Abd al Aziz al-Amawi

Abd al-Aziz al-Amawi (kwa Kiarabu: عبد العزيز الأموي ;c 1838-1896) alikuwa mtaalamu Mwislamu aliyefuata dhehebu la Washafi'i na mafundisho ya Ash'ari. Alikuwa shehe wa Wasufi wa jumuiya ya Qadiriya alikoanzisha tawi lake[1]. Alikuwa mshauri wa masultani mbalimbali wa Zanzibar.

Maisha

hariri

Al-Amawi alizaliwa mjini Barawa, Somalia, aliposoma chini ya wasomi mashuhuri, kama vile Sayyid Abu Bakr al-Mihdar al-Hadrami, Hajj 'Ali b. 'Abd al-Rahman, na msomi kutoka Afrika Kaskazini Sayyid Ahmad al-Maghribi. Kijana Al-Amawi aliondoka Barawa kwenda Zanzibar ili kusoma chini ya Muhyi al-Din al-Qahtani, aliyekuwa kadhi mkuu Mshafi'i wa Zanzibar. Al-Qahtani alimtambulisha kwa sultani wa Zanzibar, Sayyid Sa'id bin Sultan.

Mnamo 1854, al-Amawi, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na sita, aliteuliwa na Sultani kama kadhi (jaji) wa Kilwa. [2] Baada ya muda mfupi Al-Amawi alihamishiwa Zanzibar, ambapo alihudumu hadi 1891, wakati mtoto wake Burhan alipochukua nafasi yake. Al-Amawi aliandika juu ya theolojia, sheria, usufi, balagha na historia. Alianzisha kamusi ya Kiswahili-Kiarabu isiyokamilika.

Alihudumu pia kama mshauri wa kisiasa, balozi, na mwanadiplomasia huko Somalia, visiwa vya Komoro, maeneo ya mto Rovuma, na maeneo mengine kwenye Bara la Afrika kwa niaba ya masultani wawili wa Zanzibar, Sayyid Majid (utawala 1856-1870) na Sayyid Barghash (utawala 1870-1888).

Abdallah Salih Farsy aliandika kwamba Al-Amawi alikuwa kama waziri mkuu wakati wa utawala wa Sayyid Khalifa (utawala 1888-1890). [3]

Farsy aliamini maandishi yote ya Amawi yamepotea, lakini kuna takriban kurasa 2000 zilizohifadhiwa, ambazo zote hazikuchapishwa, zikipatikana kwenye hifadhi za nyaraka Dar es Salaam (nakala zake zinaweza kupatikana katika hifadhi za nyaraka za kitaifa za Zanzibar) na kwenye maktaba ya Sayyid Muhammad Al Bū Sa'idi huko Oman. Ni pamoja na sehemu za shajara yake kutoka safari mbili kati ya sita kwenda Rovuma, historia ya nasaba ya Bū Sa'idi, matini za Wasufi na kuhusu ibada, kitabu kuhusu balagha na shairi la kitheolojia kufuatia mafundisho ya shule ya Ash'ari kwenye Uislamu wa Kisunni.

Al-Amawi alipatana vema na sultani na Waomani waliokuwa wafuasi wa Uislamu wa Kiibadi, hata hivyo alifaulu kushawishi Waibadi wengine kuhamia Usunni, hatua iliyomkasirisha Sayyid Barghash.

Wakati wake Wakristo Waanglikana chini ya askofu Edward Steere walianza kuhubiri imani yao, na Amawi alikuwa kati ya mashehe Waislamu wa Zanzibar waliojisomea Biblia ili waweze kujibu[4]. Hata hivyo, inaonekana walikuwa na uhusiano mzuri na askofu Steere. Al-Amawi alimsaidia Steere kutafsiri Zaburi na Injili ya Luka kwa Kiswahili.[5] [6] Steere aliandika kwamba alikutana kila wiki na mashehe Waislamu nyumbani kwake na kujadili mitazamo yao ya imani.

Marejeo

hariri
  1. Anne Bang, Sufis and Scholars of the Sea: Family Networks in East Africa, 1860-1925, Routledge 2004, ISBN 978-0415317634, uk.95, online hapa
  2. pg 538 – Notes on Some Members of the Learned Classes of Zanzibar and East Africa in the Nineteenth Century, by B. G. Martin – African Historical Studies, 1971
  3. Abdallah Salih Farsy, The Shafi'i Ulama of East Africa, ca. 1830–1970: A Hagiographic Account, trans. and ed. Randall L. Pouwels (Madison, WI: University of Wisconsin African Studies Program, 1989), 46–48.
  4. Farsy, 43–44.
  5. Edward Steere, A Handbook of theSwahili Language as Spoken at Zanzibar (London: Society for the Promotionof Christian Knowledge, 1884), vi–vii.
  6. Aloo Osotsi Mojola, “The Swahili Bible in EastAfrica from 1844 to 1996: A brief survey with special reference to Tanzania,” in The Bible in Africa: Transactions, Trajectories and Trends, ed.Gerald O. West and Musa W. Dube (Leiden: Brill, 2001), 514.