John Wesley (17031791) alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kanisa la Kimethodisti. Alikuwa mchungaji wa Kianglikana na mwanatheolojia. Alikuwa kati ya viongozi wa kwanza katika harakati ya Wamethodisti.

John Wesley

Maisha ya Wesley yalikuwa na awamu tatu tofauti: ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Oxford kwa kuanzisha "Klabu takatifu" (Holy Club), ya pili huku Wesley akiwa mmisionari huko Savannah, Georgia; na ya tatu baada ya Wesley kurudi Uingereza. Katika maisha yake yote, Wesley aliendelea kuwa Mkristo na mtumishi wa Kanisa la Uingereza, yaani Anglikana. Aliona kuwa harakati yake ilikuwa ndani ya mipaka ya Kanisa Anglikana[1], ingawa iliendelea kwa kuwa kanisa la pekee.

Maisha ya awali

hariri

John Wesley alizaliwa huko Epworth, Uingereza. Alikuwa mtoto wa Samuel Wesley, mhitimu wa Oxford, aliyekuwa mchungaji wa Kanisa la Uingereza. Mnamo 1669, Samuel alimwoa Susanna Annesley.

Mnamo 1696, Samuel Welsey aliteuliwa kuwa kasisi kiongozi wa Epworth. Hapo ndipo John alipozaliwa. Watoto wa Wesley walifundishwa na wazazi wao wenyewe kwao nyumbani. Kila mtoto, pamoja na wasichana, alifundishwa kusoma haraka iwezekanavyo mara alipoweza kutembea na kuzungumza.

Wakati wa utoto wake, John Wesley alikuwa na hisia kali ya imani. Akiwa na umri wa miaka mitano, John aliokolewa kutoka nyumba iliyowaka moto. Kuopolewa humo kulitia hisia sana moyoni mwake. Alijiona kuwa ametengwa kwa ajili ya Mungu, kama "chapa iliyong'olewa kutoka motoni".

John alikubaliwa katika Shule ya Charterhouse, London. Huko aliishi (kwa muda) maisha ya kidini ambayo alikuwa amefunzwa nyumbani. Mwandishi wa wasifu wake, Tyerman, alisema kwamba John aliingia Charterhouse kama mtakatifu, lakini alipuuza majukumu ya kidini na kuondoka mwenye dhambi.

Mwanafunzi wa Oxford

hariri

Mnamo Juni 1720, Wesley aliingia Kanisa la Christ, Oxford, akiwa na posho ya pauni 40 kwa mwaka kama msomi wa Charterhouse. Afya yake ilikuwa mbaya na ilikuwa vigumu kwake kuepuka madeni. Huko, pamoja na kaka yake Charles, alifuata maisha madhubuti ya kidini. Alikwenda kanisani mara kwa mara, aliomba na kusaidia watu. Alitembelea wafungwa jela. Baadhi yao walihukumiwa kunyongwa. Shajara ya John imehifadhiwa inayoonyesha kwamba alijitayarishia ratiba ya masomo, ibada na huduma kwa kila siku ya juma. Akina Wesley na wanafunzi wengine wachache walishikamana katika "Klabu takatifu" wakaitwa "Wamethodisti" kwa sababu walifuata njia hii kali ya maisha (kwa Kiing. "method").

Mmisionari huko Georgia

hariri

John na Charles walikaribishwa kwenda koloni la Georgia katika Amerika ya Kaskazini wakiwa wachungaji wa kanisa Anglikana katika nchi hiyo mpya. Tumaini lao la kuwahubiria Waindio ili wawe Wakristo halikutimizwa. Baada ya mapenzi ya John kushindikana, ndugu walirudi nyumbani.

Walipovuka Bahari Atlantiki, jahazi lao ilipita katika dhoruba kali. John aliogopa litazama akawa na hofu kubwa. Lakini aliona kundi la abiria ambao hawakuonyesha hofu yoyote na hao walikuwa Wakristo Wamoravian. Tukio hilo lilimfanya afikiri kwamba imani yake haikuwa sawa na ya kwao. Aliwaona wana hakika kwamba Mungu ameshawasamehe dhambi zao kupitia imani katika Kristo kwa hiyo hawakuogopa kitu.

Mwanzo wa Uamsho

hariri

Baada ya kurudi, mnamo mwaka 1738, alisikia jinsi utangulizi wa Martin Luther kwa kitabu chake kuhusu Waraka kwa Waroma ulivyosomwa. John aliandika mistari iliyopata kuwa maarufu: "Nilihisi moyo wangu ukiwa na joto la kushangaza". Alichukua hisia hiyo kama ishara ya hakika kwamba Mungu alikuwa amemsamehe na kwamba alikubaliwa naye. Charles alipata kuwa na maarifa sawa ya wokovu karibu wakati huohuo. Hilo lilileta mapinduzi katika utumishi wao. [2] John Wesley aliandika vitabu vingi kuhusu Biblia na maisha ya Kikristo. Charles Wesley alimsaidia kwa kutunga nyimbo nyingi. [3] Nyimbo hizo ziliunga mkono ujumbe ambao John alihubiri.

Uinjilisti

hariri

Wesley alisafiri kila wakati, kwa kawaida akiwa amepanda farasi. [4] Alihubiria watu wengi. Baada ya muda baadhi ya viongozi wa Anglikana walimwambia asihubiri katika makanisa yao. Hapo alianza kuhubiri nje. Nyakati nyingine maelfu ya watu walisikiliza mahubiri yake. Wafuasi wake walibaki katika Kanisa la Anglikana, lakini waliunda “jamii” za pekee ili kusaidiana katika imani. Harakati zilipokuwa zikiongezeka, Wesley alichunguza na kutuma wahubiri, akaanza mashirika ya kutoa misaada, na kutunza wagonjwa. [5]

Wafuasi wake waliitwa Wamethodisti. Walienea katika nchi nyingi. Hivi karibuni kulikuwa na wengi katika Makoloni ya Uingereza huko Amerika. Baada ya Vita ya uhuru wa Marekani walibaki makasisi wachache wa Kianglikana huko Marekani. Wesley alituma wachungaji wawili kuwatunza Wamethodisti kule. Hatimaye, Wamethodisti waliendelea kuwa dhehebu la pekee katika Marekani na Uingereza.

Marejeo

hariri
  1. Thorsen, Don (2005). The Wesleyan Quadrilateral. Emeth Press. uk. 97. ISBN 0-9755435-3-9.
  2. "1738 John & Charles Wesley Experience Conversions | Christian History Magazine". Christian History Institute (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-08-17.
  3. "Charles Wesley | Hymnary.org". hymnary.org (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-08-17.
  4. Koontz, Terri; Mark Sidwell, S. M. Bunker (1993). World Studies. Greenville, South Carolina 29614: Bob Jones University Press. ISBN 1-59166-431-4.{{cite book}}: CS1 maint: location (link)
  5. Johnstone, Lucy (2003). Users and Abusers of Psychiatry: a critical look at psychiatric practice. Routledge. uk. 152. ISBN 0-415-21155-7.

Viungo vya Nje

hariri