Karl Marx

Mwanafalsafa wa Ujerumani (1818-1883)

Karl Marx (1818 - 1883) alikuwa mwanafalsafa kutoka nchini Ujerumani ambaye pamoja na Friedrich Engels alianzisha siasa ya ukomunisti.

Karl Marx

Maisha yake

hariri

Alizaliwa mjini Trier tarehe 5 Mei 1818.

Kati ya 1835 na 1841 alisoma sheria, historia na falsafa.

Tangu 1842 alikuwa mwandishi mkuu wa gazeti la Rheinische Zeitung mjini Köln. Alisimama upande wa wafuasi wa demokrasia dhidi ya utawala wa watemi na wafalme katika Ujerumani.

Kutokana na upinzani huo serikali ya Prussia ilimkataza asiandike tena kwenye magazeti, hivyo alihamia Ufaransa. Alipokaa mjini Paris alianza kuandika juu ya ujamaa kama ukamilisho wa demokrasia.

Baada ya kuhamia Brussels katika Ubelgiji alitunga pamoja na Engels kijitabu cha Manifesto ya Chama cha Kikomunisti (Ilani ya kikomunisti) alimotangaza imani yake ya kwamba "historia ya jamii zote ni historia ya mapambano ya matabaka". Alichora picha ya historia ambako jamii ya kikabaila imezaa ngazi mpya ya ubepari; hapo alitabiri kwamba ubepari utazaa tena mbegu wa uharibifu wake na utafuatwa na ujamaa au ukomunisti. Ukomunisti utakuwa na jamii bila matabaka na bila utawala. Aliona ya kwamba wafanyakazi kama tabaka linalozalisha utajiri wanapaswa kuchukua utawala mikononi mwao kwa njia ya mapinduzi akawaalika, "Wafanyakazi wa nchi zote muungane!".

Baadaye Marx alipaswa kukimbia Ulaya bara akapata kimbilio Uingereza alipoishi London hadi kifo chake, akitumia muda mwingi kwenye maktaba ya Britania. Alikuwa na vipindi vya umaskini mkali lakini alipata tena msaada kutoka kwa rafiki yake Engels. Kwa miaka kadhaa alikuwa mwanahabari wa gazeti la Marekani "New York Tribune".

Huko London aliandika kitabu chake kikuu "Das Kapital" (yaani "Rasilmali").

Aliaga dunia tarehe 14 Machi 1883 akazikwa kwenye makaburi ya Highgate Cemetery.

Falsafa yake

hariri

Kwa Marx kazi ya falsafa haikuwa kueleza dunia ilivyo bali kuibadilisha. Alifundisha ya kwamba mawazo, fikra na imani zote zinatokana na hali ya uchumi na teknolojia katika jamii.

Mwenyewe aliathiriwa sana na Georg Wilhelm Friedrich Hegel na kutoka kwake alipokea hoja ya kuwa historia linafuata kanuni zake likielekezwa kwenye lengo maalumu. Tofauti na Hegel aliona historia haisukumwi na "roho ya ulimwengu" bali na nguvu za uchumi wa jamii na namna ya kujipatia riziki za maisha.

Kutokana na msingi huu Marx alikataa dini na imani ya Mungu. Kwake dini ni itikadi ya jamii ya uwongo na pamoja na sahihisho la jamii alitarajia ya kwamba dini itapotea.

Matokeo yake

hariri

Baada ya kifo chake Engels aliendelea kutoa maandiko yake kama vitabu.

Marx alikuwa na athira kubwa kati ya vyama vya wafanyakazi vya Ulaya vyenye mwelekeo wa kisoshalisti.

Baadaye kundi kali kati ya wasoshalisti Warusi chini ya Lenin iliendelea kupanua mafundisho ya Marx kwa "Umarx-Ulenin" iliyokuwa itikadi rasmi ya vyama vya kikomunisti.

Marx aliheshimiwa kama nabii katika nchi zilizotawaliwa na Wakomunisti, kuanzia Urusi hadi kuenea kwa thuluti moja ya watu wote duniani.

Hasa kuanzia mwaka 1989 athari yake imepungua.

Viungo vya nje

hariri

Maandiko yake

hariri
 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Maisha yake

hariri

Makala na kamusi

hariri