusema ukweli daima ili maneno yetu yaaminike.

“Watu wanaojitangaza bora kuliko walivyo wanachukiza wenzao huku wakitaka kuwapita. Kinyume chake, wasiodhihirisha mema yote yaliyomo ndani mwao wanapendeza kwa utaratibu na kiasi” (Aristoteli). Adili la ukweli linatuelekeza kunyamazia sifa zetu: kufanya hivyo si kudhuru ukweli kwa kuwa kunyamaza si kukanusha. “Kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu” (2Kor 12:6).

Tukitekeleza adili hilo kwa maneno, matendo na mwenendo wetu wote, tutatia ukweli katika maisha yetu. Hapo Mungu, aliye ukweli mkuu, atatuinamia kwa minong’ono yake inayokuwa mwanzo wa sala ya hali ya juu. Kutumia uongo ni kuupa kisogo ukweli na kuja kukosa mianga ya kipaji cha hekima. Kuishi mfululizo katika ukweli ni kujiandaa kuipokea mianga hiyo inayotufanya tupenye na kuonja ukweli wa Mungu ambao siku moja tutauona wazi.

Usahili wa hali ya juu ni mfano wa ule wa Mungu

hariri

Lile tawi la ukweli linaloitwa usahili linatuandaa zaidi tena kumiminiwa sala kwa kuwa haupingani na undumakuwili tu, bali pia na changamano lolote la bure, na yale yote ambayo yanaiga mitindo au kuchafuliwa na nia ya kuonekana namna fulani (k.mf. wepesi wa kuguswa moyo unaojidai kuwa upendo).

Mtazamo wa mtoto ni sahili, una lengo moja tu. Kwa maana hiyo, “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru” (Math 6:22). Yaani nia yetu ikiwa nyofu na sahili, maisha yetu yote yatakuwa na umoja wa ndani, ukweli, uangavu, badala ya kugawanyika kama yale ya wanaotaka kutumikia mabwana wawili kwa pamoja. Katika ulimwengu uliojaa machangamano ya bure, sura bandia na udanganyifu wa kila aina, tunahisi kuwa adili la usahili, yaani uaminifu kamili, linaakisi mwanga wa sifa mojawapo ya Mungu.

Usahili wa Mungu ni ule wa Roho tupu aliye ukweli na wema mkuu. Ndani mwake hamna mifuatano ya mawazo, bali daima wazo lilelile lenye kweli zote ndani yake. Usahili wa akili yake ni ule wa mtazamo safi kabisa ambao hauchanganyikani na udanganyifu wala ujinga wowote, bali unaenea kutoka juu kwenye kweli zote usibadilike kamwe. Usahili wa utashi wake ni ule wa nia safi kabisa inayoratibu vizuri ajabu mambo yote, hata kuacha mabaya yatokee ili mema makubwa zaidi yatokane nayo. Kinachopendeza zaidi katika usahili wa Mungu ni kwamba unaunganisha sifa ambazo zinaonekana kupingana, kumbe ndani mwake ni kitu kimoja bila kuangamizana. Usahili huo wa ajabu unarudisha mwanga wake katika tabasamu ya mtoto na katika macho manyofu ya watakatifu, yanayoshinda busara ya ulimwengu.

Tunajidanganya tunapodhani usahili ni kusema lolote linalotujia, halafu kusema kinyume chake hali ikibadilika au mtu akiacha kutupendeza: huo ni ugeugeu tu unaozaa uongo. Kumbe usahili wa watakatifu ni ule wa hekima isiyobadilika na wa upendo safi na wa nguvu kuliko hisi za moyo. Usahili ni nia nyofu ya kumpenda Mungu ambayo ishinde mguso wowote na isisimame kujitafutia bure aina nyingi za ibada hata kusahau lengo pekee. Ndio busara bora inayolenga shabaha moja kwa moja bila kujishughulisha na matendo ya wengine.

Aliyekamilika ni mtu sahili ambaye anapima yote kwa mwanga wa Mungu (si alivyoguswa mara) na anayataka kwa ajili ya Mungu tu. Anayepima yote kwa jinsi yanavyompendeza anahangaishwa na lolote, kumbe aliye sahili anadumisha amani ya ndani kwa hekima yake na upendo wake. Tofauti na ujinga na upumbavu, usahili huo wa hali ya juu unapatana na busara ya Kikristo inayozingatia pia vipengele vidogo vya matendo yetu na matokeo yake ya mbali.

Yesu alitokeza vizuri ajabu usahili wa Mungu: ndani mwake vilipatana ukali mtakatifu wa haki dhidi ya wanafiki na huruma isiyo na mipaka kwa wale wote ambao ndiye mchungaji wao mwema. Ndani mwake vilipatana kwa usahili kujishusha hadi vilindini na kujiheshimu kwa hali ya juu. Kwa miaka thelathini aliishi kama fundi tu, akasema amekuja kutumikia, akawaosha mitume miguu, akapokea dharau za mateso kisha kumuomba Baba kwa usahili amuepushe. Kwa usahili huohuo alijishuhudia mbele ya Pilato kuwa mfalme, akamrudishia Baba roho yake akitokeza ukuu uliomfanya akida akiri, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu” (Math 27:54).

Usahili huo wa hali ya juu unaandaa hata wasio na elimu waelewe kwa ndani mambo ya Mungu: “Tafakarini habari za Bwana kwa moyo mwema, na kumtafuta katika unyofu wa moyo” (Hek 1:1). “Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake” (Mith 19:1). “Watiini… si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana” (Kol 3:22). “Kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikra zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo” (2Kor 11:3). Tunapaswa kuutunza usahili huo kwa Mungu, kwa viongozi wetu, kwetu wenyewe: ndio ukweli wa maisha.

Usahili huo unawawezesha watu safi kupenya ukuu wa Mungu, njia za maongozi yake na mafumbo yasiyochunguzika ambayo yanawakwaza wengine. Kwa walio sahili hayo ni sahili, ingawa yanafunikwa na giza, kwa sababu katika mambo ya Mungu yale yaliyo sahili zaidi (k.mf. Baba Yetu) ndiyo ya juu na ya dhati zaidi. Tunasahau ukweli huo kwa sababu katika malimwengu ni kinyume: yakiwa mchanganyiko mkubwa wa mema na mabaya yanahitaji upambanuzi, hivyo anayetaka kuwa sahili katika hayo hayaelewi, anabaki juujuu kama mjinga. Kumbe katika mambo ya Mungu usahili unaendana na udhati na ukuu, kwa kuwa yaliyo ya juu zaidi katika Mungu na yaliyo ya dhati zaidi katika mioyo yetu ni usahili mtupu.

Nyakati hizi Bwana ametujalia Teresa wa Mtoto Yesu, kielelezo cha usahili unaozama katika mafumbo. “Badala ya kufanana na watu wale wazuri ambao tangu utotoni walitimiza aina zote za kujitesa, mimi niliridhika tu na kupinga matakwa yangu, kuzuia neno lolote la kurudishia chukizo, kutoa huduma ndogondogo pasipo kuzitia maanani, na mengine mengi ya namna hiyo… Katika njia yangu ndogo mambo yote ni ya kawaida kabisa; ni lazima yale yote ninayoyafanya, watu wadogo waweze kuyafanya vilevile … Jinsi ilivyo rahisi kumpendeza Yesu na kuvuta moyo wake kwetu! Inatosha tumpende pasipo kujiinamia wala kutafiti mno kasoro zetu. Hivyo, inaponitokea kuiangukia mojawapo nainuka mara. Kumuangalia Yesu na kukiri unyonge wangu unarekebisha kila kitu. Mwenyewe alijiita ‘ua la uwandani’ (Wim 2:1) ili kutuonyesha tu anavyopendelea usahili”. Tunaona wazi lilivyotimia ndani mwake neno aliloliandika, “Mara nyingi Bwana anaridhika kuwajalia hekima walio wadogo zaidi”. Hao wanaona muungano na Mungu unadai nini ili udumu imara katika nafasi ambazo mara nyingi hazitarajiwi bali ni za tabu.

Tunapoeleza maisha ya Kiroho, ni lazima tusisitize maadili kama hilo kwa jinsi yanavyochangia namna ya kuwaza na ya kutenda. Baadaye mafundisho juu ya sala ya kumiminiwa yataonekana kuwa matokeo ya yote yaliyosemwa kuhusu ustawi wa maadili na wa vipaji saba katika watu ambao kweli wamejikana na kuambatana na Mungu karibu mfululizo.