Birgita wa Uswidi

(Elekezwa kutoka Birgita wa Sweden)

Birgita wa Uswidi (Finsta, Uswidi, 3 Juni 1303Roma, Italia, 23 Julai 1373) alikuwa Mkristo wa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko, halafu mwanzilishi wa shirika la Mwokozi Mtakatifu.

Brigita akiwa amevaa kanzu na taji la shirika lake.

Alitangazwa mtakatifu na Papa Bonifasi IX mwaka 1391, halafu msimamizi mmojawapo wa Ulaya na Papa Yohane Paulo II mwaka 1999.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 23 Julai[1].

Maisha ya awali

hariri

Birgita alizaliwa huko Finsta, katika mkoa wa Uppland (Uswidi), katika familia ya watemi.

Sehemu ya kwanza ya maisha yake ni ya mke mwenye watoto 8, ambao wa pili kati yao anaheshimiwa pia kama mtakatifu Katerina wa Uswidi. Kwa mifano na maneno yake alimhimiza mume wake, sharifu Ulf Gudmarsson, kuishi maisha ya imani ya dhati; pamoja naye alisoma Biblia, alianzisha hospitali na kuhudumia maskini.

Kutokana na kipaji chake kama mlezi aliitwa kwenye ikulu huko Stockholm, na hatimaye alifanya hija huko Santiago wa Compostela (Hispania).

Baada ya kufiwa

hariri

Kisha kufiwa mume wake mwaka 1344 alijisikia kuhama nchi yake ili kuanza utume mpya akahamia Roma (1349).

Baada ya kuhiji mahali pengi Italia, kati ya miaka 1371 na 1372 alitembelea Nchi Takatifu, alipojionea mahali alipoishi Yesu.

Alisema kuwa huko Yerusalemu alipewa ujumbe wa Bikira Maria wa kurudi Ulaya.

Huko aliwatabiria matukio Mapapa na wafalme na kuwaonya vikali hata kwa maandishi kuhusu urekebisho wa maadili ya Wakristo wote, kuanzia Papa mwenyewe, akidai anawasiliana na Yesu Kristo[2].

Kutokana na mafumbo hayo alitunga sala 15 zilizoenea sana hadi leo.

Mojawapo kati ya Sala 15 alizozitunga

hariri

Usifiwe, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kuwahi kutabiri kifo chako, kwa kugeuza kwa namna ya ajabu, katika karamu ya mwisho, mkate wa kawaida uwe mwili wako mtukufu, kwa kuwagawia mitume kwa upendo kama ukumbusho wa mateso yako mastahivu, kwa kuwaosha miguu kwa mikono yako mitakatifu na azizi, ukionyesha hivyo ukuu usio na mipaka wa unyenyekevu wako.

Heshima kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kutoka jasho la damu katika mwili wako usio na kosa kwa hofu ya mateso na kifo, na kwa kutekeleza hata hivyo ukombozi wetu uliotamani kuutimiza, ukionyesha hivyo wazi upendo wako kwa binadamu.

Usifiwe, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kupelekwa kwa Kayafa na kuruhusu kwa unyenyekevu wako uhukumiwe na Pilato, wewe uliye hakimu wa wote.

Utukufu kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kudhihakiwa pale ambapo, kisha kuvikwa nguo ya zambarau, ulitiwa taji la miba mikali sana, na kwa kuvumilia kwa subira isiyo na mipaka kwamba uso wako mtukufu ujae mate, macho yako yafunikwe, mashavu yako yapigwe kwa nguvu na mikono ya kikafiri ya watu waovu.

Sifa kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kuruhusu kwa uvumilivu mkubwa ufungwe kwenye nguzo, upigwe mijeledi kinyama, upelekwe mahakamani kwa Pilato umejaa damu, uonekane kama mwanakondoo asiye na kosa anayepelekwa machinjoni.

Heshima kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kukubali kuhukumiwa katika mwili wako mtakatifu, uliojaa tayari damu, ufe msalabani; kwa kubeba kwa uchungu msalaba juu ya mabega yako matakatifu, na kwa kutaka kupigiliwa misumari katika mbao za adhabu, kisha kuburutwa kikatili hadi mahali pa mateso na kuvuliwa nguo zako.

Heshima kwako, Bwana Yesu Kristo, kwa kuelekeza kwa unyenyekevu, kati ya mateso hayo, macho yako yaliyojaa upendo na wema kwa Mama yako mstahivu sana, ambaye hajawahi kupatwa na dhambi wala kukubali kosa dogo namna gani, na kwa kumfariji ukimkabidhi kwa ulinzi mwaminifu wa mwanafunzi wako.

Uhimidiwe milele, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kuwapa wakosefu wote, wakati wa kihoro chako, tumaini la msamaha ulipomuahidia kwa huruma utukufu wa paradiso mhalifu aliyekukimbilia.

Sifa ya milele kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kila saa uliyovumilia msalabani kwa ajili yetu wakosefu machungu na mateso makubwa kabisa; kwa kuwa uchungu mkali sana wa majeraha yako ulikuwa ukipenya vibaya mno roho yako yenye heri na kuchoma kikatili moyo wako mtakatifu sana, mpaka pale ambapo, moyo ukishindwa kazi, ulitoa kwa heri roho yako na, kisha kuinamisha kichwa, uliikabidhi kwa unyenyekevu wote mikononi mwa Mungu Baba, ukabaki mfu, ukiwa na mwili baridi.

Usifiwe, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kukomboa roho za watu kwa damu yako azizi na kwa kifo chako kitakatifu sana, na kwa kuzirudisha kwa huruma katika uzima wa milele toka uhamishoni.

Usifiwe, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kukubali mkuki ukuchome ubavu na moyo kwa wokovu wetu, na kwa damu azizi na maji vilivyobubujika kutoka ubavu huo kwa ukombozi wetu.

Utukufu kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kutaka mwili wako mbarikiwa ushushwe toka msalabani kwa mikono ya marafiki wako, ukabidhiwe mikononi mwa Mama mwenye huzuni na kuvikwa naye, halafu ufungwe katika kaburi na kulindwa na askari.

Heshima ya milele kwako, Bwana wangu Yesu Kristo, kwa kufufuka kutoka wafu siku ya tatu na kwa kukutana hai na wale uliowachagua; kwa kupaa mbinguni, siku arubaini baadaye, ukitazamwa na wengi na kwa kutawaza huko juu kwa heshima marafiki wako uliowatoa kuzimu.

Shangwe na sifa ya milele kwako, Bwana Yesu Kristo, kwa kumtuma Roho Mtakatifu mioyoni mwa wanafunzi na kwa kushirikisha roho zao upendo mkuu wa Kimungu.

Uhimidiwe, usifiwe na kutukuzwa milele, Bwana wangu Yesu, uliyeketi katika kiti che enzi kwenye ufalme wako wa mbinguni, katika utukufu wa enzi yako, mwenye mwili hai pamoja na viungo vyako vitakatifu vyote, ulivyovitwaa kutoka mwilini mwa Bikira.

Hivyo utakuja siku ya hukumu uhukumu roho za wote walio hai na waliokufa: wewe unayeishi na kutawala pamoja na Baba na Roho Mtakatifu daima na milele. Amina.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri

Marejeo

hariri
  • Duffy, Eamon (1992). The stripping of the altars: Traditional religion in England, c.1400 - c.1580. New Haven: Yale University Press. ISBN 978-0-300-05342-5
  • Schiller, Gertrud; Seligman, Janet (1971). Iconography of Christian Art, Vol. I: Christ's incarnation, childhood, baptism, temptation, transfiguration, works and miracles, (English trans from German). London: Lund Humphries. OCLC 59999963

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.