Senati

(Elekezwa kutoka Seneti)

Senati (pia Seneti kutoka Kiingereza "Senate") ilikuwa baraza kuu katika Dola la Roma.

Jina lake limetokana na neno la Kilatini senes (= mzee), kwa hiyo senati ilikuwa baraza la wazee ("Senatus").

Wakati wa Jamhuri ya Roma senati ilikuwa chombo kikuu cha dola; wakati wa makaisari tangu Augusto umuhimu wake ulipungua lakini kwa muda mrefu makaisari walijitahidi kuheshimu baraza hilo hata kama mamlaka zake zilipungua zaidi na zaidi.

Sheria zilitangazwa kwa jina la senati; wakati wa fitina kati ya senati na mtawala kulikuwa pia na amri za Kaisari zilizotangazwa bila idhini ya senati, lakini kwa jumla makaisari hawakutumia jina "sheria" kwa amri hizo.

Kimsingi senati ilijumlisha wote waliowahi kuwa maafisa wakuu wa dola. Katika utaratibu wa Kiroma maafisa wote walichaguliwa kwa muda wa mwaka mmoja. Wenye vyeo hawakupata mishahara, kwa hiyo walikuwa hasa matajiri walioweza kugombea nafasi hizo. Kwa sababu hiyo senati kama mkutano wa maafisa wa kale ilijumlisha hasa watu kutoka familia za makabaila au familia tajiri nyingine.

Wakati wa Jamhuri ya Kiroma senati ilikuwa na maseneta 100 walioongezeka baadaye kuwa 300. Gaius Julius Caesar aliongeza vyeo hivi hadi wajumbe 900.

Senati ilidumu hadi mwisho wa Dola la Roma. Katika Dola la Roma Magharibi heshima yake ilikubaliwa ndani ya mji wa Roma tu na habari za mwisho wa senati zimepatikana hadi mwaka 600 BK. Katika Dola la Roma Mashariki (Bizanti) senati ilidumu hadi mwisho kabisa, mnamo mwaka 1453, lakini karne za mwisho haikuwa na athira yoyote.

Senati ya Roma ilikuwa mfano kwa nchi nyingi; katika lugha za Ulaya taasisi mbalimbali huitwa kwa jina hili.

Senati kama kitengo cha bunge katika nchi mbalimbali

hariri

Nchi mbalimbali huwa na senati kama sehemu ya bunge ikiwa ni bunge ya vitengo viwili (nyumba mbili au vyumba viwili); hapo "senati" kwa jumla ni jina la "nyumba ya juu".

Katika Marekani "Senati" ni kitengo kimoja cha bunge ikiwa na mamlaka nyingi kuhusu siasa ya nje na kuthibitishwa kwa maafisa wakuu wa serikali. Rais anahitaji kibali cha senati kwa sehemu muhimu za siasa zake. Senati ya Marekani inaweza kusimamisha sheria zilizoamuliwa na Nyumba ya Wawakilishi (sehemu nyingine ya bunge). Senati ina wajumbe wawili kutoka kila jimbo la Marekani wanaochaguliwa kwa muda wa miaka 6.

Sawa na Marekani, kuna "Senati" kama kitengo cha bunge katika Ufaransa, Kanada, Italia (Senato della Repubblica), Rumania, Ucheki, Hispania (Senado), Poland, Ubelgiji, Australia, Kenya na Brazil.

Nchi nyingine zenye bunge la vitengo viwili hazitumii neno "senati", kwa mfano Ujerumani. Nchini Ujerumani "senati" ni jina la vitengo vya mahakama kuu.

Matumizi mengine

hariri

Katika nchi mbalimbali "Senati" ni jina la baraza kuu kwenye chuo kikuu.