Milki ya Osmani

(Elekezwa kutoka Ottoman)

Milki ya Osmani (pia: Ottomani)[1] ilikuwa dola kubwa lililotawala upande wa mashariki wa Bahari Mediteranea pamoja na nchi nyingi za Mashariki ya Kati kati ya karne ya 14 na mwaka 1922.

Milki ya Osmani mwaka 1683.
Sultani Mehmed Fatih aliyeteka Konstantinopoli mwaka 1453.

Milki ilianzishwa na Waturuki Waosmani ikachukua nafasi ya ukhalifa wa Waabbasi na Milki ya Bizanti.

Mji wake mkuu ulikuwa Konstantinopoli (leo: Istanbul) na mtawala wake mkuu alikuwa Sultani wa Waosmani. Imani rasmi ya milki ilikuwa Uislamu hata kama katika maeneo mengi idadi kubwa ya wakazi walikuwa Wakristo.

Tabaka la viongozi wa kisiasa na wa kijeshi walikuwa Waosmani waliokuwa Waturuki pamoja na mchanganyiko wa Waislamu kutoka sehemu zote za milki yao, hasa Balkani. Kwenye uwanja wa uchumi na utawala Waosmani walitumia sana Wakristo Wagiriki na Waarmenia kutokana na elimu yao.

Chanzo

Milki ilianza kama eneo dogo la kabila la Kituruki katika Anatolia chini ya chifu Osmani I likaendelea kupanuka hasa kwa kutwaa sehemu za milki ya Bizanti upande wa Asia na Ulaya ya Kusini-Mashariki.

Kutwaa kwa Bizanti

Mwaka 1453 Waosmani walitwaa mji wa Konstantinopoli na kumaliza Milki ya Bizanti wakifanya mji kuwa mji mkuu wao.

 
Upanuzi wa milki ya Osmani 1299–1683.

Katika karne ya 16 Waosmani waliendelea kupanua milki yao kwenye Balkani upande wa Ulaya, Kaukazi, Mesopotamia upande wa Asia na katika Afrika ya Kaskazini.

Ukhalifa

Baada ya kushinda Wamamaluki katika Misri, sultani (Selim I) alikuwa pia mkuu wa Makka na Madina akaendelea kujipatia cheo cha khalifa.

Kilele cha enzi yake ilikuwa katika karne ya 16 hadi 17. Mwaka 1683 Waosmani walijaribu mara ya pili kuvamia Austria na kuteka Vienna lakini walishindwa. Kuanzia tukio hilo athira yao katika Ulaya ilianza kupungua.

Mzee mgonjwa wa Ulaya

Katika karne ya 18 nchi za Ulaya zilipita Milki ya Osmani upande wa teknolojia, uchumi na polepole pia jeshi.

Wakati wa karne ya 19 Milki ya Osmani ikaitwa "Mzee mgonjwa wa Ulaya" (pia: "Mgonjwa wa Bosporus") na ilikuwa hasa mashindano kati ya Urusi, Ufaransa, Uingereza na Austria-Hungaria yaliyozuia kushindwa kwake kwa sababu kila nchi kubwa ya Ulaya ilihofia ya kwamba nchi nyingine ingejipatia sehemu kubwa za Milki ya Osmani, hivyo walizuiliana. Lakini nguvu yake iliendelea kufifia.

Kwenye mwisho wa karne ya 19 Masultani walijaribu kutekeleza matengenezo mbalimbali ya muundo wa kisiasa na kiuchumi lakini mabadiliko yalitokea polepole.

Mwisho wa Waosmani

Mwisho wa milki ilikuja katika vita vya mwanzoni wa karne ya 20.

Vita vya Balkani viliondoa karibu nchi zote upande wa Ulaya kutoka utawala wa Waosmani.

Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilimaliza milki hii. Serikali iliamua kuunga mkono Ujerumani na Austria-Hungaria dhidi ya Urusi, Uingereza na Ufaransa.

Mwaka 1918 jeshi na dola vikaporomoka kabisa. Milki ikagawiwa na washindi wa vita. Sehemu za Kiarabu zikawa nchi lindwa za Uingereza na Ufaransa. Katika maeneo yaliyobaki nchi mpya ya Uturuki ikaanzishwa.

Marejeo

  1. Historia Kuu ya Afrika hutumia "Ottomani", umbo linalotokana na matamshi ya Kiingereza ya jina "عثمان", "uthman", labda pia kwa kukosea herufi za Kiarabu "ث th" na " t"; kwa hiyo kumtamka mwanzilishi "Otman"; katika lugha za Kifarsi na Kituruki herufi ya "ث th" ina matamshi ya "s", hivyo "Osmani".

Tazama pia

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Milki ya Osmani kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.