Vita ya uhuru wa Marekani

Vita ya Uhuru wa Marekani ilipigwa kati ya Uingereza na walowezi wa makoloni yake 13 kwenye pwani ya Amerika ya Kaskazini katika miaka 1775 hadi 1783.

Jeshi la walowezi lililoongozwa na George Washington na wengineo lilishinda jeshi la Dola la Uingereza kwa msaada wa Ufaransa.

Hivyo hatimaye makoloni hayo yakapata uhuru kama “Muungano wa Madola ya Amerika" au Marekani.

Sababu za vita

hariri
 
Samuel Adams, kiongozi wa walowezi wakati wa uhuru.

Vita vilitokea kutokana na kutoelewana kati ya Dola la Uingereza na walowezi wake katika Amerika ya Kaskazini. Huko Uingereza ulikuwa na makoloni 13 (Connecticut, Delaware, Georgia, Maryland, Massachusetts, New Hampshire, New Jersey, New York, North Carolina, Pennsylvania, Rhode Island, South Carolina, Virginia) yaliyokaliwa na wahamiaji kutoka Uingereza wenyewe na nchi nyingine.

Serikali ya London ilitawala maeneo hayo kwa njia ya magavana na wanajeshi wake.

Sheria zilitungwa London zilizokataza kuanzishwa kwa viwanda kwenye makoloni na hivyo walowezi walilazimishwa kununua bidhaa nyingi kutoka Uingereza kwa bei za juu.

Baada ya Vita ya miaka saba Uingereza ulihitaji pesa ikaongeza kodi kwa bidhaa zilizosafirishwa kati ya makoloni na nchi mama. Walowezi hawakupendezwa na kodi za nyongeza: walidai kupewa wawakilishi katika bunge la London na nafasi ya kushiriki katika maazimio juu ya sheria zilizowaathiri. Walitangaza kaulimbiu ya “no taxation without representation” (hapana kodi bila uwakilishi).

Mwaka 1767 bunge la Uingereza lilikataa maombi ya wakoloni na badala yake idadi ya wanajeshi iliongezeka katika makoloni. Kwa sababu hizo wakoloni wengi walijisikia vibaya, eti walidharauliwa, wakaongeza ukali wa upinzani.

Mwaka 1773 umati ya watu walishiriki katika tukio la “Boston Tea Party“ wakatupa mizigo ya majani ya chai kwenye bandari ya Boston kwa kuonyesha upinzani wao dhidi ya kodi ya Waingereza.

Waingereza walijibu mwaka 1774 kwa sheria kali mpya na wanajeshi wao walianza kukusanya akiba za baruti katika makoloni. Hatua hiyo iliongeza uchungu kati ya wakoloni na wanamgambo wao walianza kufanya mazoezi ya kijeshi.

Viongozi wao wakaitisha mkutano wa kwanza wa wawakilishi kutoka makoloni yote wakaamua kwa pamoja kukataa biashara yoyote na Uingereza kwa muda wa mwaka mmoja hadi madai yao ya kupunguza kodi yatakapokubaliwa. Pia wakaanza kufanya mazoezi ya wanamgambo bila usimamizi wa Waingereza. Lakini hadi hapo hawakulenga bado kutafuta uhuru.

Mwaka 1775 Waingereza walitangaza koloni la Massachusetts kuwa eneo la waasi na sheria ya kukataza wavuvi kutoka Marekani kuvua samaki katika Atlantiki.

Mwanzo wa vita

hariri

Jaribio la wanajeshi wa kifalme kukamata tena akiba za baruti kati ya walowezi lilisababisha mapigano ya kwanza ya kijeshi yaliyotokea tarehe 19 Aprili 1775 karibu na mji wa Boston. Wanajeshi Waingereza walikutana na wanamgambo kwenye kijiji cha Lexington na baada ya kipindi cha kutazamana, risasi yalifyatuliwa; wanamgambo 8 waliuawa. Mapigano yalisambaa pia kwenye vijiji vya karibu. Wanamgambo wengi walifika nje ya Boston wakawazuia Waingereza ndani ya mji.

Baada ya wiki mbili mkuu Mwingereza alijaribu kuwafukuza na mapigano ya Bunker Hill nje ya Boston yalitokea. Hayo yalikuwa mapigano makubwa ya kwanza; Waingereza walishinda, lakini walipoteza wanajeshi 226 waliouawa, wakati wanamgambo walipoteza wayu 140 pekee.

Vita na uhuru

hariri

Sasa vita kamili vilisambaa. Mwanzoni Waingereza walikuwa na silaha na wanajeshi wengi zaidi, wakasonga mbele, lakini wanamgambo ya walowezi wakioongozwa na George Washington waliendelea kuwashambulia.

Tarehe 4 Julai 1776 wawakilishi kutoka makoloni yote walitangaza uhuru wa Muungano wa Madola ya Amerika. Bado Waingereza walisonga mbele wakatwaa pia mji wa New York.

Lakini tangu mwaka 1777 Ufaransa ulianza kwa siri kutuma silaha kwa Wamarekani; mwaka 1778 Ufaransa, Hispania na Uholanzi ziliungana na kutangaza vita dhidi ya Uingereza. Manowari za Ufaransa zilishambulia meli za Waingereza zilizopeleka silaha na askari kwenda Marekani.

Mwaka 1781 sehemu kubwa ya jeshi la Uingereza ilishindwa kwenye mji wa Yorktown ikalazimika kujisalimisha.

Tangu siku hiyo mapigano yalipungua na mwaka 1783 Uingereza ukakubali uhuru wa makoloni yake ya awali.

Wakazi wengi wa makoloni walioendelea kusimama upande wa Uingereza walihamia Kanada iliyobaki kuwa koloni.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Vita ya uhuru wa Marekani kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.