Ngw'anamalundi

(Elekezwa kutoka Malunde)

'

Igulu Bugomola
AmezaliwaMwakubunga Nera
AmefarikiSeke-Bukoro
Majina mengineNgw'anamalundi
Kazi yakeMcheza ngoma za Kisukuma


Ngw'anamalundi (kwa matamshi mengine Mwanamalundi; jina asili: Igulu Bugomola, Igulu ikiwa na maana ya mbingu) alikuwa mtu maarufu wa kabila la Wasukuma.

Alikuwa mcheza ngoma au Mbina mashuhuri ambaye alipewa jina hilo kama utani likimaanisha miguu myembamba na mirefu [1]

Katika maisha yake yote Mwanamalundi aliwapenda sana watu wa jamii yake, hivyo alishirikiana nao vyema katika shughuli mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi na hata katika masuala ya kijamii kama vile sherehe za kitamaduni kwa kuwachezea ngoma ya kabila lake.

Maisha

Ngw'anamalundi alizaliwa katika kijiji cha Mwakubunga Nera, Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza mnamo 1846[2] au Ng'wakwibilinga, wilaya hiyohiyo mwaka 1892, akiwa mtoto wa mwisho na pekee wa kiume kati ya watoto wanne wa familia ya mzee Bugomola na Ngolo Igulu.

Igulu (Ngw'anamalundi) alikua na tabia ya uzururaji na haikuwa rahisi kumkuta nyumbani. Alikua mahiri wa kucheza ngoma, na mara nyingi alifuatwa na kundi la watoto kwa sababu hiyo. Hali hii iliwachukiza wazazi wengi kutokana na kwamba watoto wao, ambao walikuwa wakiwategemea katika kuchunga mifugo, waliwatelekeza mifugo na kumfuata Igulu, hivyo kupelekea kupotea kwa watoto wa mifugo hao. Walimkebehi kwa msemo “Mamirundi galyo lilihumbura bhana bhise” ikiwa na maana ya “mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”: hiyo ilipelekea kufutika jina la Igulu na kuwa Ng’anamalundi.

Ngw’anamalundi alianza kujiimarisha kwenye ngoma baada ya kuona watu wengi kijijini wanamchukia, huku kulimpelekea kuanza tena kupendwa na vijana wengi; alipata wafuasi kiasi kwamba alianza kutumika kama jeshi la kukodiwa na Watemi vinapotokea vita. Kikundi chake kilikua na kuanza kutumika katika sherehe mbalimbali kwenye familia za kitemi za wakati huo.

Mwanamalundi alifariki mwaka 1936 kwa maradhi ya kawaida na kuzikwa Ididí Jihū huko kijiji cha Seke katika Mkoa wa Shinyanga. Tukio la kifo chake liliitwa "hang'witulo gwa shigela" likimaanisha "Vita vya kuwakimbia Wamasai". Hii ni kwa sababu wakati Mwanamalundi anakata roho, kulitokea kishindo kikubwa kama tetemeko la ardhi. Watu wengi walikimbia ovyo kwa hofu kuwa labda Wamasai wamevamia eneo lao ili kuwaua. Baada ya kishindo hicho, giza likaingia ghafla, giza ambalo hata kuku wakaanza kurudi nyumbani, fisi wakaanza kutembea mitaani wakidhani ni usiku. Hata baada ya mazishi yake, kaburi lake lilifuka moshi mwingi sana uliopanda mpaka juu mawinguni na kutengeneza giza la muda mfupi.

Kaburi lake lipo na linatembelewa na wafuasi wa dini za jadi.[3]

Umaarufu wake

Mwanamalundi alikuwa maarufu sana karne ya 19 (enzi za mkoloni) maeneo ya kanda ya ziwa; hususani Mwanza na Shinyanga. Habari za huyu mtu zimewahi kuandikwa kwenye kitabu kiitwacho "Mwanamalundi: Mtu maarufu katika Historia ya Usukuma". Ni kitabu ambacho kiliingizwa kwenye mtaala wa elimu ya msingi miaka ya 1970-80. Hivi sasa habari za mtu huyu ni kama vile zimepotea kabisa.

Kuna watu mashuhuri kabla yake kama akina Níndwa, Italange na Sïta waliokuwa watu wa miujiza kama Mwanamalundi ambaye anasemekana aliweza kutembea hewani bila kukanyaga ardhi, kujibadili na kuwa kiumbe tofauti kama mnyama, ndege, majani, mti au jiwe na uwezo wake wa kutembea juu ya maji au kuwa ndani ya maji kwa muda mrefu.

Inasemekana alikuwa na miujiza mingi ya kutisha: akiwa kiongozi katika jamii aliyoishi, alikuwa na wafuasi wake kama walinzi popote alipokuwa anakwenda; kwa kipindi kirefu wafuasi wake hawakubahatika kuiona sura yake, yaani ngozi yake asilia, bali muda wote waliona kama matope mabichi na yeyote yule aliyethubutu kutaka kutazama sura hiyo kwa siri wakati wa usiku hatimaye hufariki pakuchapo.

Miongoni mwa maajabu aliyoyaonesha katika jamii hiyo ambalo mpaka leo kabila la Wasukuma likirejelea kama tukio la kihistoria ni pale tu mtu huyo alipokwenda kuketi katika mwamba uliopo katika Ziwa Viktoria Nyanza, leo hii maarufu kama Bismarck Rock, na kuacha alama za makalio yake pamoja na kugongelea mambo za miti katika mwamba huo na kuzama.

Hadithi mbalimbali

Wazazi wake hawakujaliwa kupata watoto kwa muda mrefu sana. Uzee uliwakaribia bila kupata mtoto. Jambo hili liliwakosesha raha, hasa Mzee Bugomola ambaye alitamani sana apate mrithi wa mali zake. Hali hii ilimfanya Bugomola kuwa mtulivu na mpole muda mwingi katika maisha yake.

Katika jamii ya Wasukuma wakati huo, mwanamke asiposhika mimba ndani ya kipindi cha miezi 6 hadi 12 tangu aolewe, ilikuwa ni lazima aende kwa mganga kujua kinachomsumbua. Ni nyakati ambazo hakukuwa na makanisa ya maombezi, misikiti ya kuomba dua wala hospitali kama ilivyo leo hii. Waganga ndio watu pekee waliotatua matatizo mbalimbali ya jamii zao.

Mzee Bugomola na mke wake Ngolo wakaamua kwenda kwa mganga upande wa mashariki ya kijiji walichokuwa wakiishi ili wapate ufumbuzi wa tatizo lao. Mganga aliwaambia ujio wao hata kabla hawajajieleza. Mganga akawatengenezea dawa kisha akawaambia kuwa Ngolo atashika mimba na atazaa mtoto wa kiume ambaye atakuja kuwa mashuhuri siku za mbele lakini kwa bahati mbaya Bugomola hataweza kumuona mtoto huyo; yaani Bugomola atafariki kabla mtoto hajazaliwa.

Habari hii ilimfurahisha sana Bugomola pamoja na kwamba aliambiwa atakufa bila kumuona mtoto. Mkewe pia alifurahi kusikia kuwa atashika mimba. Bugomola hakujali kifo chake sababu hata umri wake ulikuwa umekwenda kidogo. Furaha yake kubwa ilikuwa kumpata mrithi wake. Walirudi nyumbani wakiwa na furaha kubwa; Bugomola hakuweza kuificha. Muda mwingi alionekana mwenye tabasamu na vicheko vingi tofauti kabisa na vile watu wavyomzoea kumuona.

Baada ya wiki kadhaa Ngolo alishika mimba. Mimba ilipotimiza miezi mitatu tu, Bwana Bugomola aliaga dunia bila hata kuugua. Ngolo ambae alikuwa mjane wakati huo aliilea mimba hiyo hadi ilipofikisha miezi 9.

Siku moja kabla Ngolo hajajifungua, wingu kubwa lilitanda angani. Mvua kubwa na yenye radi kali ikaanza kunyesha. Mtoto aliyekuwa tumboni akaruka mruko usio wa kawaida na kisha ikasikika sauti ya kitoto kutoka tumboni ikisema, "máyù nibyalage, yaani mama nizae!" Ngolo akashtuka na kuingiwa hofu baada ya kusikia sauti hiyo, hivyo akamuita mama mkwe wake na baadhi ya majirani ili nao waweze kuwa mashahidi wa sauti hiyo. Kwa bahati nzuri sauti ile ikajirudia tena na ghafla uchungu ukamshika Ngolo. Ulikuwa mwaka 1892 Ngolo alipojifungua mtoto wa kiume mwenye maajabu tangu akiwa tumboni mwake. Mtoto huyo akaitwa Igulu, yaani Mbingu.

Igulu (Mwanamalundi) alizaliwa akiwa mwenye afya njema kabisa isipokuwa tu miguu yake ilikuwa myembamba na yenye nyayo kubwa tangu alipozaliwa. Kutokana na wembamba wa miguu yake, jamii ikampa jina la utani "Mamilundi" likimaanisha "mamiguu membamba".

Igulu alikuwa mtu mwenye aibu sana enzi za utoto wake. Alikuwa akiwakimbia wageni wasimuone na kuuficha uso wake kwa aibu. Pamoja na aibu alizokuwa nazo, alipenda sana kuzurura mitaani akiwa ameambatana na marafiki zake. Baadhi ya wazazi hawakupendezwa na tabia yake ya uzururaji akiwa ameambatana na watoto wao. Mara kadhaa wazazi wa marafiki wa Igulu walimtamkia Igulu (Mwanamalundi) maneno mabaya kila alipotoka kuzurura na watoto wa majirani zake, walimwambia, “Mamirundi galyo lilihumbura bana bise”, ikiwa na maana "mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”.

Katika ujana wake Igulu, alipenda sana kucheza ngoma aina ya kahela. Kila aliposhiriki kucheza ngoma hiyo, alipenda sana kuuficha uso wake kwa kitambaa cheusi. Katika mashindano ya kucheza ngoma hiyo, Igulu na marafiki zake walishindwa kuwa washindi. Watu kama Samíke, Ng'wanikinga, Ng'wanilong'ho na Gíndù Nkíma walikuwa si rahisi kuwashinda katika uchezaji wa ngoma. Ni watu ambao walijua kucheza ngoma kwa umahiri kuliko Igulu (Mwanamalundi). Mara nyingi matumizi ya uchawi yalihusika katika kuwapa ushindi wa kucheza ngoma hiyo na kukubalika kwa watu mbalimbali.

Kutokukubalika kwa Igulu (Mwanamalundi) na marafiki zake mbele ya jamii, hasa katika uchezaji wa ngoma, kulipelekea achukue uamuzi wa kwenda kwa mganga. Igulu aliwashawishi vijana wenzie waende kwa mganga atakayewapa dawa ya mvuto kwa watu na kuwa washindi nyakati zote za mashindano ya ngoma. Vijana wenzie walikubali kwa sababu kwa nyakati zile suala la kwenda kwa mganga lilikuwa la kawaida sana.

Safari ya kuelekea mashariki zaidi mwa kijiji chao ikawadia. Mganga alikuwa mwanamke, mwenye umri ufaao kuitwa bibi ndani ya kijiji cha Nyaraja, wilaya ya Iramba, mkoa wa Singida. Walipokewa vizuri na mwenyeji wao. Iliwachukua wiki moja bila kuhudumiwa chochote kile, siku ya nane mganga akawaamuru wachukue panga na majembe kuelekea porini ili wakachimbe dawa itakayowasaidia kupendwa na watu.

‘’Tujagi lolo ngh’wiporu bhana bhane’’ akiwa na maana ya "twendeni sasa porini watoto wangu", bibi huyo aliwaambia Ngw’anamalundi na wenzake ili waongozane naye kwenda porini.

Njiani bibi alikamata vinyonga watatu na kuwawekea kichwani kila mmoja, kisha safari ikaendelea kuelekea katikati ya pori hilo nene. Baada ya kufika huko, mzee aliwaambia wasimame na kuamuru kila mmoja achimbe shimo refu sawa na urefu wake mpaka kiunoni. Baada ya zoezi hilo kukamilika aliwaambia wakusanye kuni na kuzitumbukiza humo. Baada ya hapo waliwasha moto kwa njia ya kupekecha, moto ulipokolea sana waliwachukua wale vinyonga watatu na kuwawekea dawa midomoni na kuwatupa ndani ya moto huo, wakateketea wote. Wakiwa wanaendelea kushangaa kuungua kwa vinyonga hao, Ngw’anamalundi na wenzake walimwona kifaru akitoka kwenye moto huo na kuanza kuwakimbiza; wote walikimbia hovyo kila mmoja na njia yake.

Ngw’anamalundi alikimbia na kupanda juu ya mti, kifaru yule alifika kwenye shina la mti na kuanza kuliparua kwa hasira na baada ya muda aliondoka, Ngw’anamalundi alimwona bibi yule akikutana na kifaru kabla hata hajafika mbali, na alimshuhudia akimrarua bibi yule mpaka akafa.

Igulu (Mwanamalundi) akashuka juu ya ule mti na kumwendea bibi mganga ambaye muda huo ni marehemu. Igulu akaubeba mwili wa yule bibi mganga na kuurudisha nyumbani. Akiwa njiani, ule mwili wa bibi mganga uliokuwa mabegani mwake ukaonesha kuwa ni kama vile unavuta pumzi mapafuni. Ghafla yule bibi akapiga chafya na kuamka kisha akamuuliza Igulu (Mwanamalundi), "Bhaja hálí abhayanda abhalaha" akimaanisha kuwa wako wapi vijana waliokuwa hapa? Igulu akamwambia kuwa wale vijana wenzie wamekimbia baada ya kumuona yule kifaru. Bibi mganga ambaye muda huu alionekana kuwa mzima kabisa na hana majeraha tena akaomba warudi eneo la tukio ili wachukue dawa. Wakiwa njiani kurudi eneo la tukio, yule bibi mganga akamsifia sana Igulu kwa kumuita "Ni mwanamume kamili" aliyekuja kweli kutafuta dawa. Bibi akaokota yale magome yaliyobanduliwa na kifaru na kisha kuondoka nayo.

Walipofika nyumbani, yule bibi akaamua kumwambia ukweli Igulu (Mwanamalundi) kuwa yule kifaru ni yeye mwenyewe bibi. Aliamua kujibadili ili kuwapima uwezo wao wa kuvumilia magumu. Kwa kuwa Igulu pekee ndiye aliyeonesha yuko imara, bibi yule alimtunuku dawa nzuri zitakazompa mvuto na nguvu katika ngoma zake. Wale vijana wawili walipitiliza hadi kwao bila kurudi tena kwa mganga. Bibi mganga alimpa masharti Igulu baada ya kumpa dawa: alimzuia kumparaza mtu yeyote au kumnyooshea kidole. Iwapo atafanya hivyo basi aliyeparazwa au kunyooshewa kidole atakufa hapohapo.

Igulu (Mwanamalundi) aliporudi kijijini kwake na kisha kucheza ngoma ya kwanza baada tu ya kurudi kutoka kwa mganga, alishinda. Kuna nyakati Igulu aliamua kucheza ngoma akiwa juu ya jiwe kubwa. Wakati akicheza ngoma hizo, nyazo zake zilionekana juu ya mawe aliyokuwa akitumia kucheza ngoma. Ni alama za nyayo ambazo zipo mpaka leo pale kijiji cha Nyandekwa, wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga. Ni kama km 10 tu kutoka makao makuu ya wilaya. Kuna nyakati Igulu alitengeneza mashimo ya mchezo wa bao juu ya jiwe kwa kutumia kisigino chake. Ni alama ambazo pia bado zipo kijiji cha Nyandekwa, Kahama.

Igulu aliposhinda mashindano ya ndani ya kijiji, akaamua kuomba kushindana na wapinzani wakubwa zaidi walioishi kijiji cha Ng'wagala, wilaya ya Maswa; yaani akina Samíke, Ng'wanikînga, Ng'wanilog'ho na mwanamke mwenye nguvu za kiganga aitwaye Gíndü Nkíma. Hawa watu wanne walikuwa hawana mpinzani katika ngoma lakini Igulu (Mwanamalundi) akajitosa kushindana nao kwa mara nyingine.

Mwanamalundi alipofika kwenye mashindano, akafanya miujiza kwa kujirefusha kama ngongoti asiye na magongo yoyote yale, kisha akaanza kucheza huku akiwa ameficha uso wake kwa kitambaa cheusi kama kawaida yake. Wakati anacheza ngoma akiwa ana urefu wa ngongoti, baadhi ya watu walijaribu kugusa na kuifunua miguu yake ili wajue kulikuwa na nini. Wote waliothubutu kuigusa walikufa baada ya muda mfupi. Katika ngoma hiyo, Gíndü Nkíma akatumia nguvu zake za kiganga kumrudisha Igulu (Mwanamalundi) kama alivyokuwa awali, yaani pasipo kurefuka kama ngongoti. Kwa kufanya hivyo, Mwanamalundi alipoteza pambano hilo.

Mwanamalundi akaondoka Maswa na kwenda kijiji cha Nela ambako lilipangwa shindano jingine. Shindano hili Mwanamalundi alishinda. Kwa kuwa katika safari zake zote huambatana na jopo la wapishi wa chakula, ushindi huu ulimkwaza Gíndü Nkíma, mpinzani wake mkubwa ambaye aliamua kuloga chakula anachoandaliwa Mwanamalundi ili kisiive hata kikipikwa wiki nzima.

Ni kweli kabisa, wapishi wa Mwanamalundi walilalamika kuhusu chakula kutoiva kabisa kwa muda mrefu na kuni zinakaribia kuisha. Hivyo wapishi wakaomba msaada wa kuni kwa Mwanamalundi. Baada ya wapishi kulalamika, Mwanamalundi akanyoosha kidole kwenye pori fulani eneo hilo na kuwaambia wapishi waende wakakate kuni alikonyooshea kidole. Kwa bahati mbaya wakati ananyoosha kidole hicho hakujua kama ndani ya pori hilo kulikuwa na mifugo na wachungaji kadhaa ambao wote walikufa na kukauka kama kuni.

Tukio hili la kukausha miti na kuua ng'ombe na wachungaji wake lilimuudhi sana Mtemi Masanja III ambaye aliamuru askari wake waende kumkamata Mwanamalundi haraka iwezekanavyo ili awajibishwe. Askari wa Mtemi Masanja waliogopa sana kumkamata Mwanamalundi wakihofia kufa. Iliwalazimu kumkamata tu sababu walimuogopa zaidi mtemi kuliko Mwanamalundi.

Kabla Mwanamalundi hajakamatwa, alijua jambo hilo lingetokea. Hivyo akaenda haraka kumuaga mama yake mzazi na kumuachia maagizo. Mwanamalundi alikamua maziwa kiasi fulani kwenye kikombe, kisha akampa mama yake na kumwambia, "Iwapo maziwa haya yataanza kuganda, ujue kuwa nipo katika hali mbaya, iwapo yataganda kabisa, ujue kuwa nimekufa!" Mwanamalundi akachukua shoka isiyo na mpini kisha akaiegamisha ukutani na kumwambia mama yake, "Iwapo nitakamatwa na kupelekwa kuuliwa, shoka hii itakuwa ikipanda ukutani nikiwa napelekwa kuuliwa, tukifika eneo nitakalouliwa, basi hii shoka itapandisha hadi mwisho wa ukuta kuonesha kuwa tumefika mwisho wa safari!" Mama yake alipokea maagizo hayo na haikuchukua muda Mwanamalundi akakamatwa na askari wa Mtemi Masanja.

Mtemi Masanja III aliamua kupeleka shauri hilo kwa watawala wa Kizungu (Wajerumani) ili wamchukulie hatua Mwanamalundi. Uchunguzi ukafanyika na Mwanamalundi akaonekana ana hatia ya mauaji ya watu wasio na hatia. Adhabu ya kosa hili ilikuwa ni kunyongwa.

Katika safari hii ya kunyongwa, Mwanamalundi aliambatana na Makongoro Igana ambaye alikuwa Mtemi wa Ilemela. Mtemi huyu alikuwa ana hatia ya kuwachapa fimbo Wajerumani baada ya kupita upande usio sahihi katika njia kadiri ya utaratibu wa utawala wake. Mtemi Makongoro Igana kila alipokuwa akisafiri juu ya punda, mkono wake wa kuume ulikuwa umeshika fimbo ndefu. Fimbo hiyo hutumika kumchapia kila atakayepita upande wa kuume katika safari zake. Kwa bahati mbaya Wajerumani hawakujua utaratibu huo wa Mtemi Makongoro. Siku Wajerumani walipopishana safarini na Mtemi Makongoro, walipita upande wa kuume wenye fimbo. Mtemi Makongoro akawachapa fimbo Wazungu hao kama ilivyo jadi yake. Wazungu hao walishindwa kumvumilia, wakamkamata na kumfungulia mashtaka yaliyoamuru Mtemi anyongwe.

Kaliyaya ni mtu wa pili aliyeambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa. Huyu Kaliyaya alikuwa mtu aliyeonekana mwenye ushawishi mkubwa kwa watu wa jamii yake. Kukubalika kwake kulimfanya apate wafuasi wengi ambao walihofiwa kumpindua Mjerumani. Hivyo Wajerumani wakaona ni bora wamfungulie mashtaka ili wamnyonge kabla hajawapindua. Kaliyaya alikuwa mtu wa kawaida tu ila mwenye ushawishi na kipenzi cha watu wengi.

Mtu wa tatu aliyeambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa ni Mtemi Italange wa Bugando. Mtemi huyo aliingia mgogoro na Wajerumani baada ya kuhodhi eneo kubwa la pwani ya ziwa Viktoria na bandari zake, kisha akakataa kuwapa Wajerumani. Ili kumnyang'anya utajiri huo, Wajerumani wakaamua kumfungulia mashtaka ili wamnyonge.

Zoezi la kunyongwa lilipofika, Mwanamalundi alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuvishwa kitanzi. Kamba ilipofyatuliwa tu ili kumuua, kamba ikakatika yenyewe. Zoezi la kumuua likaahirishwa, badala ya kunyongwa akabadilishiwa adhabu.

Ikaja zamu ya Mtemi Makongoro Igana. Mtemi alipowekewa tu kitanzi shingoni na kisha kuifyatua kamba hiyo ili kumuua, ghafla kukatokea mfano wa sinema kwenye ukuta. Ni sinema ya kimiujiza iliyoonesha matukio ya kivita miaka ya nyuma. Askari wakageuka kuitazama sinema hiyo. Sinema haikuchukua zaidi ya dakika moja, ikaisha. Walipomgeukia Mtemi Makongoro Igana wakaona hana kamba shingoni. Huyu naye akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu.

Akaja Mtemi Italange. Huyu alipowekewa kitanzi shingoni, naye pia kamba ilifyatuka. Akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu. Ilipofika zamu ya Bwana Kaliyaya, kitanzi kilipofyatuliwa ili kumnyonga, hakika kitanzi kilimuua. Huyu hakuwa mwenye ulinzi wowote ule kishirikina; yaani alikuwa mtu wa kawaida tu.

Ndipo mamlaka za Mjerumani zikaamuru askari wawapeleke watu hao watatu Tabora. Wakiwa njiani kuelekea huko, walifika Nzega na kuamua kupumzika kidogo chini ya mti mkubwa nje ya Shule ya Sekondari Chama ya leo. Askari wa Kijerumani wakawa wakimuuliza maswali Mwanamalundi kuhusu nguvu zake na kisha wakamuomba afanye muujiza wa mwisho kabla hajafikishwa gerezani. Mwanamalundi akawaambia askari kuwa bado ana uwezo mkubwa, hata huo mti waliopumzikia anaweza kuukausha. Aliongea maneno hayo huku akiupigapiga mti huo. Kabla hajamalizia sentensi yake kuwa anaweza kuukausha, mti ulikauka palepale na majani makavu yakaanza kudondoka. Askari wa Kijerumani waliogopa sana tukio hilo.

Walipofika Tabora mjini, Mwanamalundi na wale watemi wawili waliunganishwa na watu wengine wenye makosa ya uhaini na uhujumu uchumi na kisha kupelekwa kisiwa cha Mafia kutumikia kifungo cha miaka mitatu.

Akiwa gerezani, Mwanamalundi aliwekwa chumba kimoja na mtemi Makongoro Igana. Mtemi Makongoro akamuuliza Mwanamalundi, "Hivi huna namna ya kujiokoa mahali hapa?" Mwanamalundi akamjibu kuwa kwa wakati huo hangeweza kujiokoa, ila kuna miujiza ya shoka na maziwa amemuachia mama yake nyumbani. Mtemi akamuuliza, "Una miujiza mingine yoyote?" Mwanamalundi akamwambia Mtemi Makongoro kuwa anaweza kupanda viazi na mihogo na vikavunwa ndani ya dakika kadhaa tu vikawa tayari kabisa kwa chakula. Wakiwa kisiwani hapo, wakakubaliana kwenda bara kisha wakachukue mbegu za viazi na mihogo ili washuhudie miujiza hiyo ya kupanda na kuvuna ndani ya dakika kadhaa.

Kwa kuwa nyakati hizo wafungwa wa visiwani walikuwa wakiachwa huru sababu hawataweza kutoroka, Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walienda mpaka baharini, Makongoro akiwa ameshika jiwe na Mwanamalundi akiwa ameshika fimbo. Makongoro aliporusha jiwe umbali mrefu baharini, Mwanamalundi aliyapiga maji kwa fimbo na kisha maji yakajitenga na kuacha njia mpaka pale lilipotua jiwe. Walifanya hivyo mpaka walivyofika bara. Wakatafuta mbegu za mihogo na viazi na kuonesheana miujiza.

Kila walipokuwa wakitoroka gerezani, waliacha vivuli vyao vilivyoonekana kama watu halisi. Kuna nyakati Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walionekana wakiwa Mwanza au Shinyanga na gerezani pia muda huohuo. Jambo hili liliwachanganya sana Wajerumani.

Walipomaliza kifungo chao walirudishwa nyumbani kwao kwa ndege. Jamii ya Mwanamalundi ilipoona ndugu yao amerudishwa kwa ndege wakaamua kumpa jina jipya, "Ng'wenhwandege", wakimaanisha "aliyerudishwa kwa ndege". Mwanamalundi anaaminika kuwa ndiye Msukuma wa kwanza kupanda ndege.

Wakati anarudishwa nyumbani baada ya kumaliza kifungo chake, mama yake alifurahi sana kwa sababu maziwa hayakuganda kwa miaka mitatu, jambo ambalo lilionesha kuwa huko aliko alikuwa hai. Maziwa yalibaki katika ubora uleule kwa miaka mitatu. Shoka ilianza kuteremka taratibu kwenye ukuta kadiri Mwanamalundi alivyokuwa akikaribia kufika nyumbani. Alivyofika tu, shoka ilikuwa tayari imefika ardhini kuashiria kuwa muda wowote Mwanamalundi atafika hapo. Na ndivyo ilivyokuwa.

Aliporudi mtaani, Mwanamalundi hakuacha asili yake. Aliendelea kucheza ngoma maeneo mbalimbali. Mtemi Masanja ambaye ndiye aliyesababisha Mwanamalundi kunusurika kunyongwa na hatimaye kufungwa, aliamua kumfukuza katika himaya ya utawala wake. Mwanamalundi akaamua kuhamia kijiji kiitwacho Seke kwa Mtemi Mahizi ambako aliendelea kucheza ngoma na kufanya miujiza yake.

Akiwa Seke, wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga; Mwanamalundi alifanya muujiza uliomuongezea heshima kijijini. Wanakijiji waliibiwa ng'ombe wengi sana na Wamasai kutoka Tabora. Wanakijiji wakataka kwenda kufuatilia ng'ombe hao usiku huohuo, jambo ambalo Mwanamalundi alikataa. Mwanamalundi aliwahakikishia wanakijiji kuwa ng'ombe hao wapo salama na watarudishwa salama tu kesho asubuhi na si usiku huo. Wanakijiji walikubali kutokana na kumuamini Mwanamalundi.

Usiku wa siku hiyo, Mwanamalundi akatuma nguvu zake zilizowazingira Wamasai na kisha kuwafanya wasinzie na mifugo hiyo. Hata walipofuatwa asubuhi, walikutwa wamelala fofofo. Wanakijiji wakawaua Wamasai hao na kisha wakarudi na mifugo yao. Mwanamalundi akapewa jina jingine ugenini na kuitwa "Kishosha mang'ombe nga Seke", ikimaanisha "Aliyerudisha ng'ombe za Seke".

Kuna kipindi, Mwanamalundi alivamia pori la Mtemi wa Ng'hung'hu aitwae Chalya ili achimbe mizizi fulani ya dawa. Mtemi Chalya alipata machale kuwa kuna mvamizi katika mapori yake anachimba mizizi ya dawa. Mtemi akaondoka na kuelekea kule ambako machale yalimuelekeza. Ni kweli, akamkuta Mwanamalundi akichimba mizizi ya dawa fulani. Mtemi akamuuliza Mwanamalundi, "Kwa nini umeingia katika utemi wangu bila kunijulisha?" Mwanamalundi akajibu, "Wewe ni mtemi wa watu wote ila mimi ndiye mtemi wa miti yote!" Jibu hilo lilimkwaza Mtemi Chalya ambaye aliamua kurudi kwenye himaya yake kwa ghadhabu na kuwaamuru askari wake wamkamate Mwanamalundi ili aadhibiwe.

Askari wakiwa wameambatana na Mtemi Chalya walipofika porini eneo alilokuwepo Mwanamalundi, hawakumkuta. Badala yake waliwakuta simba wengi wakiwa wamelala eneo hilo. Ilibidi watimue mbio kujiokoa dhidi ya simba hao walioanza kuwafukuza. Walipofika kwenye himaya ya Mtemi wakiwa salama, walimkuta Mwanamalundi amemaliza kula chakula chao na anaondoka. Ilibidi mtemi amuache tu Mwanamalundi aondoke bila kumbughudhi kwa lolote.

Marejeo

  1. [1] Archived 22 Novemba 2018 at the Wayback Machine., tovuti ya gazeti la Mwananchi, 18 Januari 201, iliangaliwa Desemba 2018
  2. Mningo 2015, uk. 50
  3. Joseph L. Mbele, Hero in Sukuma Prose Narratives, makala katika Peek-Yankah 2004

Vitabu

  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ngw'anamalundi kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.