Ludwig Krapf

(Elekezwa kutoka Krapf)

Johann Ludwig Krapf (11 Januari 181026 Novemba 1881) alikuwa mmisionari wa kwanza wa Uprotestanti nchini Kenya katika karne ya 19 akatunga kamusi ya kwanza ya lugha ya Kiswahili.

Johann Ludwig Krapf.
Ukurasa wa kwanza wa tafsiri ya Biblia kwa Kiswahili ya Krapf ilivyochapishwa katika jarida la kitaalamu la Marekani mwaka 1849.

Masomo Ujerumani na Uswisi

hariri

Krapf alizaliwa tarehe 11 Januari 1810 katika kijiji cha Derendingen karibu na Tübingen, eneo la Württemberg, Ujerumani wa Kusini-Magharibi katika familia ya wakulima wadogo Walutheri.

Alisoma shule ya msingi kijijini kwake halafu shule ya sekondari Tübingen. Akiwa mwanafunzi alipenda sana masomo yote yaliyohusu jiografia na lugha. Pamoja na Kilatini na Kigiriki alisoma pia Kifaransa na Kiitalia.

Alipokuwa na umri wa miaka 16 alitembelea mara ya kwanza nyumba ya Misioni ya Basel, Uswisi. 18271829 alijiunga na kozi ya kuandaa wamisionari huko Basel lakini hakupendezwa na maisha ya pamoja; akishikwa na wasiwasi kuhusu wito wake akarudi nyumbani na kuingia masomo ya teolojia katika Chuo Kikuu cha Tübingen.

Krapf alimaliza masomo yake mwaka 1834. Vituo vya huduma kama mchungaji msaidizi na mwalimu vilifuata. Wakati ule alikutana na mmisionari aliyempa moyo kurudi Basel.

Ethiopia 1837-1842

hariri

Mwaka 1836 alikutana na mwakilishi wa Church Missionary Society (CMS) aliyemkaribisha kufanya kazi na CMS. Misioni ya Basel ilimpa ruhsa akapokea wito wa kwenda Ethiopia. Krapf alianza mara moja kujiandaa akisoma Ge’ez (lugha ya Kale ya Ethiopia) na Kiamhari (lugha ya kisasa ya Wakristo katika nyanda za juu Ethiopia).

1837-1842 Krapf alifanya kazi ya umisionari huko Ethiopia. Mpango wa misioni ya CMS ilikuwa kuwaamsha Wakristo Waorthodoksi kwa matumaini ya kwamba watakuwa wenyewe wamisionari bora kwa wenzao Wapagani au Waislamu.

Lakini Krapf hakuelewa vema Ukristo wa kiorthodoksi wa Waamhari. Alishindwa kuelewa maana ya liturgia, mila na desturi nyingi. Hakuelewa hasa kwa nini Wakristo Waorthodoksi walisoma Biblia katika lugha ya kale ya Ge’ez hata wasipoelewa lugha hiyo badala ya kutumia tafsiri ya Kiamahari aliyokuwa amefanya.

Hivyo Krapf alijisikia amevutwa zaidi na Wagalla – hili ni jina la zamani za watu wanaojulikana leo kama Waoromo au Borana. Wagalla kwa jumla walikuwa wakifuata dini zao za kiasili, athira za kiislamu zikianza kuonekana. Krapf alijifunza lugha yao alianza kutafsiri sehemu za Agano Jipya katika Kigalla (Kioromo).

Mwaka 1842 Krapf alipaswa kuondoka Ethiopia pamoja na wamisionari wengine wa Kiprotestanti, akiwa na ndoto ya kurudi na kufanya kazi kati ya Wagalla. Alikaa muda kidogo Kairo (Misri) akafunga ndoa, bibiarusi alikuwa amemfuata kutoka Ujerumani.

Wakati ule kwake nyumbani Tübingen Chuo Kikuu kilikuwa kimefuata taarifa zake na 1842 kikampa cheo cha udaktari (PhD) kwa ajili ya utafiti wake katika lugha na historia ya Ethiopia.

Afrika ya Mashariki 1844-1853

hariri

Ethiopia ilikuwa imefunga milango yake, hivyo Krapf aliwaza njia nyingine. Alikuwa amesikia ya kuwa Wagalla waliwahi kufika hadi pwani za Afrika ya Mashariki. Hivyo akasafiri hadi Zanzibar kwa lengo la kuwafikia Wagalla kupitia eneo la Kenya ya leo. Sultani Seyyed Said alimpa ruhusa ya kuanzisha kituo cha misheni huko Mombasa.

Mwaka 1844 Krapf alifika Mombasa akianza mara moja kujifunza Kiswahili pamoja na lugha ya wazalendo wa eneo la Mijikenda. Huko mke na mtoto waliugua malaria wakafa. Krapf alihamia Rabai iliyoko katika vilima juu ya Mombasa penye joto kidogo akaanzisha kituo cha Rabai Mpya.

Mwaka 1846 mmisionari mwingine (Johannes Rebmann) alikuja kufanya kazi pamoja naye. Huko Rabai Mpya Krapf alitunga kamusi na sarufi ya kwanza ya Kiswahili.

Krapf na Rebmann walikuwa Wazungu wa kwanza walioona milima yenye theluji Afrika. Rebmann aliona Kilimanjaro, Krapf aliona Mlima wa Kenya. Taarifa zao zilipofika Ulaya zilichekwa na wataalamu waliodai milima yenye theluji haiwezekani Afrika.

Krapf aliendelea kuwa na matatizo ya afya akarudi Ujerumani mwaka 1853.

Urithi wake

hariri

Hadi kifo chake aliendelea kuboresha vitabu vyake kuhusu utamaduni na lugha za mataifa mbalimbali ya Afrika. Kwa jumla aliandika kamusi au kutafsiri sehemu za Biblia katika lugha zifuatazo: Ge’ez, Kiamhari, Kioromo, Kiswahili, Ki-mijikenda, Kikamba, Kimasai.

Ludwig Krapf alitoa mchango mkubwa sana katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwani aliweza kutafsiri Injili ya Luka na ya Mathayo ,pia aliweza kuandika sarufi ya Kiswahili inayohusu jamii ya Wasambaa.

Nyumba yake huko New Rabai imekuwa makumbusho chini ya Museums of Kenya. Jengo la Ubalozi wa Kijerumani huko Nairobi limepewa jina lake.

Krapf alikuwa Mlutheri, lakini Kanisa Anglikana linamkumbuka kama mwanzilishi wa madhehebu yake nchini Kenya.

Marejeo

hariri
  • Krapf, Ludwig: A dictionary of the Suahili language, London 1882
  • Raupp, Werner: Gelebter Glaube. Metzingen/Württemberg 1993, 278 - 287: "Johann Ludwig Krapf - Bahnbrecher der ostafrikanischen Mission".
  • Gütl, Clemens. 2001. Johann Ludwig Krapf - "Do' Missionar vo' Deradenga" zwischen pietistischem Ideal und afrikanischer Realität. Hamburg, 2001 (Beiträge zur Missionswissenschaft und interkulturellen Theologie, Bd. 17); ISBN 3-8258-5525-2.
  • Gütl, Clemens: "Memoir on the East African Slave Trade" ya Johann Ludwig Krapf aliyoiandika mwaka wa 1853 bila kuichapisha rasmi. Imetolewa na Gütl pamoja na maelezo katika jarida. Vienna, 2002 (Beiträge zur Afrikanistik, 73).
  • Eber, Jochen: Johann Ludwig Krapf: ein schwäbischer Pionier in Ostafrika. Riehen/Lahr 2006.
  • Raupp, Werner: Johann Ludwig Krapf. Missionar, Forschungsreisender und Sprachforscher. 1810–1881. In: Gerhard Taddey, Rainer Brüning (Hrsg.): Lebensbilder aus Baden-Württemberg, Band 22. Stuttgart 2007, (182) - 226.
  • Raupp, Werner: Johann Ludwig Krapf, "dr Missionar vo Deradinga". In: Hin und weg. Tübingen in aller Welt. Hrsg. von Karlheinz Wiegmann. Tübingen 2007 (Tübinger Kataloge, 77), (90) - 99.
  • Raupp, Werner: Morgenroth des Reiches Gottes. In: Tübinger Blätter 96 (2010), 70 - 73.
  Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.