Kwelea Domo-jekundu

Aina ya Ndege
(Elekezwa kutoka Quelea quelea)
Kwelea domo-jekundu
Kwelea domo-jekundu wa mashariki (Quelea q. aethiopica)
Kwelea domo-jekundu wa mashariki (Quelea q. aethiopica)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Aves (Ndege)
Oda: Passeriformes (Ndege kama shomoro)
Familia ya juu: Passeroidea (Ndege kama shomoro)
Familia: Ploceidae (Ndege walio na mnasaba na kwera)
Jenasi: Quelea
Reichenbach, 1850
Spishi: Q. quelea
(Linnaeus, 1758)
Ngazi za chini

Nususpishi 3:

Msambazo wa kukaribia wa kwele domo-jekundu
Msambazo wa kukaribia wa kwele domo-jekundu

Kwelea domo-jekundu (Quelea quelea) ni ndege mdogo wa familia Ploceidae ambaye ni ndege wa porini wengi kabisa duniani. Wanatokea Afrika kusini mwa Sahara nje ya misitu mizito. Wanafanana na kwera lakini hawana rangi ya manjano. Husuka viota vyao kama kwera kwenye miti yenye miiba au miwa au matete.

Nususpishi

hariri

Maelezo

hariri

Kwelea domo-jekundu ni ndege mdogo kama shomoro mwenye urefu wa takriban sm 12 na uzito wa g 15-26. Ana domo kubwa wenye umbo la koni ambalo ni jekundu kali katika madume wanaozaliana, pinki au jekundu iliyofifia katika madume na majike wasiozaliana au machungwa hadi njano katika majike wanaozaliana.

Zaidi ya 75% ya madume wana "kinyago" cheusi cha uso kinachojumuisha paji la uso, mashavu na sehemu mbele ya macho na za koo la juu, zote nyeusi. Mara kwa mara madume wana kinyago cheupe. Kinyago kimezungukwa na mlia ubadilikao wa njano, kutu, nyekundu au zambarau. Vinyago vyeupe pengine hupakana na nyeusi. Rangi hizi zinaweza kufikia koo la chini tu au kupanua kupitia tumbo, na sehemu nyingine za chini ni hudhurungi au nyeupe zenye michirizi myeupe. Sehemu za juu zina michirizi hudhurungi na kahawia inayofuata urefu, haswa katikati ya mwili, na imefifia kwenye msingi wa mkia. Mkia na mabawa ya juu ni kahawia iliyoiva. Manyoya ya kurukia yana ombe kijani au njano. Macho yana pete uchi nyembamba na nyekundu na mboni kahawia. Miguu ina rangi ya machungwa. Nje ya majira ya kuzaliana dume hukosa rangi angavu na ana kichwa kahawiakijivu chenye michirizi myeusi, kidevu cheupe na koo jeupe, na mlia mweupe usioonekana sana juu ya macho. Kwa wakati huu miguu hupata rangi ya nyama. Majike wanafanana na madume yenye manyoya ya kutokuzaliana.

Makinda waliozaliwa hivi majuzi wana domo jeupe na wako karibu uchi wenye majunju ya malaika juu ya kichwa na mabega. Macho hufunguliwa wakati wa siku ya nne, wakati huo huo manyoya ya kwanza yanaonekana. Makinda wakubwa zaidi wana domo lenye rangi ya pembe na kidokezo cha urujuani, ingawa linapata rangi ya machungwa-zambarau kabla ya ubambuaji wa baada ya utoto. Ndege wachanga hubadilisha manyoya miezi miwili hadi mitatu baada ya kuanguliwa, na baada ya hapo manyoya yanafanana na yale ya wapevu wasiozaliana, ingawa kichwa ni kijivu, mashavu meupe, na manyoya yafunikayo mabawa na manyoya ya kurukia yana ombe hudhurungi. Wakati wa umri wa miezi kama mitano hubambua tena na manyoya yao huanza kuonekana kama yale ya wapevu wanaozaliana na wana domo zambarau-pinki.

Nususpishi tofauti zinajulikana na ruwaza tofauti za rangi za manyoya ya dume anayezaliana. Katika nususpishi ya kawaida, Q. q. quelea, madume wanaozaliana ni hudhurungi kwenye utosi, kisogo na sehemu za chini na kinyago cheusi huenea juu kwenye paji la uso. Katika Q. q. lathamii kinyago pia kinaenea juu kwenye paji la uso, lakini sehemu za chini ni nyeupe hasa. Katika Q. q. aethiopica kinyago hakienei mbali sana juu ya domo na sehemu za chini zinaweza kuwa na mng'ao pinki. Kuna tofauti nyingi ndani ya nususpishi na ndege wengine hawawezi kutolewa kwa nususpishi kulingana na muonekano wa nje pekee. Kwa sababu ya uzaanamumo vielelezo katikati ya nususpishi vinaweza kutokea mahali ambapo misambazo ya nususpishi inaingiliana, kama vile huko Ziwa Chadi.

Jike wa fumbwe mkia-mwembamba anaweza kukosewa kwa kwelea domo-jekundu wenye manyoya ya kutokuzaliana, kwani wote ni ndege kama shomoro wenye madomo mekundu yaliyo na umbo la koni, lakini fumbwe ana unyusi mweupe kati ya mlia mweusi kupitia jicho na mlia mweusi hapo juu.

Ekolojia na mwenendo

hariri

Kwelea domo-jekundu huonwa kama spishi ya idadi kubwa kabisa miongoni mwa ndege wa pori duniani, na idadi ya ndege huyu baada ya kuzaliana pengine inafika kadiri ya bilioni 1.5. Spishi hiyo inajilisha haswa kwa mbegu za spishi za nyasi za mwaka mmoja, ambazo zinaweza kuwa bivu au bado kijani lakini bado hazijaota. Kwa kuwa upatikanaji wa mbegu hizi hutofautiana na wakati na mahali, zikitokea wiki kadhaa baada ya mvua kuanza, kwelea huhama kama mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa chakula mwaka mzima. Kula chakula kingi chenye kiwango cha juu cha nishati kunahitajika ili kwelea wapate mafuta ya kutosha kuwezesha uhamiaji mpaka maeneo mapya ya kujilisha.

Wakati wa kuzaliana spishi hiyo huchagua maeneo kama vile nyika zilizo na uoto mwenye miiba (kwa kawaida spishi za migunga na vikwata) chini ya mwinuko wa m 1,000. Wakati wanapotafuta chakula, wanaweza kuruka km 50-65 kila siku na kurudi jioni kwenye makao au viota. Vikundi vidogo vya kwelea mara nyingi hujichanganya na ndege tofauti kama kwera (Ploceus) na kweche (Euplectes), na magharibi mwa Afrika wanaweza kujiunga na shomoro manjano (Passer luteus]]) na mishigi anuwai. Kwelea pia wanaweza kukaa pamoja na kwera, mishigi na mbayuwayu wa Ulaya. Matarajio yao ya maisha porini ni miaka miwili hadi mitatu, lakini ndege mmoja kifungoni aliishi muda wa miaka 18.

Mahusiano na watu

hariri

Kama chakula

hariri

Kwelea domo-jekundu hukamatwa na kuliwa katika sehemu nyingi za Afrika. Karibu na Ziwa Chadi, njia tatu za kitamaduni hutumiwa kukamata kwelea. Wategaji wa kabila la Hadjerai hutumia nyavu za pembetatu zilizoshikiliwa mikononi, ambazo zote zinateua kwelea tu na kuwa ufanisi. Kila timu ya wategaji sita inaweza kunasa ndege takriban 20,000 kila usiku. Kadiri ya kwelea milioni tano hadi kumi hunaswa karibu na N'Djamena kila mwaka, ikiwakilisha thamani ya soko ya takriban US$37,500-75,000. Kati ya Juni 13 na Agosti 21 1994 pekee, kwelea milioni 1.2 walinaswa. Ndege walichukuliwa kutoka kwa makao kwenye miti wakati wa kipindi bila mwezi kila usiku. Manyoya yaling'olewa na mizoga kukaanga asubuhi iliyofuata, kukauka kwenye jua na kusafirishwa kuelekea mjini ili kuuzwa sokoni.

Wasara hutumia nyavu za kusimama zenye matundu madogo sana, huku wavuvi wa Masa na Musgum hutupa nyavu juu ya vikundi vya ndege. Athari za utegaji kwa idadi ya kwelea (karibu ndege milioni 200 katika Bonde la Ziwa Chadi) huonekana kuwa ndogo. Mitego iliyosukwa kwa lugowi (Cynodon nlemfuensis) hutumiwa kutega mamia ya ndege hawa kila siku katika Wilaya ya Kondoa, Tanzania.

Kama msumbufu

hariri

Kwelea domo-jekundu huingia mara nyingi katika mashamba ya nafaka ambapo husababisha uharibifu mwingi, haswa kwani makundi yanaweza kuwa kubwa sana hadi kuunganisha ndege milioni 2 katika kundi moja. Ilhali kila ndege anakula gramu 10 kwa siku, kundi kubwa la kwelea linaweza kumaliza tani 20 za nafaka kwenye siku moja[1]. Kwa hivyo wanachukuliwa kuwa wasumbufu wakubwa wa kilimo katika Afrika Kusini mwa Sahara na mara nyingi huitwa "nzige wenye manyoya wa Afrika".

Serikali za Botswana, Ethiopia, Kenya, Afrika Kusini, Sudani, Tanzania na Zimbabwe zimejaribu mara kwa mara kupunguza idadi ya kwelea. Njia ya kawaida ya kuua wana wa makundi yanayoleta shida ni kwa kupulizia kiuandege fenthion, kilicho fosfati ya kikaboni, kutoka kwa anga juu ya makoloni ya kuzaliana na makao. Huko Botswana na Zimbabwe upulizaji umetekelezwa pia kutoka kwa magari ya ardhini na kwa mikono. Kenya na Afrika Kusini zilitumia bomu za moto mara kwa mara. Kwa kawaida udhibiti huelekezwa kwa kuondoa mashirika ambayo yana uwezekano wa kushambulia maeneo yaliyo rahisi kuharibiwa. Mashariki na kusini mwa Afrika, udhibiti wa kwelea mara nyingi huratibiwa na Shirika la Udhibiti wa Nzige-Jangwa la Afrika ya Mashariki (DLCO-EA) na Shirika la Udhibiti wa Nzige Wekundu la Afrika ya Kati na ya Kusini (IRLCO-CSA), ambayo hufanyia ndege zao zipatikane kwa kusudi hili.

Marejeo

hariri
  1. https://www.africa-newsroom.com/press/fao-in-emergency-response-to-the-outbreak-of-quelea-quelea-birds-in-tanzania?lang=en FAO in emergency response to the outbreak of Quelea quelea birds in Tanzania, tangazo la FAO tarehe 18 Julai 2022

Viungo vya nje

hariri