David Livingstone
David Livingstone (19 Machi 1813 – 4 Mei 1873) alikuwa mmisionari na mpelelezi kutoka Uskoti katika Afrika ya kusini na kati.
Alijulikana kwa jitihada zake za kupambana na biashara ya watumwa na safari za kati ya Afrika ya Kusini na Tanganyika hadi Kongo.
Maisha
haririUtoto na masomo ya tiba na theolojia
haririLivingstone alizaliwa katika Uskoti katika familia ya Wakristo Wapresbiteri.
Tangu umri wa miaka 10 alifanya kazi katika kiwanda cha nguo pamoja na kuwa mwanafunzi wa shule.
Baadaye alisoma tiba na theolojia kwenye chuo kikuu cha Glasgow.
Mmisionari katika Afrika ya Kusini
haririMwaka 1840 alijiunga na Shirika la Misheni la London (LMS) akatumwa Afrika Kusini. Mwaka 1841 alifika katika kituo cha Kuruman. Kutoka hapa alipewa kazi ya kuanzisha kazi mpya kaskazini ya hapo akaunda vituo vya Mabotsa na Tshonuane.
Mwaka 1844 akamwoa Mary Moffat, binti wa mmisionari mwenzake Robert Moffat. Aliendelea kupeleleza maeneo ya ndani ya bara yasiyojulikana bado na Wazungu akijaribu kujenga uhusiano mwema na viongozi wazawa na kuandaa kazi ya misheni kati yao.
Mwaka 1849 alivuka jangwa la Kalahari hadi kufikia ziwa Ngami. Pamoja na mke na watoto wake alimtembelea chifu Sebituane wa Watswana akaendelea mwaka 1851 hadi mto Zambezi. Alikutana na makaburu walioelekea kaskazini wakitaka kuepukana na utawala wa Uingereza katika kusini. Makaburu hawa waliona misheni kati ya Waafrika kuwa hatari wakamtisha Livingstone, hata mwishowe walichoma kituo na nyumba yake.
Safari za kuvuka Afrika
haririLivingstone alitafuta njia ya usafiri kati ya eneo la Watswana na pwani ya magharibi ya Afrika, hivyo akaanza safari kubwa iliyompeleka hadi Luanda (Angola). Aliporudi alikuwa Mzungu wa kwanza kuona maporomoko ya Victoria Falls mwaka 1855. Mwaka uliofuata alifika Msumbiji alipokuta meli iliyompeleka Uingereza.
Livingstone alipokewa kama shujaa kwa sababu taarifa zake zilisababisha kuchorwa upya kwa ramani za Afrika. Alipata sifa nyingi kama mtaalamu wa jiografia na mpelelezi.
Kitabu chake "Missionary travels and researches in South Africa" kilisifiwa kote. Serikali ya Uingereza ilimpa cheo cha konsuli katika Msumbiji akarudi Afrika.
Hapo alijaribu kufuata mwendo wa mto Zambezi kutoka mdomo wake akafika kwenye mto Shire na Ziwa Nyasa (Malawi).
Safari zilizofuata mwaka 1866 zikampeleka hadi ziwa Tanganyika.
Mwaka 1870 alielekea magharibi kutoka Ujiji akafikia mto Lualaba katika Kongo. Aliporudi Ujiji alikutana na Mwamerika Henry Morton Stanley aliyeongoza msafara wa kumwokoa Livingstone lakini hali halisi Stanley alihitaji msaada na Livingstone aliweza kumsaidia kupitia marafiki zake wazalendo.
Safari yake ya mwisho ililenga kugundua chanzo cha mto Nile. Hapo Livingstone aliaga dunia mnamo tarehe 30 Aprili 1873 katika kijiji cha Chitambo (Zambia).
Watumishi wake chini ya uongozi wa Myao Susi walizika moyo wake palepale wakakausha maiti yake wakaibeba hadi Bagamoyo iliposafirishwa kwa meli hadi Uingereza na kuzikwa London katika kanisa la Westminster Abbey tarehe 18 Aprili 1874.
Ukristo, biashara na maendeleo
haririLivingstone aliona mengi, lakini hasa alishtuka juu ya kiwango kikubwa cha biashara ya watumwa alichoona katika nchi nyingi za Afrika ya kati. Alikuta vijiji vilivyochomwa, maiti za watu waliochinjwa, misafara ya watumwa na masoko ambako watu waliuzwa. Aliona pia ya kwamba mahali pengi watawala walitegemea mapato kutokana na biashara hiyo mbaya.
Hapo alipata wazo alilotangaza katika vitabu vyake la kuwa Afrika yahitaji mabadiliko yanayoweza kufikiwa kwa kusambaza Ukristo, biashara na maendeleo ("Christianity, commerce, civilization"). Aliamini ya kwamba Ukristo utavusha mipaka ya makabila na kujenga uhusiano mpya kati ya Waafrika, biashara italeta aina mpya ya utajiri wa kundoa utegemezi wa mapato ya utumwa na maendeleo kwa ujumla yangeboresha maisha ya watu.
Livingstone alipingwa mara nyingi kwa ujumbe huu kwa sababu hali halisi jitihada zake zilisaidia kukandamiza utumwa lakini ziliweka pia msingi kwa ajili ya ukoloni uliofuata baadaye.
Kumbukumbu ya Livingstone katika Afrika
haririHadi leo kumbukumbu ya Dr. David Livingstone inaheshimiwa mahali pengi pa Afrika. Mahali pafuatapo paitwa kwa jina lake:
- Milima ya Livingstone katika Tanzania upande wa mashariki ya Ziwa Nyasa
- Mji wa Livingstonia katika Malawi
- Mji wa Livingstone katika Zambia
- Kisiwa cha Livingstone katikati ya maporomoko ya Victoria Falls
- Maporomoko ya Livingstone Falls ya mto Kongo
- Mji wa Blantyre (Malawi) umepewa jina lake kutokana na mji Blantyre katika Uskoti alikozaliwa Livingstone
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu David Livingstone kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |