Ngamia
Ngamia nundu-moja (Camelus dromedarius)
Ngamia nundu-moja
(Camelus dromedarius)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Artiodactyla (Wanyama wenye vidole viwili au vinne mguuni)
Nusuoda: Tylopoda (Wanyama wenye miguu inayovimba)
Familia: Camelidae (Wanyama walio na mnasaba na ngamia)
J. E. Gray, 1821
Jenasi: Camelus (Ngamia)
Linnaeus, 1758
Ngazi za chini

Spishi 2:

C. bactrianus Linnaeus, 1758
C. dromedarius Linnaeus, 1758

Ngamia ni wanyama wakubwa wa jenasi Camelus katika familia Camelidae inayowajumlisha pamoja na lama na vikunya wa Amerika Kusini.

Spishi

Makazi

Spishi zote mbili wamezoea kuishi katika mazingira yabisi kama jangwa au nusu jangwa.

Ngamia nundu-moja anapatikana katika Uarabuni, Mashariki ya Kati hadi Pakistani, Afrika ya Kaskazini, Somalia na kaskazini ya Kenya. Katika karne ya 19 walipelekwa Australia walipozoea haraka; kwa sasa takribani ngamia pori 700,000 wako kule. Spishi hii inavumilia joto kali lakini pia baridi za usiku kwenye Sahara. Anaweza kubadilisha halijoto ya mwili wake kati ya sentigredi 34 na 41 kulingana na mazingira.

Ngamia wa Asia yuko katika kanda inayoanzia Anatolia hadi Manchuria kaskazini mwa China. Amezoea zaidi baridi ya Asia ya Kati; wakati wa majira barafu halijoto ya mazingira inafikia -30°C. Joto kali inampa matatizo kidogo na kumchelewesha.

Spishi zote mbili zinakutana katika nchi kadhaa, kuanzia Uturuki, Uajemi, Afghanistan hadi Pakistani.

Mwili

Umbile lao limelingana na mazingira ya jangwani. Miguu ni mipana na kuzuia wasizame chini kwenye mchanga. Nywele ni ndefu, hivyo zinakinga dhidi ya joto na baridi.

Nundu ni mahali pa stoo ya akiba ya mafuta; kama ngamia anapitia mahali pasipo chakula anatumia mafuta kwa nishati ya mwilini. Hahitaji kula kwa kipindi hadi siku 30.

Wanaweza kushika lita 100–150 mwilini na kuendelea jangwani bila kunywa maji kwa wiki mbili. Penye majani mabichi ya kutosha, na kama joto si kali mno, ngamia anaweza kuendelea bila kunywa kwa wiki kadhaa.

Shingo ni ndefu kwa sababu kwa chakula anapendelea majani ya miti na vichaka.

Maisha

 
Ngamia wa Asia (C. bactrianus) ana nundu mbili

Ngamia ni wanyama wa kijamii na kwa asili huishi katika makundi ya dume mmoja na majike kadhaa. Siku hizi kuna ngamia wa Asia mamia kadhaa kwenye pori ambao ni mabaki ya ngamia pori wa zamani. Wako China na Mongolia.

Ngamia nundu-moja si wanyama wa pori asilia tena; inaaminiwa walitokea Uarabuni. Lakini kuna wanyama waliotoroka huko Australia na Amerika wanaoishi peke yao, hawafugwi.

Ngamia na binadamu

 
Binadamu akiongozana na ngamia

Ngamia wamefugwa na binadamu tangu miaka 5,000–6,000 iliyopita. Leo hii mifugo hao ni takriban milioni 19 na idadi kubwa, yaani milioni 14, wako Afrika, milioni 7 pekee nchini Somalia na milioni 3.3 nchini Sudan.

Watu hufuga ngamia kwa kubeba watu na mizigo. Nywele zao ni aina ya sufu inayotumiwa kutengenezea mashuka, mahema na pia vitambaa vya nguo. Wanachinjwa kwa nyama yao.

Ngamia hukamuliwa pia kama ng'ombe. Katika nchi yabisi kiasi cha maziwa yao yanalingana na ya ng'ombe.

Katika miaka ya nyuma Wamasai wa Kenya na pia Tanzania wameanza kufuga ngamia baada ya kuona ya kwamba ng'ombe zao walikufa wakati wa ukame lakini ngamia waliendelea kuishi na kutoa maziwa.

Ngamia anachukua chakula chake kwenye mti wenye mizizi mirefu kushinda manyasi yanayoliwa na ng'ombe. Kwa sababu hiyo manyasi hukauka haraka wakati wa ukame kuliko majani ya miti.

Katika Biblia

Katika mazingira ambako Biblia iliandikwa, ngamia alikuwa mnyama mkubwa kuliko wote wa nchi kavu. Ndiyo sababu alitumika katika methali mbalimbali kwa kusisitiza jambo.

Kwa mfano, Yesu alisema, "Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu la sindano kuliko tajiri kuingia mbinguni" (Mk 10:23-27).

Picha

Tanbihi

Marejeo

  • Ramet, J. P. (2011). The technology of making cheese from camel milk (Camelus dromedarius). FAO Animal Production and Health Paper. Rome: Food and Agriculture Organization of the United Nations. ISBN 92-5-103154-1. ISSN 0254-6019. OCLC 476039542. Iliwekwa mnamo 6 Desemba 2012.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Vannithone, S.; Davidson, A. (1999). "Camel". The Oxford companion to food. Oxford Oxfordshire: Oxford University Press. uk. 127. ISBN 0-19-211579-0.
  • Camels and Camel Milk. Report Issued by FAO, United Nations. (1982)
  • Wilson, R.T. (1984). The camel. New York: Longman. ISBN 0-582-77512-4.
  • Yagil, R. (1982). Camels and Camel Milk. FAO Animal Production and Health Paper. Juz. la 26. Rome: Food And Agriculture Organization Of The United Nations. ISBN 92-5-101169-9. ISSN 0254-6019.
  • Gilchrist, W. (1851). A Practical Treatise on the Treatment of the Diseases of the Elephant, Camel & Horned Cattle: with instructions for improving their efficiency; also, a description of the medicines used in the treatment of their diseases; and a general outline of their anatomy'. Calcutta: Military Orphan Press.

Viungo vya nje

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Ili kupata maelezo kuhusu masanduku ya uanapwa ya spishi angalia: Wikipedia:WikiProject Mammals/Article templates/doc.